The House of Favourite Newspapers

Kocha Yanga Ataja Straika Anayemtaka

KOCHA Mkuu wa Yanga mwenye asili ya DR Congo, Mwinyi Zahera amewaambia mabosi wake kuwa anahitaji washambuliaji wawili na kiungo mmoja wote wenye uzoefu wa kucheza michuano ya kimataifa katika kukiimarisha kikosi chake kwa ajili ya msimu ujao.

 

Kauli hiyo ameitoa akiwa nyumbani kwake, Ufaransa alipokwenda kwa ajili ya mapumziko ya wiki mbili aliyopewa na uongozi wake.

 

Kocha huyo mwenye uraia wa nchi mbili Congo na Ufaransa alikabidhiwa kikosi hicho mwishoni mwa msimu mwa ligi baada ya aliyekuwa kocha wao Mzambia, George Lwandamina kusitisha mkataba wake.

 

Akizungumza na Championi Ijumaa, Zahera alisema amekiona kikosi hicho kwenye mechi kadhaa na kubaini baadhi ya upungufu ikiwemo safu ya ushambuliaji ambayo ilikuwa inaundwa na wachezaji wengi chipukizi ambao wamekosa uzoefu wa kutosha katika timu.

 

Zahera alisema timu hiyo inahitaji washambuliaji hao wenye uzoefu kwa ajili ya kuiimarisha safu yao ya ushambuliaji ambayo msimu uliopita ilikuwa ikiwatumia chipukizi, Yussuf Mhilu, Emmanuel Martin, Anthony Matheo, Geofrey Mwashiuya, Juma Mahadhi ambao ni ngumu kupata matokeo mazuri kwa kuwatumia vijana hao.

 

“Lipo wazi kabisa katika msimu uliopita wa ligi ilikuwa ni ngumu Yanga kuutetea ubingwa wa ligi, pia kufanya vizuri katika Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuwategemea wachezaji chipukizi kupata matokeo mazuri.

 

“Hivyo, ninahitaji washambuliaji wengine wawili watakaokuwa na uzoefu mkubwa watakaoleta changamoto kwenye safu ya ulinzi ya timu pinzani katika kuhakikisha tunapata matokeo mazuri.

 

“Pia, ninahitaji kiungo mwingine mwenye uzoefu atakayeweza kukaba na kuchezesha timu ndani ya wakati mmoja na tayari nimetoa mapendekezo yangu kwa uongozi ili kuhakikisha wanakamilisha mahitaji yangu,” alisema Zahera.

 

Yanga hivi karibuni ilielezwa kuwa katika mazungumzo na kiungo mshambuliaji, Haruna Moshi ‘Boban’ ambaye ni kati ya wachezaji wenye uzoefu mkubwa wa ligi na michuano ya kimataifa.

Na Wilbert Molandi, Dar es Salaam

Comments are closed.