The House of Favourite Newspapers

SIRRO: Tunamchunguza Vanessa Mdee

Kamanda wa Kanda Maalum Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro akizungumza na wanahabari.

DAR ES SALAAM: Kamanda wa Kanda Maalum Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro amethibitisha kuwa jeshi lake linaendelea kumshikilia staa wa Bongo Fleva, Vanessa Mdee ‘V-Money’ kwa ajili ya uchunguzi na watakapokamilisha uchunguzi dhidi ya kuhusishwa na madawa ya kulevya, atafikishwa mahakamani.

….Akiendelea kuzungumza na wanahabari.

Kamanda Sirro ameyasema hayo leo alipokuwa akizungumza na wanahabari katika taarifa yake ya kuwatahadharisha wananchi wa Dar es Salaam juu ya uwepo wa taasisi feki za fedha (Saccos) yenye jina maarufu la ‘Focus Vicoba’ kwenye mitandano ya kijamii wakiwataka waweke fedha katika akaunti yao na waweze kujipatia faida mara mbili ya fedha wanayokuwa wameweka huku wakitumia majina ya viongozi mbalimbali pamoja na wafanyabiashara wakubwa nchini.

Sirro akionyesha baadhi ya silaha walizozikamata katika oparesheni.

Kwenye mkutano huo, Kamanda Sirro alipoulizwa na mmoja wa wanahabari kuhusu V-Money kumshikilia baada ya amri ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda na ni hatua gani anachukuliwa, Kamishna Sirro alisema bado  wanaendelea na uchunguzi kisha ikithibitika kama ana kesi ya kujibu,  watamfikisha mahakamani.

Wanahabari wakichukua tukio hilo.

“Ndio tunamshikilia msanii Vanessa Mdee, tunaendelea na uchunguzi wetu na tukikamilisha uchunguzi wetu na ikathibitika kama ana kosa la kujibu basi  tutamfikisha mahakamani,” alisema Kamishna Sirro.

Vanessa ni miongoni mwa wasanii  waliotajwa kwenye orodha ya awamu ya pili na mkuu wa mkoa wa Dar, Paul Makonda na kutakiwa kuripoti kituoni hapo kwa ajili uchunguzi kutokana na kuhusishwa na madawa ya kulevya.

Baadhi ya ‘bodaboda’ walizozikamata katika oparesheni inayoendelea jijini Dar.

Akizungumzia kuhusu utapeli unaofanywa mtandaoni, Kamanda Sirro alisema katika ufuatiliaji wa jambo hilo, wanamshikilia Boniface Samson Ojwando waliyemkamata Desemba 16, mwaka jana kwa kuhusika na mtandao huo wa utapeli na tayari wameshamfikisha mahakamani kujibu mashtaka yanayomkabili.

“Nitoe onyo kwa wale wote wanaoendelea kufanya udanganyifu huu wa kujipatia fedha kwa njia isiyo halali kupitia mitandao ya kijamii kuacha mara moja kwani sheria iko wazi na pindi watakapokamatwa watachukuliwa hatua kali,” alisema Kamishna Sirro.

NA DENIS MTIMA/GPL

Comments are closed.