The House of Favourite Newspapers

Gazeti La Spoti Xtra Kuingia Mtaani Kesho

Wakati wa uzinduzi wa Gazeti la Spoti XTRA ulivyofanyika jijini Dar es Salaam jana.

GAZETI jipya la Michezo na Burudani la Spoti Xtra, limezinduliwa rasmi jana Ijumaa, jijini Dar es Salaam. Spoti Xtra litaanza kutoka kesho Jumapili na litakuwa mitaani kila Jumapili kwa Shilingi 500 tu huku likiwa limesheheni matukio na chambuzi zilizofanyiwa kazi na waandishi na wahariri waliobobea.

 

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mhariri Mtendaji wa Global Publishers, Saleh Ally, alisema: “Tunayo furaha kubwa kuwaletea wasomaji gazeti hili ambalo tunaamini litakata kiu yao kwa siku ya Jumapili, kwani siku hiyo kwa muda mrefu wamekosa kupata habari za kina za michezo.

“Spoti Xtra kama ilivyo jina lake, humo ndani kutakuwa na michezo yote ambayo mnaifahamu, hivyo wasomaji wakae mkao wa kula kwani tutafika hadi vijijini ambapo wengine hawafiki.”

 

Michael Momburi ambaye ni Mhariri Mkuu wa Spoti Xtra, alisema; “Tumejipanga kuwaletea wasomaji kitu tofauti kwani hapo kabla tuliangalia sokoni kitu gani kinakosekana, tukaona ni vingi, hivyo ndani ya Spoti Xtra vitapatikana vyote hivyo. Tunawaomba wasomaji wetu Jumapili hii wasikose nakala zao.

 

“Tutajikita kwenye habari za ukweli zilizofanyiwa uchunguzi wa kutosha, tutaandika habari za uchunguzi na tutawapa wasomaji takwimu za kutosha kwenye anga mbalimbali za kimichezo.”

 

Ndani ya gazeti hilo, kutakuwa na wachambuzi wengi mahiri wa michezo wanaokubalika na wasomaji pamoja na makala za ndani na nje ya Tanzania ambazo hazipatikani kwingineko.

 

Spoti Xtra itakuwa na kurasa 24 na itakuwa chambuzi za watu mbalimbali akiwemo Haji Manara wa Simba na Dismas Ten wa Yanga.

Comments are closed.