The House of Favourite Newspapers

Nilifanya Mapenzi na Maiti 20 Nitajirike – 15

maiti-coverILIPOISHIA…

“Ichome taswira hiyo kwa hicho kisu,” iliniambia.

“Unasemaje?” niliuliza huku jasho likinitiririka, hakika niliogopa kwani nilijua kwamba endapo ningeichoma taswira ile, basi baba yangu angekufa.

“Ichome…” sauti ya mganga iliniambia, nikabaki nikitetemeka.

SONGA NAYO…

Nilibaki nikitetemeka, sikujua ni kitu gani nilitakiwa nikifanye mahali hapo. Jinsi mganga yule alivyoniambia kwamba niichome taswira ya picha ya baba yangu katika kioo kile.

Kumuua baba yangu! Kilikuwa kitu kisichowezekana kabisa, nilikumbuka namna alivyokuwa akiyasumbukia maisha yangu kipindi cha nyuma, nilikumbuka jinsi alivyokuwa akijinyima kwa ajili yangu, yaani nipate maisha mazuri, hakujali kama alikuwa akila au la, alichokijali ni mimi kula na kulala sehemu nzuri.

Nilifanikiwa, nilitaka nimuonyeshee baba kwamba hatimaye ule umasikini uliokuwa umetutafuna kwa kipindi kirefu usingekuwepo tena, nilitaka niwaonyeshee wanakijiji kwamba kitendo changu cha kuondoka nyumbani kwetu na kwenda kijijini kilikuwa sahihi kwani kile nilichokitaka, tayari nilikipata.

Nilibaki nikiiangalia taswira ile, mawazo yote hayo yalinijia kichwani mwangu wakati ambao nilishika kisu kile. Mapigo ya moyo yalikuwa juu mpaka kuhisi kwamba kama angepita mtu yeyote mahali hapo basi angeyasikia kwa jinsi yalivyokuwa yakidunda.

“Zakia, ichome taswira hiyo,” niliisikia sauti ya mganga huyo.

“Siwezi…ninashinwa,” nilisema pasipo kuogopa kitu chochote kile.

“Kwa nini unashindwa?” aliniuliza.

“Nilitafuta utajiri kwa ajili ya wazazi wangu, sasa kwa nini nimuue na wakati kila kitu nilichokuwa nacho naye alitakiwa kukiona?” niliuliza swali nililoliona kuwa na hoja, ila kwa mganga huyo, halikuwa na hoja yoyote ile.

“Basi acha tuuchukue utajiri wetu, utarudi na kuwa masikini, tena masikini mkubwa zaidi ya ulivyokuwa,” aliniambia mganga yule.

Nilichanganyikiwa, sikutaka kuuachia utajiri ule kwani tayari nilishaonja utamu wake, nilitaka kuwa nao milele, yaani hata maisha baada ya kifo kama kungekuwa na matumizi ya fedha basi nitakapokufa niende nao kwani ulikuwa mtamu mno.

Kitendo cha kuniambia mamneno hayo, nikashindwa kuvumilia, sikuwa tayari kuona utajiri huo ukiondoka mikononi mwangu, ilikuwa ni lazima nimuue baba yangu.

Kwanza nikafikiria kwamba alikuwa mzee, hakuwa na nguvu za kutosha, kama ningemuacha basi mwaka huohuo hapo baadaye ilikuwa ni lazima afariki kwani umri ulikuwa umekwenda sana.

Kitendo cha kufikiria hayo, nikashangaa kupata majibu kwamba ilikuwa ni lazima nimuue, kama nisingemuua mimi basi angekufa miezi michache ijayo. Sikutaka kujiuliza tena, mawazo hayo yakanipa nguvu na hivyo kuchoma taswira ile. Nilipomaliza, mganga akaniambia niwashe gari, nikawasha na kuanza kuondoka mahali hapo.

Nilichukua saa mbili, nikafika katika Kijiji cha Mbingu. Kwanza wanakijiji walipoliona gari hilo, wakashangaa sana, hakukuwa na gari lolote la kifahari lililowahi kufika kijijini hapo, magari yote ambayo yaliwahi kufika yalikuwa yale ya mizigo ambayo yalifuata nafaka hapo kijijini, sasa watu wakawa wanajiuliza, je, huyo aliyeingia na gari la kifahari alikuwa nani?

