The House of Favourite Newspapers

Ibrahim Ajibu Atamhukumu Kocha Wa Stars

Ibrahim Ajibu.

KILA mtu leo anaiombea timu yetu ya taifa, Taifa Stars ili iweze kupata ushindi kwenye mchezo dhidi ya Cape Verde.

Hakika ni mchezo ambao kila mmoja anausubiri kwa hamu kubwa sana na ushindi tu ndiyo unaweza kutusaidia sisi kusonga kuwa na matumaini kwenye mchezo huo.

 

 

Wengi wanaamini kuwa kwa sasa timu yetu ipo vizuri na inaweza kupata ushindi kwenye mchezo wowote ulioko mbele yao.

 

Hakika ni jambo la kusubiri na tuzidi kuwaombea lakini ukifuata rekodi vizuri utagundua kuwa mara nyingi tumeshindwa kupata matokeo mazuri kila tunapokutana na taifa hili.

 

Sawa ni kweli, lakini haimaanishi kuwa rekodi inacheza uwanjani, wakati tunacheza na Cape Verde huku nyuma hatukuwa na mchezaji hata mmoja wa kimataifa, tulikuwa tukitegemea Simba na Yanga tu ndiyo zitupe wachezaji, lakini leo tunakwenda tukiwa timu nyingine kabisa.

Kocha wa Taifa Stars, Emmanuel Amunike.

Tunkwenda tukiwa na wachezaji zaidi ya saba ambao wapo kwenye kikosi chetu na hivyo wenyeji wetu nao sasa wanagundua kuwa wanakutana na timu bora zaidi kwa sasa kwenye soka la Afrika.

 

Ushindi kwa Stars kwenye mchezo huu utawafanya kuwa kwenye kasi nzuri zaidi kwa kuwa watafikisha pointi tano kama Uganda atafungwa na Lesotho ina maana kuwa Taifa Stars watakuwa kileleni kwenye kundi.

 

Lakini jambo la kufurahisha ni kwamba siku nne baadaye Stars itakuwa hapa nyumbani kuvaana tena na timu hiyo na kama itashinda michezo yote miwili ina maana kuwa itafikisha pointi nane na hivyo kama itapata pointi kwenye mchezo wake mwingine dhidi ya Lesotho basi itakuwa nafasi kubwa kwa timu hiyo kufuzu.

 

Ni vizuri tukiwaombea kuhakikisha kuwa wanapata ushindi kule, lakini wakati mwingine naona kuna tatizo kubwa kwenye uchaguzi wa wachezaji wa timu hii.

 

Nafikiri kuna wakati tunatakiwa kuwa wakweli hata kama kazi ya kuchagua ni ya kocha, lakini kuna vitu vinaonekana kutokuwa vizuri na hata kama Stars watapoteza mchezo wa leo lazima lawama zitakuwepo.

 

Ni jambo la ajabu Stars kuwa bila mshambuliaji bora kwa sasa hapa nchini, Eliud Ambokile, jiulize mshambuliaji ndiye mchezaji bora kwenye ligi kwa sasa, ndiye kinara wa mabao, amefunga mabao sita halafu hayupo kwenye kikosi cha Taifa Stars.

 

Nafikiri kuna tatizo hata kama kocha alikuwa hamtaki, lakini kumwita kungempa morali ya juu zaidi na kuendelea kupambana, lakini kama hamtumii leo basi angeanza kumuandaa kwa ajili ya miaka kadhaa mbele.

Nafikiri wakurugenzi wa benchi la ufundi la Stars wanatakiwa kumshauri wakati mwingine kwa maendeleo ya soka la nchi hii.

 

Pia mchezaji anayeonyesha kiwango cha juu zaidi kwa sasa kwenye ligi ni Ibrahim Ajibu ambaye hadi sasa ndiye mchezaji aliyehusika kwenye mabao mengi zaidi kwenye ligi kuliko mwingine yoyote.

Sijui kwa nini kocha hakumwita Ajibu, lakini ni jambo la ajabu kumuacha kiungo mshambuliaji kama huyu kwenye timu yetu ya taifa.

 

Nafikiri kocha anaweza kusema kuwa atamwita siku nyingine, lakini kwangu naamini haitakuwa sawa kwa kuwa hakuna anayefahamu kama Ajibu atabaki kwenye kiwango alichonacho sasa kwa muda gani.

Comments are closed.