The House of Favourite Newspapers

Zahera Aondoka na nyota 20 Kwenda Mwanza

Kikosi cha timu ya Yanga.

KOCHA Mkuu wa Yanga Mkongomani, Mwinyi Zahera jana usiku alitarajiwa kurejea jijini Dar es Salaam akitokea nyumbani kwao DR Congo kabla ya kesho Alhamisi kukwea pipa kwenda mkoani Mwanza na nyota wake 20.

 

Kocha huyo alikuwepo nyumbani kwao DR Congo akiwa kwenye majukumu ya timu ya taifa ya nchi hiyo anakofundisha kama kocha msaidizi ilipokuwa ikicheza na Liberia katika fainali za kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika na kufanikiwa kufuzu.

 

Mkongomani huyo, aliukosa mchezo uliopita wa Ligi Kuu Bara walipocheza na Lipuli FC ambao walifungwa bao 1-0

ambalo lilifungwa na Haruna Shamte.

 

Akizungumza na Championi Jumatano, mratibu wa timu hiyo, Hafidh Saleh alisema kuwa kocha huyo alitarajiwa kurejea Dar jana kwa ajili ya mchezo huo wa Kombe la Shirikisho.

 

Saleh alisema, kocha huyo alizuia timu hiyo isisafiri hadi yeye atakaporejea nchini kwa ajili ya kujiunga na kikosi hicho kilichopania kuchukua Kombe hilo la Shirikisho msimu huu.

 

Aliongeza kuwa, tayari ameshafanya mawasiliano na kocha huyo kwa njia ya simu na kuahidi kurejea jana tayari kuungana na kikosi hicho na kuanza safari ya kuelekea Mwanza kwa ajili ya mchezo huo.

 

“Kocha amezuia msafara wa timu kwenda Mwanza hadi yeye atakaporejea nchini kwa ajili ya kuungana na timu iliyopanga kusafiri kwa ndege keshokutwa (kesho) Alhamisi.

 

“Katika msafara huo, kocha amependekeza kusafiri na wachezaji 20 pekee pamoja na viongozi watano wa benchi la ufundi.

 

“Wachezaji ambao watakosekana katika msafara wetu hadi hivi sasa kutokana na sababu ya majeraha na adhabu za kadi ni wanne, Abdul (Juma), Mwinyi (Haji) na Banka (Issa Mohamed) wote wenye majeraha na Ninja (Abadallah Shaibu) yeye anatumikia adhabu ya kifungo cha michezo mitatu,” alisema Saleh.

Stori na Wilbert Moandi na Khadja Mngwai

Comments are closed.