The House of Favourite Newspapers

True Memories Of My life-47

0

Wiki iliyopita niliishia pale nilipokuwa nikielezea pigo alilolipata meneja wetu, Abdallah Mrisho la kumpoteza kaka yake Dawood Mrisho aliyefariki dunia. Nikaondoka ofisini na Mhariri Mtendaji, Richard Manyota, Mhariri wa Gazeti la Championi Ijumaa, John Joseph, Mhariri wa Gazeti la Risasi Jumamosi, Erick Evarist na Mhariri wa Gazeti la Uwazi, Elvan Stambuli hadi chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Muhimbili ambako nilimkuta Mrisho, tukakumbatiana wote tukalia kwa uchungu, kifo cha Dawood kilikuwa kimemuumiza kila mmoja wetu kwa namna yake. SASA ENDELEA…

Huwa inaniumiza sana pale inapotokea nikazungumza na mtu halafu muda mfupi baadaye akafariki dunia, kifo cha Dawood, kaka yake meneja mkuu wetu, Abdallah Mrisho kilinisumbua sana moyoni mwangu kwa sababu kubwa mbili; ya kwanza ikiwa mtu huyo alikuwa mwema, mkarimu, mwenye hekima na kiongozi, namwita kiongozi kwa sababu nikiwa nyumbani kwa Abdallah Mrisho alipopata bahati mbaya ya kuondokewa na mke wake miaka michache iliyopita, Dawood aliniketisha chini na Mrisho na kusema kwamba sisi hatukuwa marafiki tu au watu tunaofanya kazi pamoja tu, bali ni ndugu.

“Ikitokea mmeshindwa kuelewana katika kazi zenu, niiteni niwasuluhishe!” hayo ndiyo yalikuwa maneno ya marehemu Dawood siku hiyo kwangu mimi na mdogo wake, Mrisho.

Sababu ya pili iliyosababisha niumizwe sana na kifo chake ni kwa sababu nilipata nafasi ya kuhangaika naye usiku huo kabla ya kifo chake hospitalini Muhimbili, akiongea nami na kunieleza jinsi alivyokuwa akisumbuka kupumua! Picha hizo hakika hazitauacha ubongo wangu mpaka naondoka hapa duniani, Mungu ampumzishe Dawood mahali pema peponi mpaka nitakapokutana naye.

Tuliondoka chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kuelekea nyumbani kwa Dawood maeneo ya Tabata jijini Dar es Salaam, ambako watu waliendelea kukusanyika, akina mama wakilia lakini wanaume wengi wakiwa na ujasiri wa kujadili namna mipango ya mazishi ingefanyika!
Uamuzi ulifikiwa na familia kuwa mwili wa marehemu usafirishwe kwenda kwao Bukene mkoani Tabora kwa mazishi, hicho ndicho kilichofanyika siku moja baadaye, bahati mbaya sikupata nafasi ya kumsindikiza Dawood kwa sababu za kifamilia, nikamwomba mdogo wangu, Masha na Richard Manyota ambaye ni Mhariri Mtendaji wa Global Publishers waniwakilishe kwenye maziko hayo.

Kazi za ofisi zikaendelea kama kawaida, jukumu nililokuwa nalo wakati huo pamoja na kazi zangu nyingi za ofisini za kuandika na kuongoza kampuni zilizo chini ya Global Publishers, ilikuwa ni kazi ya kukusanya misaada kwa ajili ya watu wa Ruangwa waliokuwa wameathiriwa vibaya na mafuriko, nikarejea katika shughuli hizo pamoja na kamati nzima niliyokuwa nayo.

Wazo hili la kusaidia watu wa Ruangwa lilinijia akilini siku niliposoma Gazeti la Nipashe ofisini kwangu ambako habari hizo zilikuwa zimeandikwa, sauti ikasikika ndani yangu ikisema “unaweza kuwachangishia watu hawa misaada na wakasaidika!” sikuwa na uhakika ningepata wapi misaada hiyo lakini nikaamua tu kuitii sauti hiyo, nikiamini ilikuwa ni sauti ya Mungu na vitu vyote duniani ni vya Mungu, wanadamu wamepewa tu kuvitunza, mwenyewe akivihitaji mwanadamu huwa hana jinsi isipokuwa kuvitoa, hii ndiyo siku zote huwa imani yangu.

