The House of Favourite Newspapers

CHELSEA BINGWA EUROPA, YAICHARAZA ARSENAL MABAO 4-1 (Picha +Video)

CHELSEA jana ilitwaa taji la Europa baada ya kuicharaza Arsenal mabao 4-1 kwenye fainali iliyokutanisha timu mbili za London zilizokabiliana katika Uwanja wa Olimpiki mjini Baku nchini Azerbaijan.


Hii ni mara ya pili kwa Chelsea kutwaa taji hilo kwani iliibuka kidedea kwenye michuano hiyo katika msimu wa 2012/13. Pia Chelsea imeongeza taji jingine la Ulaya kwenye kabati lake baada ya kunyakua kwa mara ya sita kombe la michuano ya bara hilo.

 

Chelsea imewahi kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya (2011/12), Ligi ya Europa (2012/13), Kombe la Washindi Ulaya (1970/71 na 1997/98) na UEFA Super Cup mwaka 1998.

 

Arsenal kwa upande wao kwa kipigo hicho ina maana wamebakia na rekodi ya kutwaa mara moja tu taji la Ulaya ambalo walilipata mwaka 1994 waliponyakua Kombe la Washindi.

Olivier Giroud aliipatia Chelsea bao la kwanza kwa kichwa cha kuchupa baada ya kuunganisha krosi ya Emerson mnamo dakika ya 49.

 

Bao hilo maridadi dhidi ya timu yake ya zamani ya Arsenal lilimfanya Giroud sasa kuwa mfungaji bora wa michuano ya Ligi ya Europa msimu huu wa 2018/19 baada ya kufikisha mabao 11.

Hata hivyo, Giroud hakushangilia baada ya kufunga bao lile badala yake alipiga magoti na kunyoosha mikono juu kama vile alikuwa anawaomba radhi mashabiki wa Arsenal, ambayo aliichezea kwa miaka sita kuanzia 2012 hadi 2018.

 

Chelsea ilipata bao lake la pili katika dakika ya 60 likipachikwa kiufundi na Pedro alipomalizia krosi ya Eden Hazard. Mabao hayo yaliivuruga Arsenal, ambayo ilijikuta ikipigwa bao la tatu lililopatikana kwa penalti.

Hazard, ambaye anatazamiwa kutimkia Real Madrid ndio alifunga penalti hiyo katika dakika ya 65, ambayo ilitolewa baada ya beki wa Arsenal, Ainsley Maitland-Niles kumwangusha kwenye eneo la hatari, Giroud.

Arsenal ilipata bao la kufutia machozi angalau katika dakika ya 69 baada ya Alex Iwobi kupiga shuti la umbali wa mita 20 lililomshinda kipa wa Chelsea, Kepa Arrizabalaga. Hazard, ambaye bila shaka ndio alikuwa anawaaga Chelsea alipachika bao la nne la timu hiyo katika dakika ya 72 baada ya kugongeana vyema na Giroud.

Comments are closed.