The House of Favourite Newspapers

Magufuli Aapishwa Rais Tanzania – Video

0

ALIYEKUWA rais mteule wa Tanzania Dkt. John  Magufuli ameapishwa rasmi leo Novemba 5, 2020, jijini Dodoma katika Uwanja wa Jamhuri baada ya kushinda uchaguzi wa urais katika uchaguzi mkuu uliofanyika tarehe 28 Oktoba, 2020.

 

Sherehe hizo zimehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa na kimataifa wakiwemo Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Mwinyi, marais wastaafu wa Tanzania, Dkt. Jakaya Kikwete na Ali Hassan Mwinyi, mawaziri wakuu wastaafu wa Tanzania, Edward Lowassa, Jaji Warioba, Spika Job Ndugai, Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, wakiwemo baadhi ya marais wa nje, mawaziri waliomaliza muda wao, wabunge wateule na viongozi waandamizi wa serikali.

 

“Siku kama ya leo Novemba 5, 2015, niliapishwa kuliongoza taifa letu kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita, leo tena nimeapishwa kuliongoza taifa letu kwa miaka mitano ijayo.  Namshukuru sana Mungu. Uchaguzi sasa umekwisha… uchaguzi sasa umekwisha… uchaguzi sasa umekwisha, jukumu kubwa lililopo mbele yetu ni kuendeleza jitihada za kujenga na kuleta maendeleo kwa taifa letu na niwahakikishie kuwa kiapo nilichoapa na alichoapa makamu wangu, tutahakikisha tunakienzi kwa nguvu zote.

 

“Tofauti na 2015 ambapo niliapishwa jijini Dar es Salaam, kwenye Uwanja wa Uhuru, mara hii nimeapishwa katika Uwanja wa Jamhuri, nashukuru sana nimekuwa rais wa kwanza kuapishwa kwenye jiji hili zuri la Dodoma. Kitu cha kwanza tutaanza na kujenga uwanja mkubwa hapa Dodoma ili sherehe nyingine zitakazokuja watu wote wawe wanashangilia ndani ya uwanja.

 

“Ushindi huu si wa CCM peke yao, ni wa Watanzania wote, naipongeza sana Tume ya Uchaguzi (NEC) kwa kusimamia vizuri zoezi la uchaguzi wa mwaka huu, nawashukuru viongozi wa dini kwa kutuongoza vyema katika kipindi chote cha uchaguzi.

 

“Nawapongeza pia wabunge wote na madiwani wote waliochaguliwa na bahati nzuri mwaka huu wengi wanatoka CCM nawashukuru wana Dodoma kwa kuhudhuria kwa wingi, hii pia imedhihirisha kuwa Dodoma ndiyo makao makuu ya nchi.

 

“Bado tunayakumbuka tuliyoahidi katika ilani yetu ya uchaguzi ya CCM yaliyoandikwa katika kurasa 303. Tutaendelea kudhibiti rushwa, wizi na ubadhirifu wa mali za umma. Niwakumbushe tu kuwa mwisho wa uchaguzi huu ndio mwanzo wa uchaguzi ujao,” amesema.

Leave A Reply