The House of Favourite Newspapers

Hadithi ya Eric Shigongo: Dimbwi la Damu-05

ERIC SHIGONGO DIMBWI LA DAMU-05

GLOBAL PUBLISHERS

Roho mkononi Tehran:
Katika nchi zilizopiga vita madawa ya kulevya kwa nguvu zote ilikuwa ni nchi ya Kiislam ya Iran! Ndani ya nchi hiyo adhabu kwa mtu aliyekamatwa na madawa ya kulevya ilikuwa ni kifo kwa kupiga risasi mbele ya halaiki ya watu ili kuwa fundisho kwa wengine.
AbdulAziz Akem raia wa Iran na Samweli Mazengo raia wa Tanzania waliifanyabiashara hii kwa nguvu zao zote, walikuwa safari kuelekea Iran lakini wamekwama nchini Tanzania wakitokea India! Safari hiyo ilikuwa ni kama safari ya kifo hakuna mtu hata mmoja kati yao aliyekuwa na uhakika wangerudi salama kwani wakiwa Dar es Salaam walisikia na kushuhudia kupitia katika luninga watu wakipigwa risasi hadharani na kufa baada ya kukamatwa na madawa ya kulevya aina ya heroine!
“Tutafanyaje sasa rafiki yangu!” Samweli alimuuliza AbdulAziz.
“Kwa kweli sijui, ila naogopa sana kuendelea na safari hii!”
“Na tajiri utamwambia nini”
“Siwezi kwenda kufa mimi!”
Waliendelea kuongea wakiwa wamekaa mbele ya hoteli maarufu Mjini Arusha iliyoitwa Bin One, hali zao hazikuwa nzuri madawa kwani waliyoyameza tumboni mwao yalionekana kutishia sana uhai wao.
“Cha kufanya tuyatoe tumboni na kuyaweka kwenye sanduku kisha tutafute mtu yeyote hapa Tanzania tujifanye tunamsaidia kwenda Ulaya na tumkabidhi sanduku hilo na tusafiri naye hadiTehran akikamatwa shauri yake sisi tunaingia mitini!”
*****
Jioni ya siku hiyo baada ya kufanya kazi zake za kuosha magari mitaani Nicky alikuwa amechoka aliamua kupitia maeneo ya mjini akiwa njiani kuelekea nyumbani kwao Njiro! Alikuta magari mengi sana mbele ya hoteli ya Bin one akaamua kuingia ndani kutafuta kibarua cha kuosha magari hayo, alisikia sauti ikimwita upande wake wa kulia alipogeuka kuangalia aliwaona vijana wawili wamekaa kwenye viti pembeni mwa bwawa la kuogelea!
Mmoja wa vijana hao alikuwa Mwarabu na mwingine alikuwa Mweusi, alitembea na kuwasogelea hadi akawafikia walipokaa na kuwaamkia.
“Wewe kijana unaishi wapi?”
“Naishi Njiro!”
“Unaitwa nani?”
“Ninaitwa Nicholaus!”
“Aisee unaishi na nani nyumbani”
“Na dada zangu wawili!”
“Wanafanya kazi?”
“Hapana!”
Walimuuliza maswali mengi sana na kujifanya wamemwonea huruma sana walimwomba akae kitini wakamnunulia chakula! Katika maisha yake tangu wazazi wake wafariki hakuwahi kutegemea kula katika hoteli ya kifahari namna hiyo, alipomaliza kula alishukuru na wakampa noti ya shilingi elfu kumi kumsaidia nyumbani.
“Ahsante Mungu hii pesa yote nitamsaidia dada Leah kununua chakula cha mwezi mzima!” Alisema Nicholaus aliondoka akiwa ameahidi kukutana na watu hao kesho yake saa tatu asubuhi baada ya kuahidi kumsaidia zaidi.
Alipofika nyumbani aliwasimulia Leah na dada yake Vicky juu ya watu aliokutana nao hata wao walifurahi na walizidi kumshawishi siku iliyofuata arudi tena, usiku wa siku hiyo hakulala na siku iliyofuata asubuhi alidamka na kwenda hotelini.
Mapokezi mhudumu alipiga simu chumbani na wote Samwel na mwenzake waliteremka hadi chini na kumkuta Nicholaus akiwasubiri aliwasabahi na kuwaeleza hali ya nyumbani kwao.
