The House of Favourite Newspapers

Kwa nini Uuvumilie Uchumba wa Kuumizwa Kila Siku?

Wapenzi wanaoishi kwa kugombana mara kwa mara.

Na MWANDISHI WETU|GAZETI LA IJUMAA| MAKALA

HALI gani mpenzi msomaji wangu, nakukaribisha tena kwa moyo mkunjufu kwenye uwanja huu maridhawa, mahali ambapo mimi na wewe tunajadiliana na kuelimishana kuhusu mambo mbalimbali yahusuyo uhusiano wa kimapenzi.

Nimeamua kuja na mada hii kama inavyojieleza hapo juu, baada ya siku chache zilizopita, msomaji wangu mmoja kuwasiliana na mimi kwa WhatsApp kwa kutumia namba ya hapo juu, ambapo alijirekodi sauti akieleza matatizo yanayomsumbua kwenye uhusiano wake na kunitumia.

Baada ya kuusikiliza ujumbe alionitumia, nililazimika kumpigia simu na kuzungumza naye. Baadaye tulipanga kukutana naye na hatimaye, alinieleza kwa kirefu kile kinachomsumbua kwa muda mrefu.

Kwa kuwa aliniomba nisimtaje jina, sitafanya hivyo lakini kwa faida yake na kwa faida ya wengine wenye tatizo kama lake ni vizuri tukajadiliana kwa kina kuhusu tatizo hili linalowaumiza wengi. Inafahamika kwamba unapofikia umri wa kukomaa kifikra na kimwili, unahitaji mwenza wa kuanza naye safari ambayo mwisho, mategemeo huwa ni kuja kuwa na familia na kuishi kwa amani na upendo.

Ni wazi kwamba hata kama unajitunza namna gani, au unajiheshimu namna gani, itafika kipindi ambacho hutaweza kuendelea kuishi mwenyewe, hutaweza kuendelea kuelekeza nguvu kwenye kazi au masomo, utahitaji mtu wa jinsia tofauti na yako, ambaye atakuwa chaguo lako, utakayempenda na hatimaye kujenga naye familia.

Kama wewe umeshavuka hatua hizo zote, namaanisha kama tayari wewe ni mume au mke wa mtu na mpo katika familia, iwe Mungu amewajalia kupata watoto au bado, lakini kama unaye mtu wa pembeni yako, unayempenda na anayekupenda, mnayeishi naye pamoja, bila shaka unaijua tofauti kati ya kuishi ‘single’ na kuishi katika ndoa. Ukamilifu wa mwanaume, hata awe na kasoro chungu nzima, ni kuoa na kuanzisha familia.Ukamilifu wa mwanamke pia, hata awe wa namna gani, ni kuolewa na kujenga familia.

Ipo hivyo na hakuna anayeweza kulipinga hilo kwa sababu tumeumbwa hivyo, kila mmoja ni ubavu mmoja ambao ni lazima upatikane ubavu wa pili ili kukamilisha uumbaji. Kwa bahati mbaya sana, wapo watu wengi ambao wanatamani sana kuingia katika ndoa lakini kila wanapojaribu, wanachoambulia ni maumivu, mateso na kilio.

Hicho ndicho kilichokuwa kinamsumbua dada yangu ambaye nimeanza kukueleza kwa kifupi kuhusu kilichomtokea. Tulizungumza mambo mengi na msomaji wangu huyu ambaye alikiri kwamba amekuwa mfuatiliaji mzuri wa mada zangu ninazoziandika ndiyo maana aliona mimi ni mtu sahihi kumuongoza, licha ya ukweli kwamba bado sijafikia utu uzima wa kuweza kuwa na busara kiivyo! Alinieleza kwamba yeye amezaliwa katika familia ya kidini, wazazi wake walikuwa na imani kali za kidini na walimlea katika mazingira ambayo, hakuwahi kujihusisha na masuala ya kimapenzi, mpaka alipohitimu masomo yake ya chuo na kuja jijini Dar es Salaam kuanza kazi.

“Wazazi wangu walinifundisha kwamba sitakiwi kujihusisha na mapenzi wala mwanaume hatakiwi kuugusa mwili wangu mpaka atakaponioa,” alisema dada huyo kwa upole, akaendelea kueleza kwamba kwa sababu kiumri alijiona tayari ameshakuwa mkubwa, alikubali ombi la mmoja kati ya wanaume wengi waliokuwa wakimsumbua na kumtongoza mara kwa mara. Aliniambia kwamba aliamua kumkubali kwa sababu walikuwa wakifanya kazi ofisi moja na aliridhishwa na tabia na mwonekano wake wa nje, akampa ahadi nyingi kwamba lazima atamuoa.

“Kwa kuwa alinihakikishia kwamba anataka kunioa, nilimpa sharti kwamba ni lazima twende nyumbani kwetu, akajitambulishe kwa wazazi wangu, anichumbie na kunioa hapo ndipo nitakapoweza kumpa mwili wangu,” anasimulia dada yetu huyo.

Anaeleza kwamba kweli walifunga safari na mwanaume huyo mpaka nyumbani kwao, mkoani Morogoro ambapo ni kweli mwanaume alienda kujitambulisha kwa wazazi wake na kuahidi kumuoa.

Kwa furaha aliyokuwa nayo, waliporejea Dar es Salaam, alijikuta akikubali kufanya mapenzi na mwanaume huyo kwa sababu tayari wazazi walikuwa wanamjua na alionesha kweli kuwa na nia ya dhati ya kumuoa.

“Nilipoanza kumpa mwili wangu tu, hapo ndipo asali ilipoingia shubiri, najuta sana, lakini huyo ni mmoja tu, mpaka sasa nimeshawapeleka wanaume wanne nyumbani kwa vipindi tofauti na wote wanaishia kunichumbia na kunitumia kisha wananitenda, nina mkosi gani mimi?” alisema dada huyo huku akilengwalengwa na machozi.

Je, unamshauri nini dada huyu? Na wewe una ushuhuda unaofanana na huu? Tukute wiki ijayo.

Comments are closed.