Nilipopiga hatua mbele kidogo tu katika utekelezaji wa jambo hili, nikajikuta nimekutana na watu wengine wengi ambao Mungu alizungumza nao ili kwa pamoja tufanye kazi hiyo ya kutafuta misaada, lakini juhudi zetu zikianzia na sisi wenyewe kuchangia, kampuni yangu ikatoa shilingi milioni nane kwa ajili ya kununua chakula na vifaa vya ujenzi.

Mtu mmoja ninayemkumbuka kwa jina la Aboubakary, ambaye hujishughulisha na biashara ya maduka ya kubadilisha fedha jijini Dar es Salaam na timu ya watu wengine aliowafahamu yeye walitoa tani kumi za chakula, Mohamed Dewji akatoa maji na juisi pamoja na vitenge doti mia mbili kwa ajili ya akina mama wote ambao hawakuwa na makazi kwa wakati huo.

Siwezi kuwakumbuka wote hapa lakini mtu mmoja aitwaye Shubhash Patel, mmiliki wa kiwanda cha chuma cha MMI Steel cha jijini Dar es Salaam alikabidhi mabati elfu nne na misumari kilo mia mbili! Pia nikawa nimepokea taarifa kutoka kwa wenzangu kuwa pia Ubalozi wa Kuwait ulikuwa umekubali kuwajengea wananchi walioathirika nyumba ishirini!

Haikuwa rahisi kuamini kwamba wazo lililoanzia ofisini kwangu tu lilikuwa limezaa matunda yote hayo, nikakubali kwamba Mungu huzungumza na kuwatumia watu kila siku, ila sisi wanadamu ndiyo aidha hupuuza sauti yake au hatujawa bado na uwezo wa kutambua kwamba hii ni sauti ya Mungu anazungumza na kutekeleza yale anayoyasema.

Kwa binadamu wengi bado wanafikiri Mungu akizungumza nao ni lazima iwe kama walivyosoma kwenye vitabu vya dini zao, yaani kuwe na muungurumo wa radi, mwanga mkali ujitokeze kisha atokee mwanadamu mwenye mabawa aliyevalia nguo nyeupe zinazong’ara ambaye atasema “mimi ni Mungu wako, nakuagiza uchangishe misaada kwa ajili ya kuwasaidia watu wa Ruangwa”.

Si kweli, ingawa hata mimi lazima nikiri hivyo ndivyo nilivyokuwa nikiamini siku za nyuma mpaka siku nilipojifunza kwamba Mungu huzungumza nami mara nyingi mno tangu asubuhi hadi ninapokwenda kulala, jukumu langu huwa ni kutekeleza yale ambayo sauti yangu ya ndani huniambia.

Mungu hawezi kukutuma halafu akakunyima msaada, kila anapokutuma ujue jambo hilo litatokea ila yeye kama Mungu asingeweza kushuka hapa duniani na kulifanya, hulazimika kututumia sisi wanadamu kutimiza makusudi yake! Lakini bila kukumbuka kuwa si kila sauti unayoisikia kutoka ndani yako ni sauti ya Mungu, utaipimaje sauti kujua kwamba ni ya Mungu? Hilo ndilo swali ambalo lilinisumbua kwa muda mrefu mpaka nilipoufahamu ukweli.

Sauti yoyote inayokuambia kutenda neno baya si sauti ya Mungu na utajua tu kwamba jambo hili si jema, sauti hiyo achana nayo! Mfano sauti inapokuambia kwenda kuzini, utasikia kabisa ndani yako sauti nyingine ikikueleza kwamba jambo hilo si sawa, hiyo ni sauti ya Mungu na unapotaka kufanya jambo jema kisha ukasikia sauti kutoka ndani yako ikikuonesha udhaifu wako au kukueleza kwamba huwezi, huna sifa, utashindwa, fahamu kabisa kuwa hiyo ni sauti ya shetani na unatakiwa kuipuuza ili usonge mbele.

Nilipopata wazo la kukusanya misaada kwa ajili ya watu wa Ruangwa sikujua kabisa ningekutana na Shubhash Patel atoe vifaa vya ujenzi vya milioni hamsini lakini Mungu alijua kwamba kwa Shubhash kuna vifaa vyangu vya ujenzi ambavyo ninataka viende kuwasaidia watu wangu huko Ruangwa, nilipofika tu ofisini kwake nikiwa na mzee wangu, Hanga na kumweleza kwa nini tulikuwa pale, Mungu alimwambia Shubhash mara moja atoe, naye akafanya hivyo, hivyo ndivyo Mungu wetu anavyofanya kazi.