Sikutaka kuteremka, unapofika kijijini kwetu, kwa jinsi ilivyokuwa ilikuwa vigumu sana kufika na gari mpaka karibu na nyumba yetu, ilikuwa ni lazima ufikie mbali, uteremke na kuanza kutembea kuelekea huko.

Watoto na watu wengine walishasogea mahali gari lilipokuwa na kuanza kuliangalia. Hawakujua ndani ya gari hilo kulikuwa na nani kwani vioo vya gari hilo vilikuwa ‘tinted’.

Najua walikuwa na maswali, nilichokifanya baada ya kukaa ndani ya gari kwa dakika kama tano, nikateremka, wengi waliponiona, hawakunifahamu, kwa jinsi nilivyovaa, miwani yangu na nguo za thamani, hakukuwa hata na mtu mmoja aliyehisi kwamba mwanamke huyo aliyekuwa akitembea nilikuwa mimi.

“Huyu ni Mzungu?” nilimsikia mtoto mmoja akiuliza, watoto wengine walikuwa wakinifuata kwa nyuma.

Nilitembea mpaka nilipofika karibu na nyumba yetu, kilichonishtua ambacho sikuwa nikikumbuka ni msiba uliokuwapo. Watu zaidi ya hamsini walikuwa mahali hapo, nilisikia vilio kutoka kwa watu kadhaa waliokusanyika nyumbani kwetu, nilishangaa lakini baada ya kukumbuka kwamba niliichoma taswira ya baba katika kioo kile nilichopewa ndani ya gari, moyo wangu ukaumia sana kwani niligundua kwamba mimi ndiye niliyemuua baba yangu.

“Baba amekufa! Nimemuua baba!” nilijisemea moyoni na kuanza kuelekea kule walipokusanyika watu wengi.

Wanaume wengi ndiyo waliokuwa wamekusanyika mbele ya nyumba yetu, kama walivyokuwa watu wengine kule nilipoaki gari, hata hapo hakukuwa na yeyote aliyegundua kwamba msichana aliyefika, ambaye alivalia kisasa alikuwa yule Zakia aliyeondoka mwaka mmoja uliopita.

Nilisalimia, wakabaki wakinishangaa, nikaingia ndani, nikaelekea mpaka chumbani ambapo nilikuta ndugu zangu kadhaa wakiwa na mama yangu. Hakukuwa na mtu aliyenigundua zaidi ya mama ambaye baada ya kuniona tu, kilio kikaongezeka, kila mtu akabaki akijiuliza mimi ni nani.

Moyo wangu uliumia mno, sikuamini nilichokuwa nikikona, sikuwahi kumuona mama yangu akilia kama siku hiyo, nilijuta, mimi ndiye niliyemuua baba kwa sababu ya tamaa za kubaki na utajiri niliokuwa nao.

Nikaungana nami, nikajitambulisha kwamba nilikuwa nani, watu wote wakashangaa. Kitu cha ajabu kabisa kutokea, moyo wangu haukuwa na maumivu makubwa sana, nilisikitika kwa kuwa baba alifariki lakini kusema kwamba nilie sana kama watu wengine, kwangu haikutokea kabisa.

Watu walinishangaa, walijiuliza sana kuhusu mimi, nilionekana kabisa kwamba nilikuwa na fedha, nilikuwa na utajiri mkubwa, sikutoka ndani, nilibaki nikiwafariji wengine, harakati zote zikaendelea siku hiyo, saa kumi jioni, tukaenda kuzika katika makaburi ya kijiji na kisha kurudi.

Kila niliyemwangalia, alionekana kuwa na hamu ya kufahamu, utajiri mkubwa namna hiyo niliutoa wapi? Kwani hata gari nililokuwa nalo, lilikuwa gumzo sana kijiji kizima na hata vijiji vya jirani . Eti yule Zakia aliyekataliwa kuolewa na wanaume kibao, leo alikuwa tajiri! Haikuwaingia akilini.

Comments are closed.