“Dada zangu walifurahi sana kwa msaada wenu na wana hamu ya kuwaona!” Alisema Nicholaus bila kufahamu watu aliokuwa akiongea nao hawakuwa na mpango mzuri wa maisha yake.
“Ahsante lakini samahani kidogo hivi sasa tunatoka kwenda madukani, unaweza kurudi saa tisa na nusu jioni!”
“Sawa tu braza!” Nicholaus alimjibu Samwel
“Chukua pesa hii utaitumia kama nauli!” Samwel alimkabidhi Nicky shilingi elfu kumi.
Aliporudi saa tisa na nusu kama alivyoahidiana nao walimkaribisha chumbani ambako alipewa kikombe cha chai lakini alikataa kunywa akihofia kunywesha madawa ya kulevya.
“Labda kama kuna soda!”
Samwel alifungua friji na kutoa chupa ya soda na kumpatia Nicholaus akaanza kunywa alipomaliza maongezi yao yalianza.
“Kijana sisi ni Raia wa Iran! Tulikuja hapa nchini kutafuta biashara lakini kesho au kesho kutwa tutarudi nyumbani kwetu!”
“Kweli?”
“Ndiyo!”
“Sasa mbona mimi nimewazoea?”
“Unaweza kuongozana na sisi kama utapenda!”
“Kwenda Iran?”
“Ndiyo hakuna shida hata kidogo!”
“Kweli?”
“Ndiyo kwani huamini?”
“Nauli je?”
“Tutakusafarisha usiwe na shaka!”
“Oh! Ahsante Mungu, asante Mungu!” Nicholaus alipiga kelele akishangilia.
****
Alikwenda nyumbani na kuwasimulia Leah na Vicky walilia machozi! Vicky alilia zaidi akimbembeleza kaka yake asimwache lakini Nicholaus hakusikiliza.
“Sikiliza Vicky sitakusahau maishani nakwenda kutafuta maisha ili siku moja na sisi tuwe matajiri kama alivyokuwa baba yetu! Nataka nitajirike nijenge ghorofa katikati ya mji wa Arusha mimi na nyinyi tuishi pamoja kwa raha mustarehe” Alisema Nicholaus.
“Sio vizuri uondoke uniache mimi pacha wako tena nikiwa kipofu Nicholaus!” Alisema Vicky huku akilia.
“ Vicky unajua ninakupenda kiasi gani tafadhali niruhusu nikatafute maisha ili nije kukusaidia!” Aliendelea kumbembeleza Nicholaus.
Alimbembeleza dada yake hadi saa sita ya usiku ndipo Vicky alipokubali ombi hilo kwa shingo upande na hata Leah, ilibidi akubali wote watatu walikumbatiana na kusali pamoja wakilia, ilionekana kama hiyo ndiyo ilikuwa siku ya mwisho kuonana! Roho ilimuma sana Nicholaus kuona dada zake wakilia.
“Nyamazeni mimi nikirudi machozi yenu yote yatakauka dada zangu! Niombeeni tu kwa Mungu na mambo yakiwa safi mapema ninaweza kurudi kuja kuwachukua!”
“Sawa ahsante!” Aliitikia Victoria
Nicholaus aliingiza mkono mfukoni na kuchukua noti ya shilingi mia mbili akaichana katikati na kumkabidhi dada yake kipande kimoja.
“Victoria!” Aliita
“Naam!”
“Hicho ni nini?”
“Kipande cha karatasi!”
“Hicho ni kipande cha noti ya shilingi mia mbili je unaweza kununua kitu chochote na kipande hicho?”
“Hapana kaka yangu mpaka vipande vyote viwili!”
“Basi vivyo hivyo na mimi bila wewe ni kipande cha pesa siwezi kufanya lolote, nitakukumbuka sana Victoria na sipendi kutenganishwa na wewe ila imelazimu!” Alisema Nicholaus na wakakumbatiana wote huku wakilia machozi.
“Kitunze sana kipande hicho mpaka tutakapokutana tena usikitupe dada yangu huu ndio ukumbusho wangu kwako!”
“Sawa nitafanya hivyo Nicholaus!”
Wote walikuwa wakilia wakati Nicholaus akitoka ndani ya chumba chao tayari kwenda hotelini kwa safari, alipofika mbelealiangalia nyuma na kuwaona Leah na Vicky wamesimama mlangoni roho yake ikauma na kumfanya alie! Ulikuwa ni kama mwisho wa kuonana kwa upande mwingine wa moyo wake ulimwambia asiondoke lakini alipingana nao.
