The House of Favourite Newspapers

Dondoo Muhimu Katika Kuyasaka Mafanikio!

Na AMRANI KAIMA| GAZETI LA IJUMAA| SAIKOLOJIA, MAISHA NA WEWE

MPENZImsomaji wangu, mafanikio ni kitu ambacho kila mtu anatamani kukipata katika maisha yetu. Mishemishe zote zinazofanywa na binadamu hapa duniani, lengo ni kutafuta mafanikio ambayo yatamfanya aishi kwa amani na furaha.

Huwezi kuwa na furaha maishani mwako kama huna uwezo wa kujipatia mahitaji muhimu wala huna ziada ya kuwasaidia ndugu zako. Pia huwezi kuwa na amani kama kila unayofanya yanakwama na mwanga wa mafanikio huuoni.

Ndiyo maana tuna kila sababu ya kuhakikisha tunapambana ili tufanikiwe. Yapi ya kuzingatia sasa ili uweze kufanikiwa? Dondoo hizi hapa chini zitakusaidia sana.

EPUKA NJIA ZA MKATO

Jaribu kufanya kila jambo linalowezekana katika kutafuta mafanikio. Usitumie njia za mkato, tafuta njia halali itakayokufikisha kule unakotaka kufika.

PAMBANA

Katika kuhangaika kwako kutafuta mafanikio, utakutana na vikwazo vingi, usirudi nyuma, wewe songa mbele tu. Kuwa kama mwanajeshi anapokuwa mstari wa mbele vitani, hakuna kurudi nyuma.

CHAGUA WASHAURI SAHIHI

Si kila mtu atafurahi kukuona unafanikiwa hivyo unatakiwa kuwa makini katika kuchagua watu au marafiki wazuri wa kukushauri juu ya mipango yako. Lakini pia unaposhauriwa nawe uwe na akili yako binafsi. Ushauri mzuri chukua na ule usiofaa achana nao.

JIELIMISHE

Elimu ni nyenzo ya kukurahisishia kufika kule unakotaka kufika kwa kukuwezesha kuona fursa mbalimbali. Elimu si lazima iwe ile ya darasani, hata ile ya nje ya darasa inafaa ilimradi tu ikupe mwanga na uwezo wa kuona fursa na kujua namna ya kuziendea.

PESA ISIWE KIKWAZO

Pesa ni kikwazo kwa watu walio wengi katika kutafuta mafanikio. Ili utimize malengo yako unahitaji kwanza pesa. Sasa vipi utaweza kuzipata wakati taasisi za kifedha hazikopeshi watu wasio na dhamana kama wewe? Utaipataje pesa wakati hakuna taasisi za wazi za kuwapa sapoti wajasiriamali wachanga?

ANZA NA KIDOGO ULICHO NACHO

Ushauri mzuri ni kwamba, kidogo ulichonacho anza nacho hichohicho hata kama ni kwa biashara ndogo. Wahenga walisema, ndondondo si chururu. Jifunze kujiwekea
akiba kidogokidogo.

Usichague kazi ambayo unaamini inaweza kukuingizia pesa.

ISHU YA VIKOBA

Mahali ulipo unaweza kuanzisha vikoba au kitu kama hicho kwa kuwashirikisha vijana wenzako wenye hamu na mafanikio. Mara kwa mara jiwekeeni akiba na kisha mkopeshane wenyewe kwa wenyewe.Kama una ujuzi wowote hakikisha unautumia vizuri, unaweza kuwa mkombozi wako. Tafuta kipawa chako. Jiulize ni kitu gani unaweza kukifanya kwa ufanisi? Ukikibaini, jibidishe kwenye hicho mwishowe kitakusaidia katika kupiga hatua za kuelekea kwenye mafanikio.

VUMILIA

Vumilia mazingira magumu utakayokuwa unakumbana nayo, kila siku muombe Mungu akuongeze katika njia iliyonyooka na vile vizingiti utakavyokuwa unakumbana navyo akusaidie uweze kukabiliana navyo na kuvivuka.

USIKATE TAMAA KABISA

Tambua kwamba, mpaka kuyafikia mafanikio ni lazima utakuwa unakumbana na changamoto nyingi, huna sababu ya kukata tamaa. Pambana bila kuchoka na amini kuna siku mambo yatanyooka. Kumbuka hata mtoto ili aweze kusimama na kukimbia ni lazima awe ametambaa sana, baadaye akajaribu kushika mahali ili asimame, akawa anadondoka na wakati mwingine katika harakati hizo, ataumia lakini haachi kujifunza kusimama.

Hatua hizo za mtoto katika kukua ndizo hatua za wewe kwenye kuelekea mafanikio. Utaanza taratibu, utakumbana na changamoto nyingi lakini hutakiwi kuacha, endelea kupambana hadi usimame katika mambo yako.

USIOGOPE KUPATA HASARA

Wapo watu huko mtaani ambao wameshindwa kufanikiwa kupitia biashara kwa sababu wanaogopa kupata hasara. Iko hivi, ukiwa mfanyabiashara, lazima utengeneze mazingira ya kupata faida lakini jua hata hasara inaweza kukupata. Hasara katika mradi au biashara haikwepeki.

Haitakuwa sahihi wewe kuacha kufanya biashara kwa kuogopa kupata hasara. Hasara ni katika changamoto za kujaribu. Ni sehemu ya kujifunza ulipokosea ili baadaye usirudie makosa yaleyale.

Ndiyo maana ukikaa na yeyote aliyefanikiwa akakupitisha katika mapito yake hakika utapigwa na butwaa. Ni hayo tu kwa leo, tukutane tena wiki ijayo kwa mada nyingine.

Comments are closed.