The House of Favourite Newspapers

Yanga Watengewa 10m Waiue JKT, Uhuru leo

LEO Ijumaa kwa mara nyingine bosi mpya wa Yanga, Charles Mkwasa atakuwa na kibarua cha kusaka ushindi wake wa pili mbele ya JKT Tanzania tangu apewe kuiongoza timu hiyo, ambapo kitu kizuri kwake ni kuongezeka kwa majembe yake ambayo yalikuwa pembeni kutokana na majeruhi.

 

Mkwasa alipewa nafasi ya kukaimu nafasi ya Kocha Mkuu wa Yanga baada ya kuondoshwa na Mkongomani Mwinyi Zahera mapema mwezi huu. Huu unakuwa mchezo wa pili kwa Mkwasa kuiongoza Yanga tangu apewe timu hiyo mechi yake ya kwanza aliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Ndanda FC mkoani Mtwara.

Msemaji wa Yanga, Hassan Bumbuli amesema kuwa katika mchezo huo watakuwa na wachezaji wao, Mohammed Issa ‘Banka’, Lamine Moro raia wa Ghana na Ali Ali ambao walikuwa nje kutokana na majeraha.

 

“Licha ya kwamba mechi yetu ilitakiwa kuchezwa Jumamosi na kurudishwa nyuma Ijumaa lakini sisi tuko vizuri kwa ajili ya mechi hii. Kitu kizuri ni kwamba wachezaji wetu ambao walikuwa nje ya uwanja wamerudi na watacheza mechi hii. “Wale wenye majeraha ya muda mrefu akiwemo Paul Godfrey ‘Boxer’ bao.

 

Wengine watakaokosekana ni waliokuwa timu ya taifa, Kelvin Yondani na Abdulaziz Makame, hawakuwemo katika mazoezi ya mwisho ambayo timu iliyafanya,” alisema Bumbuli.

 

Naye Mhamasishaji wa timu hiyo, Antonio Nugaz alisema: “Uzuri ni kwamba mzigo wa milioni 10 kama timu ikishinda upo palepale na nitawakabidhi mwenyewe kitita hicho cha fedha. Lakini pia tumeanza mazungumzo na wadhamini wetu wengine kwa ajili ya kuongeza kiasi hicho cha fedha na inawezekana kwenye mechi hii isiwe tu hiyo milioni 10 bali kukawa na zaidi ya hapo.”

Comments are closed.