The House of Favourite Newspapers

Vijana Msiache Sifa ya Ujasiri Iwe ya Paul Makonda Peke Yake

HADITHI: Na Eric Shigongo | IJUMAA WIKIENDA| KUMBUKUMBU ZA KWELI ZA MAISHA YANGU

ILIKUWA ni wiki ya hekaheka, vyombo vyote vya habari vilikuwa vimeelekeza macho yake kwa Yusuf Manji, si kwa vita dhidi ya dawa za kulevya tena! Najua sheria zipo, lakini mimi naomba nikiri bila unafiki, sikuwahi kufikiria hata siku moja kwamba mtu mwenye utajiri mkubwa kama Manji eti siku moja angeweza kulala selo. 

Kwa ushawishi mkubwa aliokuwa nao katika tawala zilizopita, akiwa mwenyekiti wa klabu kubwa ya mpira wa miguu ya Yanga, yenye uhusiano wa karibu na Chama Cha Mapinduzi (CCM), pia Diwani wa Kata ya Mbagala-Kuu jijini Dar es Salaam, haikuwa rahisi Yusuf Manji kumweka ndani! Ndiyo maana wiki iliyopita nililazimika kumwamkia mdogo wangu Makonda, kwani alikuwa amefanya jambo ambalo watu wengi huko nyuma liliwashinda.

Siku nane, Manji alikuwepo mahabusu, narudia tena, MAHABUSU, akipekuliwa nyumbani na ofisini kwake na pia kupelekwa kwa Mkemia Mkuu kupimwa kuona kama alikuwa mtumiaji wa dawa za kulevya au la! Nilijiuliza maswali mengi sana kichwani mwangu, ni dawa za kulevya tu au kuna lingine? Hata hivyo, nikachagua kubaki kimya niache shughuli iendelee, moyoni mwangu nikitamani sana kukutana na Manji ili nimpe ushauri kama kuna jambo alikuwa amelifanya dhidi ya utawala ambalo huku nje lilikuwa halifahamiki basi nimshauri ajishushe, hata kama ni bilionea kwani hakuna mwenye fedha popote pale ulimwenguni aliwahi kushindana na utawala akashinda vita.

Yusuf Manji akiwa na maaskari kanzu

Barack Obama hakuwa bilionea, lakini mabilionea kama Marc Zukerberg, Warren Buffet, Bill Gates na wengineo wengi hawakuwahi hata siku moja kushindana naye, walimtii na kumheshimu pamoja na mabilioni yao kwa sababu walijua mamlaka ilikuwa na nguvu kuliko utajiri! Simaanishi kuwa yanaendelea dhidi ya Manji, ni mashindano kati ya fedha na utawala, nawaza tu, kama binadamu ikiwa kuna jambo la namna hiyo basi Manji hana jinsi zaidi ya kushuka na kunyenyekea au kuwafanya watawala waelewe tafsiri nyingine vichwani mwao tofauti na inayoweza kuwa imejengeka.

Kumbukumbu zangu kichwani zinanikumbusha juu ya bilionea mmoja huko Urusi aitwaye Mikhail Khodorkovsky, huyu alijaribu kupambana na utawala wa Rais Vladimir Putin ambaye hakuwa bilionea zaidi ya kuwa na mamlaka tu, naweza kusema bilionea huyo alikuwa tajiri kuliko Yusuf Manji lakini mwisho wa siku alinyoosha mikono kwa Putin na akaishia gerezani, hii inathibitisha kwamba mamlaka siku zote yanaposhindana na utajiri, yenyewe ndiyo huibuka mshindi.

Narudia tena, simaanishi kwamba kinachoendelea hapa nchini ni mapambano dhidi ya tajiri Manji, la hasha! Maana waliokamatwa na kuhojiwa kwa dawa za kulevya si yeye peke yake, ni wengi, lakini ninachosema ni kwamba kama kauli zake za “Makonda ni mdogo wangu tu…” zimetafsiriwa na utawala kama dharau basi kuna jambo la kufanya kwa walioshikilia mpini.

