The House of Favourite Newspapers

Unending Love- 58

2

Mapenzi ya dhati aliyonayo Jafet kwa Anna, yanamfanya awe tayari kutoa figo yake moja na kumpa Anna ambaye alikuwa na matatizo ya figo zake kushindwa kufanya kazi. Anaamua pia kukataa kusomea upadri akiamini kwamba akimaliza shule, ataoana na Anna ili waishi kama mume na mke.
Siku zinazidi kusonga mbele huku wawili hao wakizidi kupendana mno. Hata hivyo, licha ya wema wake kwa Anna, wazazi wa msichana huyo wanaanza kumchukia Jafet hasa baada ya kufika nyumbani kwao, kijijini Rwamgasa na kujionea maisha ya kifukara waliyokuwa wanaishi Jafet na wazazi wake. Ili kumtenganisha na Jafet, Anna anatafutiwa chuo nchini Marekani.
Siku zinasonga mbele na baadaye, Anna anajikuta akiwa katika uhusiano wa kimapenzi na kijana kutoka familia tajiri, William. Mapenzi yao yanaendelea na baadaye Anna anaanza kuona dalili zisizo za kawaida. Anapoenda kupima anagundulika ni mjamzito lakini kijana huyo anaonesha kukasirishwa na hali hiyo, anataka wakautoe ujauzito huo.
Anna anaamua kutoroka kurejea nyumbani kwao, Mwanza bila Jafet kujua chochote lakini akiwa anaelekea uwanja wa ndege, anakutana na Jafet katika mazingira ambayo hakuyategemea. Hata hivyo, wanashindwa kuelewana na kulazimisha Anna kuendelea na safari yake. Anapofika Mwanza, wazazi wake wanapigwa na butwaa kubwa kusikia kwamba binti yao alikuwa na ujauzito.
Je, nini kitafuatia?
SONGA NAYO…