Nimelazimika kuchukua muda mrefu kidogo kuelezea jambo hili ili watu waweze kujifunza na kwamba kila mmoja wetu anaweza kutumiwa na Mungu, bila kujali elimu, nafasi yako katika jamii, kabila, rangi na dini, sote tunaweza kutumiwa, cha muhimu ni kuisikia sauti ya Mungu na kutekeleza maelekezo yake, nisingetii sauti yake na kwenda kwa Shubhash, mabati yasingepatikana! Wewe unayesoma hapa leo, usijipuuze, Mungu huwa anasema nawe, chukua hatua za kufanyia kazi yote ambayo Mungu anazungumza nawe kila siku, maisha yako yatabadilika na utakuwa msaada mkubwa sana kwa jamii inayokuzunguka.

Siku lori la kwanza lilipoondoka kwenda Ruangwa likiwa na chakula, sukari, maji, sembe, mchele, nilinyanyua mikono yangu juu na kumshukuru Mungu kwa muujiza aliokuwa ametenda! Nachukua nafasi hii leo kutoka ndani kabisa ya moyo wangu kuwashukuru watu wote waliotusaidia, hatujafanya jambo hili kwa faida yetu wenyewe, bali tumemwakilisha Mungu, ofisini kwa Shubhash kuna karatasi ukutani iliyoandikwa maneno “Service to mankind is service to God” yanayomaanisha kumsaidia mwanadamu ni kumsaidia Mungu, hilo ndilo lililofanyika na Mungu amefurahi.

Nawashukuru sana wanakamati wenzangu wote kwa ujumla wao, nimefurahi kukutanishwa nao, rafiki yangu Mr. Kor kutoka Uholanzi naye pia alikuwa sehemu ya kamati yetu, hakujali kwamba yeye ni Mzungu, alitaka kusaidia watu wenye shida maana matatizo hayana kabila wala taifa. Namshukuru pia Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa mama yangu Mariam Mtima, amesafiri mara kadhaa kutoka Ruangwa kuja Dar es Salaam, kilometa zaidi ya elfu moja kuja na kurudi, yote hii ni kwa sababu ya watu anaowatumikia.

Baada ya shughuli hizo, jioni nilirejea nyumbani nikiwa nimechoka, nikapata nafasi ya kuangalia taarifa ya habari ya ITV ambako nilimshuhudia Rais John Pombe Magufuli akihutubia, nikaongeza sauti ili nisikie vizuri, maana hotuba za rais wangu kila zinapotokea huwa ni lazima watu watulie kusikiliza, hakuna mtu huwa anapiga kelele.

Ilikuwa ni kwenye sherehe za Siku ya Sheria iliyofanyika kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam, nilimwonea huruma alipoanza kuzungumza juu ya wizi unaofanyika katika taifa letu huko serikalini, aliongea mpaka akafika mahali fulani akashindwa kuzungumza kwa jinsi suala la vitambulisho vya taifa lilivyomchefua, mwisho akawaomba Watanzania wamwombee.

Nilichogundua ni kwamba rais wangu hatanii, ameamua kwa moyo mmoja kabisa kuwatumikia watu wake, lolote litakalompata limpate, lakini abadilishe maisha ya Watanzania na aoneshe mfano utakaokumbukwa wa utumishi uliotukuka! Kweli? Watu watumie shilingi bilioni 179.6 za wavuja jasho kutengeneza vitambulisho vya taifa tena visivyo na sahihi, visivyotimia milioni mbili? Hii ni aibu.

Jambo pekee ambalo Watanzania tunatakiwa kufanya ni kumuunga mkono Rais wetu John Pombe Magufuli, tuweke kando itikadi zetu na tutangulize uzalendo kwa taifa letu mbele tukiamini kabisa tunakokwenda ni pazuri, hata kama hapa tulipo tunateseka, ASUBUHI NJEMA INAKUJA…

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO, BOFYA HAPA ===>https://www.facebook.com/shigongotz/

 

Leave A Reply