The House of Favourite Newspapers

Watoto wenye ulemavu wawamwagia wabunge, mawaziri changamoto zao

0

2.Baadhi ya watoto wenye ulemavu wakiwa kwenye picha ya pamoja na waheshimiwa wabunge na mawaziri nje ya Ukumbi wa Pius Msekwa mjini Dodoma. Baadhi ya watoto wenye ulemavu wakiwa kwenye picha ya pamoja na waheshimiwa wabunge na mawaziri nje ya Ukumbi wa Pius Msekwa mjini Dodoma.

Watoto wenye ulemavu wakiwakilishwa na viongozi wa mabaraza ya watoto wenye ulemavu kutoka mikoa mbalimbali nchini, wamepata nafasi ya kukutana na wabunge ambao ni wajumbe wa kamati ya Katiba na Sheria na kuanika changamoto zao.

Tukio hilo lilichukua nafasi hivi karibuni baada ya watoto hao kwa msaada wa Free Pentecostal Church of Tanzania (FPCT) kupata fursa ya kuhudhuria vikao vya bunge mjini Dodoma kisha baadaye kufanya mkutano ndani ya Ukumbi wa Pius Msekwa uliowajumuisha walezi wao, wabunge na mawaziri.

Wakieleza changamoto zao mbele ya wabunge hao pamoja na mgeni rasmi ambaye ni Naibu Waziri (Ofisi ya Waziri Mkuu) Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu , Abdallah Possi, watoto hao waliweka bayana mambo mbalimbali yanayowapa wakati mgumu katika maisha yao ikiwa ni pamoja na jinsi wasivyopata haki sawa na watoto wengine.

Baadhi ya watoto wenye ulemavu wakiwa kwenye picha ya pamoja waheshimiwa wabunge na mawaziri nje ya Ukumbi wa Pius Msekwa mjini Dodoma.Baadhi ya watoto wenye ulemavu wakiwa kwenye picha ya pamoja waheshimiwa wabunge na mawaziri nje ya Ukumbi wa Pius Msekwa mjini Dodoma.

Akisoma risala akiwawakilisha watoto wenzake, Kaimu Mwenyekiti wa Baraza la Watoto Wenye Ulemavu Tanzania, Wilfred Wilbert alisema kwanza anawashukuru FPCT kwa namna ambavyo wameweza kuwasaidia kuwaweka pamoja, kutambua na kuzidai haki zao za msingi.

“Mabaraza ya watoto wenye ulemevu yametuunganisha na kutupa wakati mzuri wa kujadili pamoja changamoto zinazotukabili katika mikoa yetu, tumekuwa tukipaza sauti zetu na hata wakati mwingine kushirikiana na viongozi mbalimbali kuwaanika wale ambao wamekuwa wakificha watoto walemavu.

“Changamoto tunazopitia zinazokwamisha malengo yetu ni nyingi lakini nipongeze serikali ambayo kwa namna moja ama nyingine kupitia sauti zetu wamekuwa wakifanyia kazi mambo kama vile miundombinu,” alisema mtoto huyo.

Naye Mhazini wa Watoto Wenye Ulemavu Mkoa wa Tabora, Mpaji Nicolaus alipata nafasi ya kueleza changamoto zinazowakumba ikiwa ni pamoja na ukosefu wa fedha za kuendeshea vikao vya mabaraza na kusafirisha watoto kutoka sehemu moja hadi nyingine pamoja na vifaa vya kutunzia ‘dokyuments’.

“Serikali itenge bajeti maalum kwa ajili ya pesa za kuendesha mabaraza haya. Lakini pia wadau mbalimbali wajitokeze kusaidia mabaraza haya. Kompyuta za kutunzia nyaraka mbalimbali za mabaraza haya ni tatizo pia,” alisema Mpaji.

 Naye, Christina Majugwe ambaye ni Katibu wa Baraza la Watoto Wenye Ulemavu Taifa alizitaja changamoto nyingine zinazowakabili watoto wenye ulemavu kuwa ni kutotekelezwa kwa sheria, sera, taratibu na miongozo inayowahusu wao, hali inayopelekea kujihisi wametengwa.

