The House of Favourite Newspapers

Wabunge stop ‘ganja’

0

msukuma-640x478Mbunge wa Geita Vijijini kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mh. Joseph Kasheku (Msukuma).

Na Mwandishi Wetu, Risasi Jumamosi

DODOMA:Kauli aliyoitoa bungeni hivi karibuni Mheshimiwa Joseph Kasheku (Msukuma), Mbunge wa Geita Vijijini kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya kulitaka bunge kupitisha sheria ya kuruhusu matumizi na biashara ya bangi na mirungi, imeendelea kuwa gumzo kubwa mitaani huku wananchi wakiwataka waheshimiwa hao kuacha matumizi ya mihadarati hiyo.

Katika kauli yake aliyoitoa siku chache zilizopita ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mjini Dodoma, Msukuma alienda mbali zaidi na kueleza kuwa wapo waheshimiwa ambao hupuliza ‘ganja’ na anawajua lakini haiwaathiri chochote hivyo ufike wakati, wananchi nao waruhusiwe kisheria kuitumia.

“Unajua nilishangaa sana kusikia mheshimiwa akitoa kauli kama ile bungeni na kubwa zaidi nilishtuka kusikia eti wapo waheshimiwa nao wanavuta bangi. Ndiyo maana muda mwingine hawa waheshimiwa wanafanya mambo ya ajabu bungeni kumbe zinakuwa siyo akili zao. Kama kweli wapo wanaotumia, waache mara moja kwa masilahi ya taifa,” Ismail Mtafya, Mkazi wa Area C, Dodoma aliliambia Risasi Jumamosi.

“Zitungwe sheria kali za kuwabana waheshimiwa ili kugundua kama wapo wanaovuta bangi kabla ya kuingia bungeni, kama wanavyodhibitiwa madereva walevi. Huwezi kutunga sheria za maana kama wewe mwenyewe umevuta bangi, hawa waheshimiwa waache kufanya masihara kwenye masuala ya msingi yanayohusu mustakabali wa taifa,” Salama Rajabu, mkazi wa Chang’ombe Dodoma alimwambia mwandishi wetu.

Kati ya wasomaji waliohojiwa na gazeti hili, wengi walionesha kukemea vikali tabia ya waheshimiwa kulewa, hasa kuvuta bangi kabla ya kuingia bungeni kwani hiyo ndiyo sababu kubwa inayofanya kuwe na vurugu na matukio ya ajabu ndani ya mhimili huo wa kutunga sheria.

Kabla ya Msukuma, kauli kama hiyo ya kutetea bangi, iliwahi kutolewa pia na Mbunge wa Nkasi, Ally Kessy katika bunge lililopita.

Leave A Reply