The House of Favourite Newspapers

Tatizo la kupoteza hamu na uwezo wa kushiriki tendo la ndoa!-2

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA…

Wiki iliyopita tuliona ni kwa jinsi gani tatizo la kukosa hamu ya tendo la ndoa linavyowasumbua wengi. ENDELEA…

MATATIZO YA KISAIKOLOJIA

Wanazuoni wa kale waliyaona haya, mwanazuoni Sigmund Freud alizungumzia libido kuwa ni nguvu kubwa au nishati iliyo ndani ya penzi bila mtu mwenyewe kujifahamu na kujikuta ametumbukia kwenye mapenzi kwa kumpenda na kuwa na hamu kubwa ya kuwa na ampendaye.

Pia mwanazuoni huyo anazungumzia hatua mbalimbali za hamu na hisia za mapenzi na kujamiiana zinavyoanza tangu utotoni.

MATATIZO YANAYOATHIRI

Matatizo haya yanahusishwa na vichocheo na kemikali mbalimbali mwilini, ambapo kitaalam tunaita endogenous compounds ambavyo tayari tumevizungumzia kwa kifupi, mfano; homoni na neurotransmitters. Vichocheo na kemikali hizi, pamoja na kusaidia hamu na hisia za ngono, kwa mwanamke humjenga na kumfanya afike kileleni wakati wa tendo na kabla ya tendo atoe majimaji ya kulainisha uke. Endapo hali hii haitakuwepo, huyu mwanamke atalalamika uke kuwa mkavu na kupata maumivu wakati wa tendo.

MATATIZO KATIKA MFUMO WA HOMONI

Homoni au vichocheo vinavyomfanya mwanamke awe na hamu kubwa ya tendo la ndoa ni testosterone. Vichocheo hivi huongezeka mara tu mwanamke anapomaliza hedhi yake hadi siku mbili kabla ya kupevusha mayai. Kipindi cha ovulation ambacho mayai hupevuka testosterone hupungua na ile hamu kubwa ya tendo la ndoa hupungua.

Uwepo wa homoni ya progesterone baada tu ya ovulation husababisha ugumu kwa mwanamke kufikia kileleni. Kwa mwanamke yeyote aliye katika umri wa kuzaa, kiwango cha homoni ya estrogen huwa juu. Hivyo njia yoyote au uwezekano wa kufanya progesterone ipande, hushusha estrogen na kusababisha mwanamke awe na uke mkavu, maumivu wakati wa tendo na kupoteza hamu.

Hali hii huwatokea zaidi wanawake waliofikia ukomo wa uzazi, menopause. Pamoja na kipindi hiki cha ‘menopozi’ kuwa ni cha uzee au utu uzima kwa mwanamke, viwango vya homoni ya estrogen hushuka, lakini homoni au kichocheo cha testosterone hupanda na kumfanya mama mtu mzima kuwa na hamu ya tendo, lakini uwezo wa kulifanya unapotea kutokana na kukosa majimaji ya kulainishia uke.

MATATIZO YA KIJAMII NA KISAIKOLOJIA

Baadhi ya matatizo haya hupunguza hamu na hisia za tendo, uchovu, msongo, migogoro ya kifamilia, kikazi, kimasomo na kimapenzi hupunguza hamu ya tendo.

Matatizo ya kimazingira kwa kiasi kikubwa husababisha mtu kupoteza hamu ya tendo. Mfano; kufanya kazi au kuishi katika maeneo yenye sauti kubwa za muziki na mwanga mkali (bright light), nyakati za usiku hupunguza hamu na hisia za tendo.

MATATIZO MWILINI

Vyanzo vya matatizo haya kitaalam tunaita physical factors, huharibu uwezo wa kupata hamu na hisia kwa wanaume na wanawake, hii hutokana na kupungua kwa vichocheo kutokana na sababu mbalimbali, upungufu huu mfano tatizo liitwalo hypothyroidism husababishwa na kutopata virutubisho vinavyostahili au unatumia baadhi ya madawa, vinywaji au una ugonjwa unaoathiri vichocheo hivi.

Kwa mwanaume, endapo utakuwa unatoa manii mara kwa mara, basi hata kiwango cha homoni ya testosterone mwilini hupungua na kukufanya upungukiwe hamu na hisia za tendo. Hivyo mwanaume anayepiga sana punyeto au anayefanya tendo la ngono mara kwa mara kwa kujilazimisha, mwisho wa siku hujikuta akilalamika kukosa hamu ya tendo ambapo kwa mwanaume uume hukosa nguvu na kujikuta unashindwa kabisa.

Upungufu wa damu mwilini au anaemia ni mojawapo ya vyanzo vya tatizo hili, lakini zaidi kwa wanawake.

Uvutaji wa sigara na matumizi yoyote ya dawa za kulevya na ulevi wa kupindukia, hupunguza sana hamu ya tendo kwa wote. Endapo utatoka katika haya na utazingatia ufanyaji wa mazoezi na kuzingatia tiba hospitalini, basi utarudi katika hali ya kawaida.

USHAURI

Matatizo haya ya kupoteza hamu na hisia za tendo huweza kuepukwa kwa kuzingatia yote tuliyoyaeleza, epuka matumizi ya dawa ya aina yoyote bila ya ushauri wa daktari. Matatizo haya yanahitaji uchunguzi wa kidaktari, kuna mengine yanatibika kwa dawa na mengine ni ushauri nasaha.

Ni kawaida kwamba hamu ya tendo la ndoa kwa mwanaume huwa juu wakati wa balehe hasa katika umri wa miaka kumi na mitano hadi kumi na sita na kuendelea kuwa sawa na kuanza kupungua taratibu katika umri wa kuanzia miaka thelathini, huku hali hiyo ikizidi kupungua kuelekea uzeeni.

Kwa mwanamke ni tofauti kidogo, hamu ya tendo la ndoa mara tu baada ya balehe au kuvunja ungo huwa ya kawaida au isiwepo hadi ichokozwe, lakini huwa juu sana kuanzia umri wa miaka thelathini hadi hamsini wakati huu kwa mwanaume inashuka. Hii ni kutokana na vichocheo vya testosterone kushuka kwa mwanaume na kupanda kwa mwanamke.

Kwa hiyo, kwa wanandoa kuanzia umri huu hasa mwishoni mwa umri wa miaka thelathini, ni vema hekima, busara, upendo na amani vitawale, vinginevyo migogoro itaanza. Kwa mwanaume inashauriwa uanze kupata ushauri wa kidaktari endapo utahisi tatizo na kuzingatia lishe bora na kuepuka ulevi wa aina yoyote.

JINSI YA KUONGEZA HAMU YA TENDO

Jitahidi kupata muda wa kupumzika, hasa umri unapozidi miaka thelathini, lala usingizi wa kutosha zisipungue saa nane, kula vizuri na epuka vinywaji vilivyosindikwa, kunywa maji na juisi asilia.

Pendelea kula vyakula vya asili hasa jamii ya mbegu na mizizi, mazao ya bahari hasa samaki ni wazuri kwani wana testosterone ya kutosha.

Comments are closed.