The House of Favourite Newspapers

Mzee Kilomoni: Tunaenda Mahakamani Kuzuia Mkutano

0
Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini wa Simba Mzee Hamis Kilomoni.

BARAZA la Wadhamini la Klabu ya Simba chini ya Mwenyekiti, Hamisi Kilomoni limesema litakwenda mahakamani iwapo viongozi waliokaimu nafasi ya uongozi klabuni hapo wataendeleza mchakato wa mkutano mkuu unaotarajiwa kufanyika Agosti 13 na 20 kwa kuwa ni kinyume na sheria.

 

Simba imepanga kufanya mkutano wake mkuu Agosti 13 na ule wa mabadiliko ya katiba Agosti 20 kwa ajili ya kupisha mabadiliko jambo ambalo linapingwa na wadhamini wa klabu hiyo kwa madai kuwa ni kinyume na taratibu kwa kuwa wanaweza kuingilia uhuru wa mahakama.

 

Kilomoni amedai mkutano huo hawautambui kwa kuwa hauwezi kufanyika wakati viongozi wa Simba rais, Evance Aveva na makamu wake Geofrey Nyange (Kaburu) wakiwa ndani mahabusu.

 

Akizungumza na Championi Ijumaa, mzee Kilomoni alisema kama agizo hilo walilolitoa halijatekelezeka watatinga mahakamani kuwashitaki kwa kuwa wao ndiyo wasimamizi wa mali za Simba.

 

“Kamati ya utendaji imevunja kanuni ya katiba ya 2014 ibara ya 24 kifungu cha (1) ambacho kinasema mkutano mkuu utaongozwa na rais wa klabu na endapo hatakuwepo kwa sababu yeyote ile, mkutano mkuu utaongozwa na makamu wake na endapo hatakuwepo utaongozwa na mjumbe wa kamati ya utendaji, kitu ambacho aliyekaimu hana sifa hizo za kuongoza mkutano huo.

 

“Kwa sababu hana sifa ya ujumbe wa muda mrefu, hakuna ibara katika katiba hiyo inayomruhusu mjumbe wa muda mrefu kumkaimisha kwa muda mfupi, hivyo kama hayupo wa muda mrefu maana yake ni kuwasubiri viongozi kwa siku 90 kwa mujibu wa katiba.

 

“Nashangazwa kuona mkutano mkuu unakwenda kuitishwa hali ya kuwa viongozi wa juu wanatuhumiwa, wadhamini hatujakataza kuendeleza shughuli yoyote ya kiutendaji za kila siku bali bodi inapinga uvunjaji wa taratibu wa sheria na kanuni tulizowekewa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alisema Kilomoni.

Leave A Reply