****
Alipofika hotelini alikuta AbdulAziz na Samwel wapo tayari, walimkabidhi karatasi zote za safari na kumkabidhi pia begi kubwa.
“Hilo begi lina nguo zako zote tumekununulia mdogo wetu, lakini kuna jambo moja la muhimu sana katika safari hii usitake watu wajue sisi na wewe tupo safari moja hutakiwi kutusemesha wala kutukaribia.
“Sawa tu ili mradi ninayo tiketi yangu tutakutana hukohuko Tehran wala msiwe na wasiwasi nawashukuru sana kwa msaada wenu!” Alisema Nicholaus bila kujua kuwa ndani ya begi lake kulikuwa na kitu ambacho kingeweza kuchukua uhai wake.�
****
Wote watatu Samwel, �Nicholaus na �AbdulAziz waliondoka hotelini wakiwa ndani ya gari aina ya benzi lililomilikiwa na hoteli ya Bin One lilikodishwa kwa wageni mbalimbali waliopanga ndani ya hoteli hiyo!
Nicholaus alivaa suti nyeusi pamoja na viatu vyeusi vilivyong’aa kwa hakika alipendeza! Ilikuwa ni mara ya kwanza kwake tangu wazazi wake wafariki kuvaa nguo za thamani kiasi kile! Kila mara alijiangalia ilikuwa ni kama ndoto.
Njia nzima Nicholaus alimfikiria dada yake na roho ilimuuma sana kumwachaVicky, ukizingatia dada yake alikuwa kipofu! Hakuwa na la kufanya ilikuwa ni lazima aondoke kwenda kutafuta maisha, hakutaka kuiachia bahati aliyoamini ameipata.
Ndani ya nafsi yake aliamini baada ya muda mfupi tu angerudi tena Tanzania akiwa tajiri na kujenga jumba kubwa pia kununua magari ya kifahari na maisha yangekuwa ya raha mustarehe baada ya hapo!
“Nyie mnakaa mjini Tehran kabisa au?”
“Ndiyo!”
“Lakini mimi nataka kwenda Marekani, nchi yenu ina vita sana na mimi sipendi vita, watu wanakufa mno, sitaki kufa bila kumwona tena dada yangu!”
“Haina shida ili mradi sisi tumeamua kukusaidia tukishafika Iran tutakutafutia tiketi nyingine ya ndege ili uondoke kwenda huko Marekani au ulitaka kwenda Uingereza na Canada?” Samweli alimuuliza.
“Hapana mimi nataka Marekani tu!”
“Basi hakuna shida!”
Muda wa kuripoti uwanja wa ndege kwa abiria wote ilikuwa saa sita mchana masaa mawili kabla ya ndege ya shirika la Gulf Air kuruka. Gari lao liliwasili uwanjani saa moja kabla ya muda wa kuruka kutimia, ilikuwa ni mara ya pili kwa Nicholaus kufika uwanja wa ndege wa Kilimanjaro!Mara ya mwisho ilikuwa miaka miwili kabla ya wazazi wake hawajafariki! Siku yeye na mama yake walipomsindikiza baba yao aliyekuwa akisafiri kwenda Ubeligiji kibiashara!
Uwanja wa ndege wa KIA ulimkumbusha mengi kuhusu wazazi wake na kumtia huzuni zaidi, aliwakumbuka baba na mama yake kwa kila kitu na aliamini kama wasingekufa asingekuwa safarini kwenda katika nchi asiyoifahamu siku hiyo.
“Baba na mama walikuwa na kila kitu lakini leo hii tunateseka, mali zote wanatumia baba mdogo na shangazi pamoja na watoto wao! Lakini hili ni kosa la baba sababu ya kutokuacha wosia mzuri nafikiri ni sababu ya kifo chake kilikuwa cha ghafla mno!” Aliwaza Nicholaus baada ya kuteremka katika gari.
“Nicholaus tangulia hukuelewa tulivyokueleza, hatutaki kuongozana na wewe au hutaki kwenda safari nini?”
“Nataka!”
“Haya basi tangulia!”
Huku akitabasamu na kuchukulia mkwara aliopigwa kama utani Nicholaus alianza kutembea taratibu kuelekea kwenye lango la kuingilia uwanjani tiketi yake ikiwa mkononi!