 “Tunawaomba waheshimwa wabunge mtusaidie katika kuishauri serikali ili hizi sheria zinazotuhusu sisi ziweze kufanya kazi kuanzia ngazi ya chini hadi juu,” alisema mtoto huyo.

Akizungumzia changamoto ya fedha kwa ajili ya kuwasaidia watoto walemavu, Mbunge wa Jimbo la Mlalo, Rashidi Shangazi alisema kuwa, ni vyema kukawepo fungu maalum kutoka serikalini la kuwasaidia watoto hao badala ya kutegemea wasamaria wema.

“Tusiwasaidie watoto hawa kwa staili ya mwenye nacho atoe, kuna suala la kuchoka na kwamba wanaowasaidia wanaweza kuchoka na watoto hao wakabaki kwenye mazingira magumu. Kuwepo na mfumo maalum wa kuwawekea mfuko wao wa fedha za kuwasaidia,” alisema Shangazi.

Mbunge huyo pia akatumia fursa hiyo kuwapongeza FPCT kwa kazi ya kiroho ya kuwasaidia watoto hao na akamtaka Waziri Possi kuangalia njia nzuri ya kuwasapoti ili waweze kufikia malengo yanayotakiwa.

“Hizi jitihaza hazitakiwi kuachwa kwa kanisa. Mifuko ya hifadhi ya jamii iwaangalie watoto hawa. Naahidi nitakuwa mbunge maalum wa kuwatetea sehemu yoyote.”

Naye Mbunge wa Tabora Mjini, Emmanuel Mwakasaka alisema kuwa, watoto hao walemavu wanatakiwa kuchukuliwa kama watoto wengine kwa kuhakikisha wanapatiwa haki zao za msingi na kikubwa elimu iendelee kutolewa ili watu wajue umuhimu wa kuishi nao vizuri.

“Wakati tunaangalia jinsi ya kuwasaidia, nyie wenyewe muwe wamoja, mpendane, msibaguane ili iwe rahisi kwa jamii kuwasaidia.”

Alipopewa nafasi ya kusema chochote, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Eng. Stella Manyanya kwanza aliwapongeza FPCT kwa kazi kubwa wanayofanya katika kuwasaidia watoto wenye ulemavu lakini pia akiahidi kuzifanyia kazi changamoto zote zinazoihusu wizara yake.

“Najua kuna changamoto za kutokuwepo na vifaa vya kutosha vya kufundishia kwa watoto wenye ulemavu na idadi ndogo ya wakalimani ila niseme tu kwamba wizara yangu katika bajeti imetenga fedha kwa ajili ya mitaala ya kuwawezesha walemavu kupata fursa kulingana na mahitaji yao.

“Pia  tutahakikisha vinapatikana vitabu vitakavyowawezesha watoto kujifunza vizuri. Kwa kifupi changamoto zote tumezichukua na tutazifanyia kazi,” alisema Waziri Manyanya.

Naye Waziri Possi alipozungumza na watoto hao alionesha kuwaunga mkono kwa jitihada zao za kutetea haki zao na akawataka kuendelea hivyo hivyo huku akiahidi kuwaunga mkono katika kila wanachokifanya.

“Vipaumbele maalum vitakuwepo ili watu wenye ulemavu waishi vizuri. Niseme tu kwamba serikali itafanya kila inaloweza kuhakikisha changamoto zinazowakabili zinafanyiwa kazi,” alisema Possi.

Akiizungumzia ziara hiyo, mratibu wa mpango wa kuwasaidia watoto wenye ulemevu kutoka FPCT, Lucas Mhenga alisema watoto waliobahatika kukutana na wabunge walifarijika sana na walitumia fursa hiyo kueleza changanoto zao wakiamini wao wanayo nafasi kubwa ya kuwasaidia.

 “Ilikuwa ni ziara yenye mafanikio makubwa, watoto walipata nafasi ya kueleza changamoto zao lakini kile kitendo cha wabunge kuacha majukumu mengine na kutumia muda wao kuwasikiliza, kimewapata faraja kubwa.

 “Tunaamini yale waliyoyaongea yatafanyiwa kazi ili watoto hawa ambao kwa muda mrefu jamii imekuwa ni kama imewatenga waweze kuishi maisha mazuri kama wanavyoishi watoto wengine,” alisema Mhenga.

Leave A Reply