The House of Favourite Newspapers

Ufaransa Wababe Wanaopewa Nafasi Urusi 2018

KUNA mataifa mengi yanapewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri kwenye Kombe la Dunia mwaka huu.

 

Zikiwa zimebaki siku nane kabla michuano hiyo haijaanza nchini Urusi, Ufaransa ni kati ya taifa ambalo linatajwa kuwa linaweza kutikisa kwenye fainali za mwaka huu.

Ufaransa imejaza vijana wengi wenye vipaji vya hali ya juu, ambao wanaweza kufanya jambo lolote kwenye soka.

Klabu nyingi kuna kama Man United, PSG, Chelsea, Arsenal na nyingine nyingi zimejaza wachezaji ambao wanatoka kwenye timu hii na kuendelea kuipa ubora wa hali ya juu.

 

Hii imeifanya kuwa nchi ambayo inasubiriwa kuwa inaweza kufanya mambo makubwa kwenye fainali za mwaka huu.

 

Kuna mambo mengi ambayo yanaonekana kuwafanya Ufaransa kuwa bora, lakini kuna mengine yanatia mashaka kama timu hiyo itaweza kuwika kwenye michuano hii ya mwaka huu.

 

KIKOSI HATARI

Kuanzia Ufaransa walipofika fainali ya Michuano ya Euro mwaka 2016, hawajaonyesha tena kuwa wanaweza kufanya jambo la tofauti kwenye michuano mikubwa duniani pamoja na kwamba wamekuwa wakibadilisha kikosi mara kwa mara.

 

Kwa sasa wanakwenda wakiwa na wachezaji wengi ambao hawana uzoefu kama Kylian Mbappé, Thomas Lemar na Ousmane Dembélé, lakini pia wakiwa na kiungo matata kama Corentin Tolisso lakini naye uzoefu kwake ni mdogo.

 

Pamoja na kuwa na wachezaji hawa, Ufaransa pia itategemea huduma ya mastaa kama Poul Pogba, Antonie Griezimann na Olvier Giroud ambao wamekuwa wakifanya vizuri kwenye timu zao.

 

Maswali mengi yamekuwa yakiulizwa kuhusu eneo la mabeki wa kushoto wa Ufaransa, baada ya kuonekana kuwa kocha wa timu hiyo amewachukua mastaa wawili, Djibril Sidibé na Benjamin Mendy, ambao muda mwingi msimu huu walikuwa na majeraha na hawakupata nafasi ya kucheza.

 

Kocha Didier Deschamps anapendelea mfumo wa 4-4-2 au 4-3- 3, mfumo huu umekuwa ukiwafanya viungo wa timu hiyo kujaa wengi katikati na kutoa nafasi kubwa kwa timu hiyo kushambulia.

 

Deschamps ambaye michezo mitatu ya hivi karibuni amecheza kwa mfumo wa 4-3-3, ameonekana kuwa lazima atawatumia wachezaji wa kiungo Paul Pogba, N’Golo Kanté na Blaise Matuidi.

 

Lakini michezo miwili ametumia mfumo wa 4-4-2, ambapo amekuwa akiwachezesha mbele Antoine Griezmann-Olivier Giroud huku staa Matuidi akianzia kwenye benchi.

 

MCHEZAJI ATAKAYESHANGAZA

Kylian Mbappé, anaaminika kuwa ndiye mchezaji anayeweza kufanya maajabu kwenye mchezo huu, huyu amekuwa akitajwa kuwa ni Thierry Henry mpya ambaye wakati anacheza Kombe la Dunia mwaka 1998, alikuwa na umri wa miaka 20 kama alivyo Mbappe leo.

 

NANI ANAAMINIKA KUWA ATACHEMKA

Paul Pogba ameshaonyesha kuwa hawezi kuisaidia timu hiyo kutokana na kiwango ambacho amekuwa akikionyesha kwenye michezo ya kirafiki.

Lakini inaonekana kuwa kitendo cha kuzomewa mara kwa mara na mashabiki wa timu hiyo kimekuwa kikimfanya ashindwe kuonyesha uwezo wake uwanjani.

 

Haonekana kuwa na kiwango cha juu kama vile alivyokuwa alipokuwa akiichezea Juventus miaka miwili iiliyopita.

Inaonekana kuwa anaweza kukosa nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo kama tu atacheza kwenye michezo miwili vibaya iliyobaki ya kirafiki.

 

MATARAJIO MAKUBWA KWA UFARANSA NI NINI?

Hakika hakuna jambo lingine ambalo wanaweza kulifanya wakafanikiwa zaidi ya kufika kuanzia nusu fainali na kuendelea, kumbuka nchini Brazil walitolewa hatua ya robo fainali na hivyo ni lazima mwaka huu wafanya mambo makubwa zaidi ya yale.

Lakini pia kutwaa ubingwa tu ndiyo jambo ambalo linaweza kuokoa kibarua cha kocha Deschamps kwenye timu hiyo ambayo inawaniwa na makocha wengi.

Comments are closed.