“Nicholaus!!!” Alisikia sauti ikimwita kabla hajaingia uwanjani �alipogeuka alishangaa kumwona Leah akiwa amemshika mkono Victoria! Badala ya kuingia alikimbia kuwafuata walipokuwa wamesimama na kuwakumbatia.
“Vipi mbona mpo hapa mmekuja na nini?”
“Tumekodisha teksi!”
“Kwanini mnatumia pesa vibaya hivyo si tulishaagana lakini?”
“Hapana Nicky mimi sitaki uondoke, moyo wangu umeshtuka nahisi kuna kitu kibaya kinakwenda kukupata na hautarudi tena! Nahisi wanakweda kukuua!” Alisema Victoria huku akilia mwili wake ulishahisi kitu kibaya.
Kwa dakika kama mbili Nicholaus hakujibu kitu chochote alikaa kimya akitafakari alichoambiwa, alipomwona dada yake akilia naye alianza kulia, Leah nae alishindwa kujizuia wote watatu walianza kulia na waliendelea kwa kama saa nzima!
Nicholaus alikuwa njia panda na alitakiwa kufanya uamuzi mgumu kupita maamuzi yote aliyowahi kufanya katika maisha yake, upande mmoja wa akili yake ulimweleza asiondoke lakini upande mwingine ulizidi kusisitiza aondoke kwenda kutafuta maisha bora kwa ajili yake, dada yake na Leah.
“Kaka usiondoke! Tafadhali nakuomba Nicholaus kama kufa na umasikini wetu acha tufe!” Aliendelea kusisitiza Vicky huku akisaidiwa na Leah!
“Abiria wote wanaosafiri kwa ndege ya shirika la ndege la Gulf Air mnaombwa kupanda ndani ya ndege kwani ndege itaruka baada ya dakika kumi na tano, ahsanteni!” Ilikuwa ni sauti nzuri nyororo iliyotoka katika kipaza sauti kilichokuwepo uwanjani hapo!
Mwili wa Nicholaus ulishituka kufuatia sauti hiyo na alipoangalia kwenye lango aliwaona Samweli na AbdulAziz wakimwita kwa ishara! Alitaka awaeleze kuwa asingeondoka tena lakini alishindwa kufanya hivyo.
“Vicky!” Alimwita dada yake.
“Naam kaka!”
“Siwezi!”
“Huwezi nini?”
“Siwezi kuacha kuondoka, niombee tu kwa Mungu tutaonana Mungu akipenda na nitaendelea kukupenda siku zote za maisha yangu!” Alisema Nicholaus na baada ya maneno hayo alinyanyua sanduku lake na kuanza kukimbia mbio kwenda ndani ya uwanja akiwaacha dada yake na Leah wakilia.
“Nicholaus usiondoke tafadhali rudi!” Alisema Vicky huku akilia machozi mwili wake ulishahisi kaka yake alikuwa akienda kufa!
*****
Kwa haraka na mbio alizokuwa nazo sanduku wa Nicholaus halikukaguliwa kabisa, aligonga tiketi yake mhuri na kukimbia mbio hadi ndani ya ndege bila kusimamishwa mahali popote na alikuwa mtu wa mwisho kuingia ndani ya ndege.
AbdulAziz na Samwel ambao hawakuwa na uhakika kama Nicholaus angekivuka kizingiti cha uwanja wa ndege wa Arusha walipomuona walinyanyuka vitini na kushangilia, Nicholaus alishangaa na hakuelewa ni kwanini walifurahi kiasi hicho alijikuta akiamini kuwa kweli walimpenda na waliamua kumsaidia!
Dakika kumi tu baada ya kukaa kitini na kufungiwa mkanda ndege ilianza kuiacha ardhi ya Tanzania! Akiwa juu aliingalia Arusha na roho ilimuuma sana, picha ya mwisho aliyoagana na dada yake pamoja na Leah uwanjani ilimuumiza kupita kiasi alishindwa kuelewa ni kwanini Vicky alisisitiza kuwa safari yake ingekuwa na matatizo.
“Wasichana bwana anataka tukae tu kuangaliana wakati umasikini unatutesa! Litakalokuwepo mbele acha liwepo Mungu anajua!” Alisema Nicholaus huku ndege ikiondoka.

Je, nini kitaendelea?
Tukutane Ijumaa hapahapa.

Comments are closed.