DAR ES SAALAM: Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) jana imezindua rasmi huduma ya mawasiliano ya simu ya kuhama mtandao mmoja kwenda mwingine bila kubadilisha namba ya awali. (Mobile Number Portability ‘MNP’).
Akizungumza katika hafla hiyo, iliyofanyika Makao Makuu ya Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA), Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Mhandisi James Kilaba mbele ya Waziri wa Ujenzi Uchukuaji na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa ambaye alikuwa mgeni rasmi, aliyataja mambo hayo 10 ya kuzingatia kwa mtumiaji:
GHARAMA YA LAINI
Kampuni ya simu husika inahitajika kumpa mteja laini mpya aidha bure au kukmuuzia bila gharama zingine zaidi.
KUSHAWISHIWA
Mtoa huduma wa awali haruhusiwi kumshawishi mteja kubaki kwenye huduma yake kwa namna yoyote ile, akifanya hivyo mteja anapaswa kutoa taarifa TCRA, ila anaweza kuahirisha kuhama mwenyewe, kabla hajatuma ujumbe wa HAMNA KWENDA 15080.
MTEJA MPYA
Kwa mteja mpya aliyesajiliwa na kampuni husika hivi karibuni, anaruhusiwa kuhamia mtandao mwingine baada ya siku 60.
KUJUA NAMBA ULIYOHAMA
Mteja akipiga simu kwenye namba aliyohama, atagundua imehamia mtandao mwingine kwa kusikia sauti ya milio miwili mifupi (beeps) unapoanza tu kupiga. Mlio huo utamtaarifu gharama za simu unayopiga inaweza kuongezeka zaidi.
KUTUMA FEDHA NAMBA ILIYOHAMA
Mteja anapotuma fedha kwenda namba aliyohama, atapewa taarifa ili awe na maamuzi ya kutuma au la! Kulingana na taratibu za mtandao husika.
MUDA WA KUPATIKANA HUDUMA
Huduma hiyo imeanza kutolewa rasmi leo (Machi Mosi, 2017), maduka, ofisi na maeneo ya mauzo ya mtoa huduma wako mpya wanaendelea na huduma kawaida.
KUHUSU SIMU BENKI
Kutokana na mteja anayehamia mtandao mwingine kupewa namba mpya, hivyo anapaswa kuwasiliana na tawi la benki yake ingawa inategemeana na benki kama inatoa huduma ya simu benki.
MUDA WA MAONGEZI
Mteja aliye na salio la muda wa maongezi, anapaswa kutumia salio lake lote kabla ya kuhama vinginevyo salio linaweza kupotea.
FEDHA MTANDAO
Kwa mteja mwenye salio la pesa kwenye simu yake anapaswa atoe kwanza pesa yake kabla hajahama, vinginevyo itabidi afuate taratibu zingine kupata pesa yake. Ila muda wote pesa itakuwa salama.
MALALAMIKO AU MAOMBI
Kwanza wasiliana na mtoa huduma wako mpya ili kupata ufumbuzi, usiporidhika toa malalamiko yako TCRA.
Comments are closed.