The House of Favourite Newspapers

Yanga: Tunawaumbua Wabotswana Kwao Leo

POTEZEA hujuma zao walizozipanga na kugonga mwamba huko Shirikisho la Soka Afrika ‘Caf’, leo mbona kazi wanayo hao Township Rollers mbele ya Yanga!

 

Unaambiwa Kocha Mfaransa, Mwinyi Zahera hataki masihara amesisitiza kwamba atapanga mziki wote na ndani ya dakika 10 anataka kuwanyamazisha.

 

Kipa wa Rollers aliyedaka mechi ya Dar es Salaam amekiri kwamba leo atalazimika kufanya kazi ya ziada kwa guu la kushoto la Patrick Sibomana ambalo lilimsumbua sana Taifa.

 

Yanga ni kama wana kiburi f’lani hivi kilichowafanya wavamie mapema kwenye mji wa Gaborone, Botswana ambako Rollers ndiyo maskani kwao na kuweka kambi ya maandalizi ya mchezo huo wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Siyo kawaida kwa timu pinzani kufika mapema kwa mwenyeji wake na kuweka kambi, lakini Yanga wamefanya hivyo kwani tangu Jumatatu iliyopita saa sita mchana walikuwa tayari wametua nchini humo.

Ni mchezo mgumu utakaokuwa mtamu na upinzani mkubwa kwani kila timu imejiandaa kupata matokeo mazuri ya kushinda ni baada ya mechi ya awali iliyochezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kutoka sare bao 1-1.

 

Kocha Zahera ameweka wazi mapema tu kuwa hataki utani na amepanga kushusha mziki mzima ambao anataka kuona timu yake inapata bao ndani ya dakika 10 za kwanza ili kuwaondoa mchezoni wapinzani.

Benchi la ufundi la Rollers limeonekana kupagawa kwa jinsi Yanga inavyopanguliwa kila mara na wanategemea kikosi kipya tofauti na kile cha Dar es Salaam.

 

Kama kawa golini anakaa yule kipa namba mbili wa Taifa Stars, Metacha Mnata. Njoo kwenye safu ya ulinzi pembeni, kulia yupo Paul Godfrey ‘Boxer’ ambaye mchezo uliopita alishindwa kumalizia mchezo huo baada ya kupata majeraha ya goti na kushoto yupo, Ally Mtoni ‘Sonso’.

 

Ukipiga jicho pale katikati utakutana na miamba, Kelvin Yondani, Mghana Lamine Moro.

Safu ya viungo atakuwepo fundi Mohamed Issa ‘Banka’, Mapinduzi Balama, Papy Tshishimbi mbele wakisimama Juma Balinya, Sadney Urikhob na winga matata anayezua hofu zote huko Rollers Mnyarwanda, Patrick Sibomana ambaye ni hatari kwa mipira iliyokufa hadi kipa wa Rollers, Wagarre Dikago akakiri jamaa ni hatari.

 

Akizungumzia mchezo huo Zahera alisema kuwa: “Nikiangalia yale mazoezi ambayo tumefanya tangu tumefika hapa Botswana, mengi ni yale ambayo tunapaswa kwenda mbele kushambulia goli la wapinzani.

 

“Tumefanya programu hiyo kwa kipindi chote tulichofika hapa na kikubwa tunataka kupata ushindi wa hapa ugenini kitu ambacho kinawezekana, kama tumeweza kufunga nyumbani kwanini tushindwe ugenini?

 

“Ninataka kuona idadi ya washambuliaji ikiwa kubwa golini tukiwa na mpira tukishambulia na katika hilo sitaki kuona washambuliaji wangu wakibahatisha golini katika kufunga mabao.

“Nawatambua vizuri wapinzani wangu ubora wao umejificha kwenye viungo jambo ambalo nimelifanyia kazi kwa muda mrefu kwa sasa wameiva na wanatambua namna ya kuwadhibiti wapinzani.

“Nahitaji kufunga mabao mawili ya haraka kisha niyalinde ili kusonga mbele kwani kazi ya kupata matokeo ugenini sio rahisi ila ninawaamini wachezaji wangu,” alisema Zahera

Comments are closed.