“Lakini mume wangu, kwani kukataliwa na baba yake ndiyo kigezo cha kutoa mimba? Kwani sisi hatuwezi kumlea mjukuu wetu?”
“Tatizo siyo hilo pekee mke wangu, mwanao bado mdogo na isitoshe, unajua vizuri kuhusu matatizo yake, unafikiri atawezaje kulea ujauzito wakati afya yake yenyewe bado ni tiamaji tiamaji?” alisema baba yake Anna, kauli ambayo ilimuingia mkewe.
Ni kweli Anna alikuwa kwenye kipindi kigumu mno kwa sababu ili kuendelea kuwa na afya njema, ilikuwa ni lazima kila siku anywe vidonge vya Cyclosporin ambavyo hutumiwa na wagonjwa waliofanyiwa upandikizwaji wa figo ili kuzuia tatizo ambalo kitaalamu huitwa ‘rejection’; kitendo cha seli za mwili kuikataa ogani iliyopandikizwa na kusababisha matatizo kwa mgonjwa.
“Tena umenikumbusha, hivi mwanao anaendelea kutumia dawa kweli?”
“Mh! Hebu ngoja nimuite tumuulize,” alisema mama yake Anna na kupaza sauti kumuita Anna ambaye alipokuja, jambo la kwanza alitakiwa kwenda kuleta kiboksi chake kilichokuwa kikitumika kuhifadhia dawa hizo.
Muda mfupi baadaye, Anna alikuwa amesimama mbele ya wazazi wake akiwa na kiboksi hicho. Kilichowashangaza ni kwamba bado dawa zilikuwa nyingi kuonesha kwamba Anna hakuwa akinywa dawa hivyo kama alivyoelekezwa na daktari, kila mmoja akajikuta akiishiwa nguvu.
“Hivi kwa nini hujipendi mwanangu? Umeshasahau matatizo yaliyokukuta leo unaanza kufanya ujinga uleule tena, una nini wewe?” alisema mama yake Anna huku akioneshwa kuchukizwa mno na tabia hiyo ya Anna kwani hakuwa mtoto mdogo aliyestahili kusimamiwa kwa kila kitu.
“Halafu hiyo midomo yako ina nini? Mbona kama siku hizi unakunywa pombe?” mama yake Anna alizidi kumbana binti yake huyo ambapo ilibidi aeleze ukweli wa kila kitu, kuanzia jinsi William alivyomlewesha na kumuingilia kimwili kwa mara ya kwanza na jinsi walivyoendelea kuwa wanakunywa kiasi kikubwa cha pombe kisha kufanya ngono.
Ilibidi waondoke na Anna haraka na kuelekea Hospitali ya Bugando ambapo waliomba kuonana na daktari aliyekuwa akimtibu siku zote, wakasubiri kidogo na baadaye kupata nafasi ya kuzungumza naye ambapo ilibidi wamueleze kila kitu kuhusu binti yao.
Taarifa hizo zilimshtua hata daktari mwenyewe kwa sababu kutokana na umri wa Anna, isingekuwa rahisi kwake kujifungua salama, ukichanganya na matatizo yake ya figo ambayo bado hayakuwa yamepona kabisa, alikuwa kwenye hatari kubwa.
Kingine kilichozidi kumchanganya hata daktari huyo, ni taarifa kwamba Anna alikuwa akinywa pombe na kutozingatia dozi ya Cyclosporin, dawa ambayo ilikuwa ni lazima anywe kila siku kwa maisha yake yote, kuanzia siku aliyofanyiwa upasuaji wa kubadilishwa figo.
“Hii ni hatari sana, inabidi nimfanyie vipimo vya kina kujua ni kwa namna gani kutokunywa dawa kwa mpangilio na kunywa pombe kulivyoathiri figo mpya aliyopandikizwa,” alisema Dokta Innocent Kashinje huku naye akiwalaumu wazazi wake kwa kushindwa kumsimamia vyema binti yao wakati walikuwa wanajua matatizo yaliyokuwa yanamkabili.
“Unajua mimi najisikia vibaya sana kwa jinsi tunavyolaumiwa na kuonekana kama wote hatuna akili wakati wewe ndiye uliyesababisha yote haya.”
“Jamani mume wangu, mbona kila mara unanitupia mimi lawama?”
“Wewe ndiyo wa kulaumiwa, narudia tena kusema wewe ndiyo chanzo cha yote kwa sababu Anna kwa kipindi kirefu alikuwa kwenye uhusiano salama na Jafet, ukamuona kijana wa watu maskini hana chochote, ukalazimisha aende kusoma nje ya nchi, kama hiyo haitoshi amekuja na mwanaume hapa umempokea kama mfalme eti kisa ni mtoto wa balozi, matokeo yake ndiyo haya.”
“Lakini wakati yote haya yanatokea na wewe si ulikuwepo? Kama ulikuwa unaona nakosea kwa nini hukusimama kwenye nafasi yako kama baba?”
“Mara ngapi nimekukanya lakini ukawa husikii? Tena usiendelee kunichongea mdomo ukaamsha mashetani yangu hapa,” baba yake Anna alikuja juu na kumfanya mkewe awe mpole, wakaendelea kukaa kwenye viti nje ya ofisi ya daktari wakati binti yao akiendelea kuchukuliwa vipimo.
“Kwa nini hujionei huruma Anna?”
“Nisamehe dokta!”
“Siyo suala la kukusamehe, hujanikosea mimi bali unahatarisha maisha yako mwenyewe. Tazama umejisababishia matatizo mengine ambayo muda wowote yanaweza kulipuka upya,” alisema Daktari Kashinje wakati akiendelea kumpima msichana huyo mdogo.
Baada ya kumaliza kazi yake, daktari alimuita baba yake Anna na kuanza kujadiliana naye kuhusu alichokibaini baada ya kumfanyia Anna vipimo.
“Ukiachilia mbali tatizo lake la ujauzito, nimebaini kwamba yupo kwenye hatari kubwa ya kushambuliwa na magonjwa mengine ambayo ni hatari sana kwa mtu aliyepandikizwa figo. Kwanza uzito wa mwili wake umeongezeka, ‘cholestrol’ kwenye damu pia imeongezeka na kuna hatari ya kupata ugonjwa wa moyo sambamba na kisukari.”
“Mungu wangu, sasa itakuwaje daktari?”
“Inabidi awekwe chini ya uangalizi maalum, tufanye utaratibu wa kumuandalia vibali kwa ajili ya kutoa ujauzito kisha baada ya hapo aendelee kuwekwa chini ya uangalizi wa karibu vinginevyo uwezekano wa figo aliyopandikizwa kufeli ni mkubwa sana,” alisema Dokta Kashinje na kusababisha baba yake Anna ajiinamie.
Daktari huyo aliendelea kumsisitiza juu ya umuhimu wa kumsimamia mwanaye kwa karibu ili kuhakikisha hajihusishi kwenye vitendo vinavyoweza kuiweka afya yake hatarini, ikiwemo kujihusisha na mapenzi, kunywa pombe na kutozingatia dozi.
“Nimekuelewa daktari, kwa hiyo si tunaanza na hili suala la kumtoa ujauzito kwanza?”
“Yaah! Hilo ndiyo litakuwa la kwanza na kama nilivyokwambia inabidi kwanza tufuatilie vibali kwa sababu kutoa mimba kisheria ni kosa la jinai isipokuwa kwa sababu za kitabibu ambazo nazo ni lazima zihakikiwe na bodi ya madaktari na kutolewa kibali,” alisema.
Je, nini kitafuatia? Usikose Jumamosi kwenye Gazeti la Risasi Jumamosi.

2 Comments
  1. Majoy says

    Maskini Anna!

  2. mwanaidi says

    Comment. kiukwel haya yanatokea hivyo wazazi tusichagulie wato
    to wetu wachumba

Leave A Reply