The House of Favourite Newspapers

Hesabu za Meddie Kagere leo Arusha ni balaa!

STRAIKA kiwembe wa Simba, Meddie Kagere raia wa Rwanda ameweka bayana anawaingia kiakili Singida United ambao wanacheza nao leo Jumapili huku lengo lake ni kutaka kuendeleza kutunisha mfuko wake wa mabao.

 

Kagere ataliongoza jeshi la Simba kusaka pointi tatu katika mechi ya Ligi Kuu Bara ambayo watacheza na Singida United mkoani Arusha katika Dimba la Sheikh Amri Abeid.

 

Kagere mwenye mabao saba hadi sasa, ameliambia Spoti Xtra, kuwa licha ya matokeo mabaya ambayo wanayo Singida United lakini hilo halimfanyi awadharau badala yake anawaingia kwa akili kubwa kuona anaipa pointi tatu timu yake.

“Ndiyo tunatambua Singida hawana matokeo mazuri katika ligi, lakini hilo halifanyi eti ndiyo tuwadharau. Tunawachukulia kuwa wapinzani wetu na watatupa changamoto kwenye mechi hii, hivyo kitu cha muhimu kuwaingia kiakili.

 

“Lakini kitu cha muhimu zaidi ni kupata matokeo mazuri, tunahitaji pointi tatu kutoka kwao kama ambavyo tumefanya katika mechi tano zilizopita za ligi pia mimi nahitaji kufunga zaidi kwa ajili ya kuchangia ushindi wa timu yangu,” alisema Kagere.

PACHA YA FRAGA

Kilichowapata Azam FC, ndicho walichoandaliwa Singida United, mara baada ya kocha wa Simba Patrick Aussems kupanga kuwatumia viungo wake wawili, Mzamiru Yassin pamoja Gerson Fraga katika mchezo huo.

 

Fraga na Mzamiru walinoga sana kwenye mchezo wa mwisho waliocheza kwenye Uwanja wa Taifa dhidi ya Azam FC wakati Simba ikishinda bao 1-0.

 

“Nimepanga kufanya mabadiliko kadhaa ya wachezaji kutokana na hali ya kiwanja ila Mzamiru na Fraga walionyesha kiwango kizuri kwenye mchezo wa mwisho dhidi ya Azam FC, hivyo bila shaka watabaki kama walivyo,” alisema Kocha wa Simba, Patrick Aussems.

 

Singida inarusha karata yao ya nane huku wakijaribu kutafuta ushindi wa kwanza msimu huu ili waweze kujinasaua kutoka mkiani.

Comments are closed.