The House of Favourite Newspapers

Jinsi Ya Kujinasua Kwenye Uchumba Sugu!

0

 

WENGI wetu tunapoingia kwenye uhusiano tunategemea kupitia hatua kadhaa kabla ya kuingia kwenye ndoa.

Kuna ambao wanaamini ili uweze kumjua vizuri mwenzako na kufanya uamuzi sahihi wa kuoana, unapaswa kudumu na mwenzi wako kwa miaka zaidi ya miwili au mitatu hivi.

 

Lakini kuna wengine wao wanaamini kufanya uamuzi wa ndoa, wanahitaji miezi miwili au mitatu.

Wanaosema wanahitaji miaka mitatu wanakuwa na hoja zao. Wanakwambia wanataka kujiridhisha kwenye kila ‘idara’.

 

Mwanamke anataka amjue vizuri mwandani wake, ajue tabia zake japo si zote lakini aweze angalau kumsoma kama anaweza kumvumilia au la.

 

Mwanaume naye vivyo hivyo, anataka kujua aina ya mwanaume aliyenaye kama ni sahihi au la. Anahofia kufanya maamuzi ambayo anaamini akikosea anaweza kujutia maisha yake yote.

Ili kujiridhisha, anahitaji kuwa karibu na mchumba wake katika kipindi hicho ili aweze kumjua zaidi kama anaweza kumvumilia au la.

 

Anataka kujiridhisha kwamba udhaifu alionao mwenzake ni wa kiasi cha kawaida ambacho anaweza kumbadilisha na kwenda katika mstari ulionyooka?

Kama akiona hawezi, anaghairi. Haijalishi amepoteza muda gani. Iwe miezi au hata mwaka mmoja, miwili au hata mitatu.

 

Katika kipindi cha kuchunguzana, kuna wengine wanapitiliza. Wanataka wakae muda mrefu zaidi. Wanataka angalau wafikie hatua ya kupata mtoto mmoja au wawili.

 

Uhusiano unapokuwa wa muda mrefu ndiyo tunauita uchumba sugu. Wengi hujikuta kwenye uchumba sugu kutokana na sababu mbalimbali.

Kuna ambao wanataka kutoka lakini wanashindwa kutokana na wenzi wao kuwa ‘wabishi’ kufanya maamuzi.

Wenzi hao kwa sababu zao wanazozijua wanaamua kuchelewa kuingia kwenye ndoa. Hawataki tu, wakati mwingine hawana hata sababu za msingi.

 

UCHUMBA UPI NI SAHIHI?

Kimsingi ili uweze kuingia kwenye ndoa na mtu, yakupasa upate muda wa kumchunguza na kujiridhisha japo katika baadhi ya mambo ili usije kujutia uamuzi wako huko baadaye.

Hupaswi kuingia kwenye uhusiano na mtu kisha ukafanya maamuzi ya haraka. Lazima umjue mwenzi wako ana tabia za aina gani?

 

Ana sifa unazozihitaji? Mathalani, ana hofu ya Mungu? Si muhuni wa kupindukia? Hayo yote huwezi kuyajua ndani ya muda mchache, inahitaji muda kidogo kuweza kuyabaini.

 

Hakuna muda maalum unaopaswa kushauriwa kudumu kwenye uchumba lakini unatakiwa usiwe mfupi au mrefu sana.

Jitahidi usikae muda mrefu kwenye uchumba. Jenga tabia ya kuufanyia tathimini uchumba wako kila baada ya kipindi fulani, mfano unaweza kufanya hivyo katika vipindi vya miezi sita sita.

 

Kufanya hivyo kutakufanya ujue, uhusiano wenu unakua au umesimama palepale. Kukua, uonekane katika fikra na matendo yenu. Kama huoni kukua katika kipindi cha miezi sita ya awali, huoni mabadiliko pia katika miezi sita mingine, ni bora ukaahirisha safari hiyo haraka.

 

Jenga mazoea ya kuzungumza na mwenzi wako na mjiwekee mikakati ya kufikia hatua fulani ndani ya muda fulani.

Kwa kufanya hivyo, itakutoa haraka kwenye safari ndefu ya uchumba. Usikubali kukaa muda mrefu hadi kufikia hatua ya kuzaa watoto. Endapo itatokea bahati mbaya umepata, basi hakikisha kitendo hicho hakijirudii.

 

Zungumzieni kuhusu safari yenu na endapo mmoja wenu ataona mwenzake hana uelekeo mzuri, ni vyema mkaachana.

 

Unapoingia kwenye uhusiano mpya, hakikisha hauingii mkenge kwa mara nyingine. Jitahidi kumsoma mwenzako tabia kabla kuruhusu moyo wako kumpenda na uchumba wenu usiwe wa muda mrefu (sugu), jifanyieni tathimini kila wakati.

Tubadilishane mawazo kupitia namba zilizopo hapo juu, waweza nicheki Facebook na Instagram kwa jina la Erick Evarist, Twitter natumia ENangale.

Leave A Reply