Binafsi naomba niseme wazi, ninamheshimu Paul Makonda tangu siku ambayo Rais John Pombe Magufuli alitamka kwamba Makonda ndiye mwakilishi wake katika Mkoa wa Dar es Salaam, kamwe siwezi kumwonesha dharau hata siku moja! Lakini ndugu zangu naomba nisisitize kuwa NAMHESHIMU MAKONDA, SIMUOGOPI na kama Makonda anapenda kuogopwa badala ya kuheshimiwa basi mimi si miongoni mwa watu watakaomuogopa.

Ni kweli nimeshuhudia Makonda anavyokua kisiasa, hata yeye anafahamu, sina sababu ya kuyataja yote ambayo mimi na Makonda tumewahi kushauriana au kufanya kwani najua wapo watu ambao wametoa mchango mkubwa kwa Makonda kuliko mimi!

Ninachotaka kusema hapa ni kwamba hata kama namfahamu Makonda kiasi gani, lazima sasa nimheshimu kwani ni kiongozi wangu, wala sitafanya naye mashindano labda tu pale atakapotaka kunionea au kunigandamiza kwa sababu yeye ni Mkuu wa Mkoa na Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Dar es Salaam, mmiliki wa polisi wote na Usalama wa Taifa.

Februari 16 nilishuhudia kupitia Global TV Online, Yusuf Manji akipandishwa kizimbani kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akishtakiwa kwa kosa la kutumia dawa za kulevya aina ya Heroine! Mahakamani ndiko haki hutolewa, nikachagua kutulia nishuhudie ambacho kitatokea baadaye, kwani hakuna mtu aliye juu ya sheria au mwenye uwezo wa kuiamuru mahakama ifanye apendandavyo, hata rais wa nchi hana uwezo wa kuiingilia mahakama.

Kelele za Masongange aliyewahi kukamatwa na dawa za kulevya huko Afrika Kusini na baadaye kuachiwa ambaye alipigiwa kelele sana na Msanii Wema Sepetu kwamba ni kwa nini alikuwa hajakamatwa, hatimaye zikafika mwisho pale msichana huyo alipokamatwa siku ya Februari 15 na kupelekwa kwa Mkemia Mkuu kupimwa damu ili kuona kama alikuwa akitumia dawa za kulevya au la! Alitarajiwa kufikishwa mahakamani siku ya Ijumaa ya Februari 17 lakini hakupelekwa pamoja na ndugu zake kujazana wakimsubiri.

Ndugu zangu, Maumbile yangu hayaniruhusu kukaa kimya ninapoona jambo fulani haliendi vizuri, vivyo hivyo jambo zuri linapofanyika ninayo haki ya kupongeza, eneo pekee la kukaa kimya ni pale nitakapotakiwa kutoa sifa au pongezi zisizostahili au kukosoa pasipostahili, kukosolewa eti sababu tu aliyestahili pongezi si mwenzangu.

Naomba niseme ukweli, pamoja na yote yanayoendelea katika mitandao ya kijamii dhidi ya Makonda, mimi naomba niseme Makonda ni JASIRI, kitu ambacho ni kigumu sana kukikuta ndani ya mioyo ya vijana wetu hasa katika mazingira ya sasa ambayo vijana wamejazwa hofu, hawawezi kuzungumza wanavyojisikia, kabla hawajawaza au kusema chochote lazima wageuke huku na kule au kumwangalia mtu aliyeko mbele yao kama harekodi.

Lazima tukubali kwamba ni Makonda aliyesababisha nchi yetu iingie kwa nguvu kubwa katika vita dhidi ya dawa za kulevya, bila ujasiri wa Makonda kufanya alichokifanya nina uhakika Baraza la Taifa la Kudhibiti Dawa za Kulevya lenye idadi kubwa ya mawaziri ambalo kisheria lipo chini ya Waziri Mkuu, lisingeingia kazini hivi karibuni kama ilivyotokea.

