The House of Favourite Newspapers

Al Ahly Wavunja Mazoezi Yanga SC

Kikosi cha timu Ya Yanga.

KATIKA kuhakikisha anapata pointi tatu mbele ya watani wao wa jadi Simba, Kocha Mkuu wa Yanga, Mkongoman, Mwinyi Zahera amevunja programu ya mazoezi ili awatazame wapinzani wake waliotarajiwa kuvaana na Al Ahly ya Misri. Simba jana.

 

iliwakaribisha Al Ahly kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam waliovaana katika mchezo wa marudiano wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Baada ya mchezo huo, Simba itacheza mchezo wake wa Ligi Kuu Bara na Yanga Jumamosi ijayo kwenye Uwanja wa Taifa, unaotarajiwa kujaa upinzani mkubwa kutokana na upinzani unaokuwepo.

 

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatano, kocha huo alisitisha programu ya mazoezi ya jioni yaliyotarajiwa kufanyika kwenye Uwanja wa Chuo cha Biblia, Bigwa nje kidogo ya Mji wa Morogoro ili waangalie mechi ya Simba.

Mtoa taarifa huyo alisema, timu hiyo jana ilifanya mazoezi mara moja pekee saa mbili kamili asubuhi kabla ya kumaliza saa tano na baada ya hapo walirudi kambini kwa ajili ya kuusubiria mchezo wa Simba na Al Ahly. Aliongeza kuwa, kikubwa kocha huyo alikuwa anataka wautazame mchezo huo wote na kuangalia mbinu wanazozitumia katika kushambulia na kulinda lango lao kabla ya kuwavaa Jumamosi hii.

 

“Tulifika na kuweka kambi hapa Morogoro jana (juzi) Jumatatu tukitokea Tanga tulipotoka kucheza mchezo wa ligi na JKT Tanzania kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wetu na Simba.

 

“Tukiwa hapa, kocha alitoa programu ya kufanya mazoezi mara mbili kwa siku ambayo tuliianza leo (jana) asubuhi kwa kufanya mazoezi, lakini jioni kocha alisitisha programu hiyo kwa ajili ya kuuangalia mchezo wa Simba na Al Ahly,” alisema mtoa taarifa huyo.

 

Alipotafutwa Zahera kuzungumzia hilo, alisema: “Kama nilivyosema awali, baada ya mchezo na JKT Tanzania ninaanza maandalizi ya mchezo unaofuata wa ligi dhidi ya Simba ambayo tayari nimeyaanza na kikubwa ninahitaji pointi tatu.”

Comments are closed.