The House of Favourite Newspapers

HAMTAAMINI KOCHA AL AHLY AINGIWA MCHECHETO

KOCHA wa Simba,Patrick Aussems anaamini asilimia zote kwamba kikosi chake kiko fiti kisaikolojia kwa mchezo wa leo usiku dhidi ya zmjini hapa. Amewaomba mashabiki na Watanzania wawaombee dua njema kwani watapigana kufa na kupona kwenye mechi hiyo itakayoonyeshwa na vituo vya ZBC2 na Supersport 4&8 saa 4 usiku wa leo.

 

Katika mechi hiyo ya Ligi ya Mabingwa itakayopigwa kwenye Uwanja wa Borg El Arab, kocha huyo amewaonyesha wachezaji video za Ahly na lakini uwanjani akawafundisha kwa vitendo jinsi ya kucheza nao. Simba ambao walitua hapa Jumatano alfajiri, waliamua kuwahi ili kuzoea mapema hali ya hewa ambayo ni baridi kwa sasa.

Aussems ambaye amewazuga waandishi wa habari wa hapa kwamba hatarajii kufanya maajabu yoyote kwenye mechi ya leo, aliliambia Championi kwamba anafurahia morali kubwa waliyokuwa nayo wachezaji wake katika kuelekea mchezo huo.

 

Aussems aliongeza kuwa, pia walifanikiwa kuziangalia picha za video ambapo walifanikiwa kubaini mbinu mbalimbali za wanazotumia wapinzani wao wanapokuwa ndani ya uwanja lengo la kufanya hivyo ni kuhakikisha timu yake inapata ushindi. Aliongeza kuwa, hana hofu ya mchezo huo licha ya hali ya hewa ya baridi kali waliyoikuta, kwani vijana wake wamefanya mazoezi vizuri.

 

“Tumefanya mazoezi kwa siku mbili na wachezaji wangu tangu tumefika hapa kwa muda wa usiku na kikubwa kuzoea hali hiyo ambayo tutakutana nayo katika mechi. “Kabla ya mazoezi ya siku ya kwanza  tulipata muda wa kuangalia video mbili za mechi zao za mwisho tukiwa hapa Misri.

 

“Hivyo, tumeshajua cha kukifanya katika mchezo huo na kikubwa tutashambulia na kulinda goli letu ndani ya wakati mmoja hilo ndilo jambo la msingi,” alisema Aussems.

 

KOCHA AL AHLY AINGIA MCHECHETO

Hali ni tofauti kwa Kocha Mkuu wa Al Ahly, Martin Lasarte ambaye ameanza kulia na ugumu wa ratiba. Lasarte amelitupia lawama Shirikisho la Soka Misri kutokana kuwachezesha mechi za ligi kila baada ya saa 72 hali inayosababisha kuongezeka kwa majeruhi kikosini mwake.

 

“Naamini fiziki ya wachezaji wetu ipo sawa. Tatizo lililopo ni kwamba tunacheza mechi za ligi kila baada ya saa 72 kitu ambacho siyo sawa  kwa kuwa tunaongeza idadi ya wachezaji majeruhi.”

 

Katika mchezo wa leo, Ahly wameruhusiwa kuingiza mashabiki 10,000 na wengine zaidi ya 70,000 wamezuiwa na hawatapewa tiketi kabisa. Uwanja ambao mechi itapigwa unaingiza mashabiki 86,000 lakini mamlaka za usalama zimesisitiza kwamba tiketi zitakazouzwa ni 10,000 isizidi hata nukta, jambo ambalo huenda likapunguza vurugu na kuipa ahueni Simba.

 

YAVUTA WAWILI FASTA Kufuatia hofu ya majeruhi kuongezeka, Al Ahly imevuta majembe mengine mawili ambayo yataingia kuongeza nguvu kwenye michuano hiyo. Awali Al Ahly walitangaza wachezaji 23 wa kushiriki michuano hiyo lakini sasa imewaongeza wawili ambao ni beki wa kati Rami Rabia na mlinzi wa kushoto, Mahmoud Wahid.

Wahid amejiunga Al Ahly kwenye usajili mdogo uliofungwa Januari 31, mwaka huu akitokea El-Makassa na Rabia ameongezwa kwenye michuano hiyo baada kukosekana kwa misimu miwili kutokana na kuwa majeruhi.

 

WACHEZAJI SIMBA KUWA MAMILIONEA

Mtendaji Mkuu wa Simba (CEO), Crescentius Magori aliliambia Championi kuwa, endapo wachezaji watapambana na kushinda mchezo huo wameandaliwa donge nono la fedha huku akigoma kusema ni kiasi gani.

 

Hata hivyo Championi linafahamu kuwa, endapo Simba watashinda mchezo huu basi kila mchezaji atalamba Sh milioni 4 hawa ni wale ambao watacheza mechi, watakaokuwa benchi kila mmoja Sh mil 3, wakati watakaokuwa jukwaani na ambao hawajasafiri na timu kila mmoja atapata Sh mil 1.

Comments are closed.