Mnyonge mnyongeni, haki yake mpeni! Jana nilipopata nafasi ya kuzipitia upya baadhi ya video ambazo Mheshimiwa Makonda amewahi kuzitoa siku za nyuma akiwa pale UVCCM kuwashambulia Edward Lowassa na Rostam Aziz, nilikiri moyoni mwangu kuwa Makonda ni JASIRI na ni ujasiri wake ndiyo uliomfikisha alipo leo, bila shaka kama hatakuwa mnafiki mahali fulani Makonda ni lazima akiri kwamba mtu aliyekuwa akimvutia sana katika siasa ni Nape Nnauye ambaye pia ujasiri ulimsaidia sana kufika alipo leo.

Mwalimu Nyerere alikuwa JASIRI, Nelson Mandela alikuwa JASIRI, Mahatma Gandhi alikuwa JASIRI, Jomo Kenyatta alikuwa JASIRI! Kwame Nkrumah alikuwa JASIRI, Che Guevara alikuwa JASIRI, vivyo hivyo Fidel Castro, kama hivyo ndivyo basi tukubaliane kwamba UJASIRI ndiyo njia pekee inayoweza kumfikisha mwanadamu, hasa mwanasiasa, mwanamapinduzi kwenye kilele cha mafanikio yake, si uoga na hofu! Vitu hivi viwili vinaweza kumfanya mtu awe mtumwa katika nchi iliyo huru.

Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa, Makonda anafahamu kabisa kuwa ni UJASIRI uliomfikisha hapo alipo, nilichokitarajia kutoka kwake baada ya kuwa amefika juu ni kuanzisha kampeni za kupanda mbegu za UJASIRI katika mioyo ya vijana wa taifa hili, tofauti na matarajio yangu ninachokishuhudia ni juhudi za Mheshimiwa Makonda kujaribu kutengeneza hofu mioyoni mwa vijana wa Kitanzania.

Kama nilivyosema huko juu, nitasifia mahali pa kusifia, lakini nitakosoa mahali pa kukosoa bila woga! Sifurahishwi sana na tabia ya Mheshimiwa Makonda ambaye UJASIRI umemfikisha mahali alipo bila kufanywa chochote, bila kuwekwa ndani saa arobaini na nane, bila kufukuzwa katika Mkoa wa Dar es Salaam, yeye leo kwenye hotuba zake anasimama na kututishia kwamba ana uwezo wa kutuweka ndani na hata kutufukuza kwenye mkoa wake! Najiuliza sana nini lengo la Makonda anapotumia kauli hizi?

Anataka tuingiwe na hofu ya kuwekwa ndani au kufukuzwa Dar es Salaam? Je, Makonda alitaka yeye peke yake ndiye awe kijana wa mwisho katika taifa hili kuitwa JASIRI? Kama yeye aliweza kunyanyuka wakati ule na kumkemea Lowassa na Rostam ni kwa nini anatengeneza hofu ndani ya vijana wetu? Hataki vijana wengine nao wanyanyuke na kumkemea yeye ndani ya taifa pale atakapokwenda kinyume?

Awaache vijana wetu wawe JASIRI kama alivyokuwa yeye, hatutaki kutengeneza taifa la wanafiki, watu wasioweza kuzungumza yaliyoko mioyoni mwao kwa hofu kwamba baadaye wanaweza kupambana na mkuu yeyote, wakajikuta mahabusu au wanafukuzwa kwenye mkoa wa mkuu! Watu watakapotafsiri kwamba mkuu wa mkoa anatumia sheria zilizopo, nyingine zilitungwa wakati wa ukoloni kuwakomoa watu atachukiwa, atatengwa na jamii anayoiongoza, hivi ndivyo imekuwa miaka yote tangu kuumbwa kwa dunia. Misingi ya taifa hili ilijengwa katika kuongea ukweli bila hofu na hivyo ndivyo tunavyotaka taifa letu liwe, leo hii kila unakopita mioyo ya watu imejaa hofu kauli kama hizi za Makonda zinafanya watu waogope kuongea yaliyomo mioyoni mwao.

