The House of Favourite Newspapers

Jokate Afunguka Baada ya Kuteuliwa Mkuu wa Wilaya

Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo. 

MWANAMITINDO na mjasiriamali, Jokate Mwegelo, aliyeteuliwa na Rais John Magufuli kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, amefunguka jinsi alivyohaha hadi kupata nafasi hiyo.

 

Jokate amesema mwaka jana alitaka kukata tamaa kwenye maisha yake ya siasa kwani aliona giza mbele yake lakini hakufanya hivyo,  hii ni kutokana na kupokea maoni mengi kutoka kwa vijana ambao alikuwa anawashawishi kuingia kwenye siasa.

 

Akifunguka kuhusu changamoto, Jokate amesema  vijana wengi si wavumilivu pale wanapopatwa na changamoto na ndiyo maana wanakata tamaa badala ya kutambua kwamba wakati mzuri wa kujitathmini ni pale mtu anapopatwa na changamoto.

 

Ufuatao ni ujumbe wa Jokate Mwegelo kwa mashabiki wake:

”Amini Mungu ni mwingi wa rehema kamwe hamtupi amtumainiye yeye!! Ahsante Mungu Wangu. Labda ni-share kitu kidogo, kuna muda mwaka jana mwishoni nilikuwa so down nilitamani kukata tamaa na kila kitu kwenye maisha nilikuwa pia sijaelewa vizuri hatma yangu kwenye siasa. Nilikuwa kwenye mkutano mkuu wa chama kuna mdada mmoja kutoka Arusha akanikimbilia na kunikumbatia kwa nguvu sana alikuwa na mama mmoja hivi walikuwa wamekuja kupiga picha namimi.

Huyo dada mdogo hivi akasema ananipenda sana sana na mimi ndio nilimfanya aingie kwenye siasa na akagombea nafasi kupitia mkoa wa Arusha akashinda!! Nikabaki natabasamu. Ikanipa nguvu kubwa ya kupiga moyo konde na kusonga mbele. Nilifurahi kuona kuna mdada nimeweza kumhamasisha na kumpa ujasiri wa kugombea. Unaweza ukawa unapitia mitihani migumu sana kwenye maisha yako lakini inakubidi usikate tamaa saa zingine kwasababu tu ya wale wanaokutegemea, wanaokuangalia na kuvutiwa nawe na kujifunza kupitia maisha yako.

Lakini zaidi kwasababu safari ya mafanikio ina milima na mabonde, inabidi upambane na kiukweli hakuna mafanikio yasiokuwa na changamoto. Na kuna muda changamoto ndio haswa zinatengeneza “character” zetu.
Kikubwa zaidi wakati wa changamoto tukumbuke kuwa wanyenyekevu, wenye kujishusha na kumuomba Mungu aendelee kutupa imani, hekima na busara ya kusubiri wakati wake. Tukumbuke Mungu hamtupi mja wake. Nawatakia Jumapili Njema. Nawapenda Sana. Ahsanteni 🙏🏽”

Comments are closed.