
Na BONIPHACE NGUMIJE| UWAZI| SHOWBIZ
SAKATA la mastaa na watu mbalimbali wakiwemo askari 15 wanaohusishwa katika matumizi pamoja na biashara ya kuuza na kutumia madawa ya kulevya ‘unga’ walioagizwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kujisalimisha katika Kituo cha Polisi cha Kati linazidi kupamba moto na kuchukua sura mpya kila siku kwenye media na mitandao mbalimbali ya kijamii.
Baadhi ya majina ya mastaa waliotajwa na Makonda ni Miss Tanzania 2006, Wema Sepetu, Wanamuziki TID, Chid Benz, Nyandu Tozi, Mr Blue, Vanessa Mdee na Mtangazaji Babu wa Kitaa pamoja na video queen anayefahamika zaidi kwa jina la Tunda.
Miongoni mwa majina yaliyotajwa, wapo ambao walikwisha jisalimisha katika kituo hicho cha polisi, wakiongozwa na Wema Sepetu, Tid pamoja na Babu wa Kitaa kwa ajili ya mahojiano na kulisaidia jeshi la polisi kufahamu baadhi ya mambo katika vita hiyo ya kitaifa ya kupambana na biashara haramu ya madawa ya kulevya.
Vita ndiyo kwanza imeanza, ambapo katika makala haya mwanamuziki ambaye pia ni mwanaharakati anayepambana kuhakikisha vijana wanaacha kujihusisha na madawa hayo Bongo, Kala Pina anafunguka mtazamo wake katika vita hii, nini kifanyike ili kuhakikisha suala la madawa ya kulevya linakuwa historia Bongo.
Showbiz: Bila shaka jitihada alizoanza kufanya Mkuu wa Mkoa wa Dar umezisikia juu ya kupambana na matumizi pamoja na biashara ya madawa ya kulevya, kama mwanaharakati wa muda mrefu katika vita hiyo unalipi la kusema?

KALAPINA: Kikubwa napenda kumpongeza kwa jitihada zake. Ameonyesha kuthubutu maana kabla yake hakuna kiongozi yeyote aliwahi kufanya jambo kama hili.
Showbiz: Kuna baadhi ya wasanii, askari polisi na watu mbalimbali wametajwa kuhusika katika biashara hiyo, mtazamo wako ni upi katika vita hiyo?
Kala Pina: Kwa upande mmoja inaweza kusaidia lakini upande mwingine inaweza isisaidie ukizingatia watumiaji wengi wananunua kutoka kwa wauzaji wa rejareja mitaani, sasa kuupata ule mtandao mzima inabidi kufanyika kazi ya ziada, hasa kupita katika vituo vikubwa ambavyo vinajulikana vinauza dawa hizo. Mpaka sasa vituo hivyo bado havijaguswa, nina uhakika hapa tunapozungumza huko mitaani Kinondoni, Ilala na Temeke madawa hayo yanaendelea kuuzwa kwani vituo yanapouzwa vinajulikana na ni muda mrefu ila inashangaza kuona vyombo vya dola vinavifumbia macho. Kwa upande wa hao waliokamatwa na kuwekwa rumande kama ni watumiaji inatakiwa kufahamika kuwa ni wagonjwa na wanatakiwa kupewa ‘special treatment’ na wasiishi kama wafungwa wa kawaida.

Showbiz: Mpaka hapa sakata hili lilipofikia kipi unaweza kumshauri Makonda?
Kala Piana: Atushirikishe wadau ambao tupo kwenye vita hii kwa muda mrefu, tuna mambo mengi mno ambayo yanaweza kusaidia katika kuimaliza vita hii kwani tunaelewa tobo la biashara hiyo lilipo.
Showbiz: Unamaanisha nini unapozungumzia tobo la biashara ya unga?
Kala Pina: Namaanisha watafutwe wafanyabiashara wakubwa wanaojihusisha na biashara ya madawa ya kulevya, mabig don au papa. Nazungumzia wanaoingiza madawa hapa nchini. Kikubwa wanajulikana na siyo suala la siri, hata njia zao zinajulikana, wanaingiza kupitia baharini. Sasa huko kukidhibitiwa hawa vijana wengine namaanisha wasanii wenzangu waliokamatwa wenyewe wasaidiwe kujinasua huko kwenye matumizi.

Showbiz:Unaweza kuwaweka wazi wafanyabiashara unaowafahamu wanaojihusisha na biashara hiyo kumsaidia Makonda?
Kala Piana: Siwezi kutamka kienyeji. Ndiyo maana nimesema wadau tushirikishwe ili kusaidia katika vita hii. Kuhusu kuwataja siyo ishu maana hata serikali inawafahamu nina uhakika huo.
Showbiz: Kipi ambacho unafikiri Makonda hakifahamu katika vita hii?
Kala Pina: Labda juu ya ugumu wa kulimaliza suala hili. Kiukweli hii ni vita ya kitaifa kama anavyosema mwenyewe na ni vigumu kuimaliza. Ili kuishinda inabidi kuwa na nia ya dhati pamoja na mkuu wa mkoa na serikali yake kushirikiana vyema na watu binafsi ambao wapo kwenye hizi harakati kwa muda mrefu.
Showbiz: Nakupa nafasi kama una lolote lingine ambalo unaweza kuzungumza juu ya sakata hili.
Kala Pina: Kikubwa ajifunze kwa viongozi waliofanikiwa kuishinda vita hii akiwemo Rais wa Philippines, Rodrigo Duterte. Itasaidia kufahamu mbinu gani zilitumika kushinda vita hii yenye changamoto kubwa.