Hapo ndipo taifa letu lilipofika, watu hawazungumzi maumivu yaliyomo mioyoni mwao, ukiwatazama usoni huonekana wanatabasamu lakini vifuani wamejaa chuki, hii ni mbaya. Ushauri wangu kwa mkuu wa mkoa ni kubadilisha mtindo wa kutuongoza, awe na moyo mpana, mvumilivu na mwenye subira! Hata kama watu wangemtukana vipi mtandaoni, aelewe tu kwamba ukubwa ni jalala na yeye si mtu wa kwanza kutukanwa, inafanyika hivyo hata kwa viongozi wakubwa kuliko yeye, atulie na atuongoze kwa upendo si vitisho vinavyoua UJASIRI ndani ya mioyo ya vijana wetu.

Tukitengeneza taifa la watu waoga, wasiozungumza yaliyomo mioyoni mwao kwa sababu ya hofu ya kuadhibiwa, si kwamba hawataongea kweli bali sauti zao zitapita chini ya kwapa kwa miaka mitano na siku ya mwisho watakuja kuyaongea yote yaliyokuwa vifuani mwao kwenye boksi la kupigia kura, tutakuwa tumechelewa.

Nilizaliwa Tanzania, nikakulia Tanzania, nawafahamu vizuri sana Watanzania wenzangu, wana tatizo la kutokuwa wakweli, wanaweza kukuonesha meno ukadhani wanacheka, wakapiga magoti kukusalimia ukadhani wanakuheshimu, wakapiga makofi ukadhani wanakushangilia, lakini siku Mungu akikufungulia vifua vyao na kujua yaliyokuwemo mioyoni mwao utagundua kumbe halikuwa tabasamu, haikuwa heshima na haukuwa ushangiliaji, ilikuwa chuki.

Mbunge mmoja huko Kanda ya Ziwa, nisingependa kumtaja jina alifanya kila lililo jema kwa wapiga kura wake, akajenga hospitali, akatengeneza barabara, akasaidia wasiojiweza na kila alipopita watu walimshangilia, cha kushangaza uchaguzi ulipokuja alishindwa vibaya, alipopeleleza kutaka kujifunza kwa nini ameshindwa alipata jibu rahisi tu “alikuwa hasikilizi wala kusalimia wala kukaribia watu, kila alipopita na gari lake vioo vilikuwa vimefungwa!” jambo hilo peke yake likafanya apoteze ubunge, kumbe angewasikiliza watu angejua mapema na kulifanyia kazi. Hebu tujiulize, pamoja na kazi nzuri ya kupambana na dawa za kulevya anayoifanya Mheshimiwa Makonda, je, kwenye boksi la kupigia kura kama angekuwa anagombea ubunge leo hii jimbo lolote, ingekuwaje?

Dawa ya jambo hili ni kuacha kuwaogopesha, kuwatisha watu na kuwaondolea ujasiri wa kujieleza, bali viongozi akiwemo Makonda wawe tayari kuwasikiliza wananchi kwa upendo, bila kuwatia hofu, watakapoongea ndipo tutajua maumivu yao ila tukiwaogopesha tu watanyamaza na wataongea siku watakaposimama mbele ya boksi la kupigia kura.

Njia ya kulifanya jambo hili ni kauli tu, viongozi wetu kama Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam lazima wajifunze kuchagua kauli za kuzungumza mbele za watu, nyingine zinatisha na kuogofya! Lakini mimi nasema wazi, nakataa kuogopa, nakataa kujazwa hofu, nitazungumza yaliyomo moyoni mwangu ilimradi sivunji sheria, maana uhuru wa kujieleza ni haki yangu ya kuzaliwa kama mwanadamu, nimalizie kwa kusema;VIJANA MSIACHE SIFA YA UJASIRI IWE YA MAKONDA PEKE YAKE.

Comments are closed.