The House of Favourite Newspapers

Matola Apanga Kumtibulia Mfaransa Wa Simba SC

Wacezaji wa timu ya Lipuli.

KOCHA Msaidizi wa Lipuli FC, Selemani Ma­tola, amesema hatakubali kufanywa daraja la kuipa Simba ubingwa wa Ligi Kuu Bara wakati timu yake itakapokutana nao Juma­mosi wiki hii.

 

Timu hizo zinatarajiwa kuvaana Jumamosi kwenye Uwanja wa Samora mkoani Iringa badala ya Ijumaa kama ilivyopangwa hapo awali.

 

Katika mchezo wa raundi ya kwanza uliochezwa kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1.

Akizungumza na Championi Jumatano, Matola alisema katika mechi hiyo timu yake itaingia uwanjani ikiwa na morali baada ya matokeo ya ushindi wa bao 1-0 walioupata dhidi ya Singida.

Matola alisema, hataki kuona timu yake ikipoteza katika uwanja wa nyumbani, hivyo ameahidi kuifun­ga Simba ili kuvunja rekodi ya Simba ya kutofungwa kwenye ligi msimu huu.

 

“Nimemaliza mechi ya ligi dhidi ya Singida kwa ushindi wa bao 1-0 ambao kwangu nauona mkubwa, kama una­vyoiona ligi msimu huu ilivyo ngumu.

 

“Matokeo haya ya Singi­da yatawafanya wachezaji wangu waingie uwan­jani wakiwa na morali ya hali ya juu na kuongeza hali ya kujiamini na kupata ma­tokeo mazuri.

 

“Nitaingia uwanjani nikijua Simba haijawahi kufungwa tangu ligi ya msimu huu imeanza, lakini hiyo hainifanyi niogope zaidi nitakiandaa kikosi changu kuhakikisha tunavunja re­kodi yao,” alisema Matola.

Comments are closed.