The House of Favourite Newspapers

Waziri Mkuu Amliwaza Shigongo

MAMA mzazi wa Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Global Group, Eric Shigongo, Bi Asteria Kahabi Kapela, amefariki dunia alfajiri ya jana Ijumaa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, Muhimbili jijini Dar alipokuwa amelazwa kwa matibabu.

Marehemu alikuwa akisumbuliwa na maradhi kwa muda mrefu kabla ya kufikwa na umauti ambapo msiba upo Mikocheni B jijini Dar na mwili unatarajiwa kusafirishwa kwenda mkoani Mwanza kwa shughuli za maziko.

 

Muda mfupi baada ya kutokea kwa msiba huo, miongoni mwa watu wa karibu waliofika nyumbani hapo kutoa pole ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, Majaliwa Kassim Majaliwa.

Akizungumza na Championi Jumamosi, Mwenyekiti wa Kamati ya msiba huo ambaye ni Meneja Mkuu wa Global Publishers, Abdallah Mrisho alisema msiba upo nyumbani kwa marehemu maeneo ya Mikocheni B ambako taratibu zote za msiba zitafanyika kabla ya kuelekea Mwanza kwenye maziko.

 

“Kutokana na msiba mzito wa mama wa mkurugenzi wetu, kwa sasa ratiba kwa ajili ya kwenda kupumzisha pendwa wetu itaanzia kesho (leo) hapa kwake Mikocheni kwa mkesha wa ibada baada ya kuchukua mwili wa marehemu kutoka Muhimbili.

 

“Mwili utalala hapa nyumbani, Jumapili saa sita mchana kutakuwa na misa maalumu ya kumuombea hapa nyumbani kisha kutakuwa na misa nyingine katika Kanisa la Katoliki la Mikocheni B.

 

“Lakini baada ya misa na watu kuaga, safari ya kwenda uwanja wa ndege itaanza kwa ajili ya kuusafirisha kwenda Mwanza ambapo utawasili huko Jumatatu saa tatu asubuhi, kisha kupelekwa nyumbani kwa marehemu Nyakato Nundu.

 

“Saa sita mchana waombolezaji watapata nafasi kuuaga mwili kabla ya kupelekwa katika Kanisa la Katoliki la Nyakato Nundu kwa ajili ya misa hadi jioni,” alisema Mrisho na kuongeza:

 

“Siku ya Jumanne asubuhi safari ya kutoka Nyakato kuelekea Bupandwa Mhela itaanza, huko mwili utalala nyumbani kwake kisha siku ya Jumatano tutampumzisha mpendwa wetu katika nyumba yake ya milele hapohapo Bupandwa baada ya misa ya mazishi,” alisema Mrisho.

 

Baadhi ya viongozi mbalimbali wa serikali walihudhuria akiwemo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

 

Kwa niaba ya wafanyakazi wa Makampuni ya Global Group, tunatoa pole kwa familia ya Shigongo, ndugu jamaa na marafiki, kwa wafanyakazi wenzetu kwa kupata pigo la kuondokewa na mpendwa wetu.

Bwana alitoa, bwana alitwaa, jina lake lihimidiwe

Comments are closed.