The House of Favourite Newspapers

Zahera Akamilisha Hesabu, Awaita Waarabu

KOCHA Mkuu wa Yanga Mkongomani, Mwinyi Zahera, amesema kuwa maandalizi ya kikosi chake yamekamilika ambacho kipo tayari kupata ushindi watakaposhuka uwanjani kupambana na Pyramids FC ya nchini Misri.

 

Timu hizo zinatarajiwa kuvaana kesho Jumapili kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza mara baada ya kubadilishwa uwanja ambao ulitakiwa upigwe Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

 

Yanga watawavaa Pyramids wanaonolewa na Kocha Mfaransa, Sebastien Desabre kesho wakiwa wametoka kupata ushindi wa Ligi Kuu Bara baada ya kuwafunga Mbao FC bao 1-0 na kupata morali ya kupambana na kupata matokeo mazuri katika mchezo huo mgumu.

Akizungumza na Championi Jumamosi, Zahera alisema jana Ijumaa usiku alitarajiwa kufanya kikao na wachezaji wake hotelini sambamba na kutazama video za mechi za mwisho ambazo wapinzani wamezicheza.

 

Zahera alisema kuwa, lengo la kuzitazama video hizo ni kuzijua mbinu za uchezaji wanazozitumia wakiwa ugeni na kuwajua wachezaji hatari kwa ajili ya kuwadhibiti.

 

Aliongeza kuwa tayari ameshamaliza mazoezi ya kiufundi ya uwanjani, hivyo kilichobakia ni wachezaji kuonyesha watakapokuwa uwanjani na kikubwa amemtaka kila mchezaji atimize majukumu yake, mabeki kuzuia na kupunguza hatari, viungo kuchezesha timu na washambuliaji kufunga mabao.

“Nina imani kubwa ya kupata matokeo mazuri ya ushindi wa hapa nyumbani, kwani tayari wachezaji wangu nimewapa maelekezo ya jinsi ya kucheza tukiwa kwenye uwanja wa nyumbani.

 

“Nimewaambia wachezaji wangu hatutaki kuruhusu bao golini kwetu, kwa maana kama hatufungi, basi tusiruhusu bao golini kwetu.

 

“Hatutakiwi kuruhusu bao nyumbani, kwani ni hatari kwetu na ili tufanikiwe tufuzu hatua ya makundi ni lazima tupate ushindi wa mabao zaidi ya mawili kabla ya kurudiana kwao.

 

“Kama tukipata ushindi mnono wa mabao mengi, tutampa presha kubwa mpinzani wetu mchezo wa marudiano, hivyo sitaki kuona tukiruhusu bao zaidi ya sisi kufunga,” alisema Zahera.

WACHEZAJI WAWATOA HOFU MASHABIKI

Wachezaji wa Yanga, kupitia kwa kiungo mkongwe, Papy Tshishimbi wamewaondoa hofu mashabiki wa timu hiyo kwa kuwaambia waende uwanjani kwa wingi kwani wana imani hawatawaangusha.

“Ninaamini sapoti yao uwanjani ndiyo itakayotupa sisi nguvu wachezaji ya kupambana na kuwapa furaha ya matokeo mazuri ya ushindi.

 

“Hivyo, niwaondoe hofu mashabiki wa Yanga kuwa ushindi utapatikana katika mchezo huo, ninafurahia kuona baadhi ya wachezaji wenye majeraha wakirejea tayari kwa ajili ya mchezo huo,” alisema Tshishimbi.

 

Kikosi cha Yanga kinatarajiwa kuwa hivi; kipa Metacha Mnata, Juma Abdul, Ally Mtoni ‘Sonso’, Ali Ali, Kelvin Yondani, Abdulaziz Makame, Mapinduzi Balama, Feisal Salum ‘Fei Toto’, Sadney Urikhob, Papy Tshishimbi na Patrick Sibomana.

Stori Wilbert Molandi, Dar es Salaam

Comments are closed.