The House of Favourite Newspapers

Emery Akimtaka Ozil wa Hivi, Atafeli

Mesut Ozil

NILIBAHATIKA kumuona Mesut Ozil akiichezea Arsenal kwa mara ya kwanza nikiwa uwanjani msimu uliopita wa Ligi Kuu England.

 

Ilikuwa ni mechi Arsenal wakiwa nyumbani Uwanja wa Emirates jijini London dhidi ya Bournemouth na mwisho wa mchezo walifanikiwa kushinda kwa mabao 3-0, Ozil akiwa ametoa mchango mkubwa katika ushambulizi.

 

Lakini kuangalia kwenye runinga hasa kwa mtu unayependa kuangalia mpira huku ukijifunza, kuna tofauti kubwa sana na kuangalia ukiwa uwanjani. Katika runinga kuna raha yake lakini picha za runinga zinakulazimisha uangalie kwa matakwa ya wataalamu wao.

 

Unapokuwa uwanjani unapata nafasi ya kuangalia mchezo kwa wigo mkubwa sana. Mfano, katika mechi hiyo ya Bournemouth, nilipata nafasi ya kumfuatilia Ozil kwa kiasi kikubwa, niligundua mengi yaliyokuwa yakisemwa juu yake yana ukweli mwingi sana.

Wakati wanaotazama runinga walikuwa wakiangalia mpira ulipokwenda. Mimi sababu nilikuwa uwanjani, zaidi nilimuangalia Ozil ambaye alinishangaza kuona mchezaji wa kiwango chake, tena mchezaji wa kulipwa anafanya alivyofanya.

 

Alionekana hayupo mchezoni, aliendelea kutembea kawaida na katika suala la kukaba ndiyo kabisa. Kwani hata pale alipojitahidi kukaba, alikuwa akiishia kuanguka tu akionekana wazi, lile suala kwamba ni mvivu wa mazoezi, lilikuwa ni usahihi mkubwa.

 

Unaona huo ulikuwa ni wakati wa Arsene Wenger. Lakini zama mpya za Unai Emery nazo zinaonekana kuwa ngumu tena kwa Ozil baada ya kocha huyo kumtaka ajitume na kupambana kwa ajili ya timu.

 

Ukifuatilia kitaalamu, utagundua Ozil ni mchezaji bora kabisa na wa kiwango cha juu kabisa katika maeneo manne ambayo ni krosi, pasi za kuchezesha, pasi za mabao au asisti na upigaji mipira iliyokufa kwa maana ya set pieces.

 

Suala la umiliki wa mpira ni 60% na ile mipira ya kupenyeza pia ni 65%. Lakini maeneo haya mawili, kurejea na timu na kusaidia ukabaji, hovyohovyo kabisa.

 

Ozil hajawahi kubadilika katika maeneo haya tokea akiwa Werder Bremen ya Ujerumani ambayo alianza kuchipukia na ninakueleza hivi kwa kuwa mwaka 2009, nilimshuhudia uwanjani akiitumikia Werder Bremen dhidi ya majirani wa eneo hilo, Hamburger. Ni mtu yuleyule kwa maana ya tabia na mienendo uwanjani.

 

Kati ya makocha ambao wanajulikana kwa kutokubaliana na wachezaji wanaotaka kuonekana ni mastaa au kufanya wanavyotaka wao ni Jose Mourinho. Lakini wakati akiwa Real Madrid, mwisho alikubaliana na aina ya uchezaji wa Ozil.

 

Wenger pia, utaona aliwahi kusema aliyoyasema Emery lakini mwisho alikubaliana na aina ya uchezaji wake na mwisho hadi ameondoka amemuacha akiwa kipenzi cha mashabiki wa Arsenal hasa jijini London.

 

Emery alipaswa kusema kuhusiana na Ozil lakini hana nafasi ya kumbadilisha kwa kuwa moja ya sifa za Ozil ni kuamini aina ya uchezaji wake na mwisho ni misimamo mikali bila ya woga.

 

Ozil anataka klabu imchague na kocha akubaliane naye. Anajua si mchezaji mzuri katika kukaba lakini haamini anaweza kujifunza kuwa bora katika ukabaji kipindi hiki.

 

Hakabi kweli, lakini wakati anaondoka Real Madrid kwenda Arsenal, wachezaji walionekana kutofurahia na walitaka abaki. Maana yake wanaujua mchango wake katika kikosi.

 

Wachezaji wanaujua mchango wake lakini makocha wamekuwa wakimtumia na anafanikiwa kuwaletea matunda na mfano mzuri ni Kocha wa Ujerumani, Joachim Loew ambaye amebeba makombe ya Ulaya na Dunia akiwa na Ozil.

 

Tena Ozil amekuwa ni mchezaji tegemeo katika kikosi. Hii inaonyesha wakati mwingine kocha anaweza kujitahidi kuona mchezaji mvivu lakini mwenye matunda ya ubora katika pasi za uchezeshaji, pasi za mwisho anazopika.

 

Kuna wachezaji wengine wanaweza wasiwe wazuri katika maeneo ya Ozil, ubora wao ukaongozwa na kukaba au ulinzi. Hao wanatumika kuziba mapengo ya Ozil wakati yeye akipambana kuziba ya kwao.

 

Hiyo ndiyo maana ya timu na inawezekana kabisa, Emery analazimika kufanya hivyo kuhakikisha Ozil anaendelea kuwa msaada la sivyo hawatafika mbali pamoja.

 

Misimamo ya Ozil inatokana na asili yake, ni mtu kutoka Uturuki. Hivyo kukosa kitu kwake linaweza lisiwe jambo kubwa sana. Lakini bado anabaki kuwa mmoja wa viungo bora na wenye mafanikio katika soka la kipindi hiki.

 

Anaendelea kufeli katika aina ya uchezaji katika ukabaji au usaidizi wa ulinzi. Lakini timu inaposhambulia, ubora wake unakuwa juu na msaada wake unakuwa “hitajika”.

Comments are closed.