The House of Favourite Newspapers

Undani wa Mnenguaji wa Twanga Pepeta Aliyeua na Kutoweka

0
Mnenguaji Idd Masamaga

 

MNENGUAJI wa Bendi ya African Stars ‘Twanga Pepeta’ aliyefahamika kwa jina Idd Masamaga maarufu kama ‘Maga’, anadaiwa kumpiga na kumuua mpangaji mwenzake kwa kile kinachodaiwa kuwa wivu wa kimapenzi huko Kinondoni mwishoni mwa wiki iliyopita, Risasi Mchanganyiko limeambiwa.

Kwa mujibu wa chanzo cha habari hiyo, Magu ambaye pia ni baba wa mtoto mmoja, alikuwa akiishi kinyumba na mwanamke ambaye aliachika, lakini ambaye aliyekuwa mumewe aliishi katika nyumba hiyohiyo.

“Marehemu awali alikuwa na maisha yake mazuri tu, lakini alipostaafu maisha yaliyumba kidogo kiasi kwamba alilazimika kurejea ukweni ambako alipewa hifadhi. Lakini aliyekuwa mkewe, alikuwa akiishi kinyumba na huyo mnenguaji na walikuwa wanaenda vizuri tu.

 

 

“Inasemekana pamoja na kuwa wameachana, lakini alikuwa bado anampenda na kitendo cha yule bwana kuingia kulala na mkewe kilikuwa kinamuuma, sasa siku hiyo inadaiwa kulikuwa na ugomvi kati ya Maga na mpenzi wake, huyo mwanaume akaona huruma, akaenda kwa ajili ya kuwaamulia, ndipo alipogeuziwa kibao na kupigwa, kitu kilichosababisha kupoteza maisha,” kilisema chanzo hicho kinachokaa jirani.

Chanzo kingine kilidai kuwa siku ya tukio, Maga alikuwa amekaa kwenye baa moja iliyopo nyuma ya Ukumbi wa Mango, Kinondoni akiwa pamoja na baadhi ya wanamuziki wenzake wakijiburudisha kabla ya ugomvi kutokea.

“Tulikuwa tumekaa pale tunakunywa, baadaye kukatokea ugomvi kati ya Maga na mmoja wa wapiga drum wa Twanga, baada ya kuamuliwa, ndipo jamaa akaenda zake kwake ambako ndiko baadaye tukasikia amempiga yule mtu na kumuua,” kilisema chanzo hicho.

 

 

Mwalimu wa wanenguaji wa Twanga Pepeta, Hassan Musa Mohamed ‘Super Nyamwela’ alipoulizwa kuhusu tukio hilo, alisema hata yeye amesikia tu kwa watu, lakini kwa jinsi alivyomfahamu Maga alikuwa ni mtu mzuri licha ya kuwa alikuwa mnywaji wa pombe.

“Siwezi kujua alipokuwa anaishi kwa sababu kama unavyojua watu tunakutana tu kazini na kila mmoja anaendelea na hamsini zake. Mara ya mwisho kuonana naye nafikiri kama wiki hivi si unajua tulikuwa tumepumzika kupisha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na mimi hapa narudi Dar natokea Dodoma,” alisema Nyamwela.

Mara mbili Risasi Mchanganyiko lilimtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Susan Kaganda bila mafanikio, lakini hatimaye alipopatikana, alisema alikuwa likizo, hivyo kama tukio hilo limetokea, basi kutakuwa na taarifa ofisini ambazo bado hajazipitia.

 

NA GLADNESS MALLYA | RISASI MCHANGANYIKO |DAR ES SALAAM

Leave A Reply