The House of Favourite Newspapers

Abdulkarim Karimjee: Spika wa Kwanza Mtanganyika

Abdulkarim Karimjee (kushoto) akiwa na afisa raia wa uimgereza

Na WALUSANGA NDAKI| RISASI JUMAMOSI| NAJUA UNAJUA

UKUMBI wa bunge uliokuwa unatumika jijini Dar es Salaam kabla ya kuhamia Dodoma unaitwa Karimjee Hall.  Kwa kifupi, majina hayo yanatokana na familia ya Karimjee ya Madhehebu ya Bohra, iliyoongozwa na Jivanjee Budhabhoy mwaka 1825, iliyotoka huko Cutch Mandvi, India na kuja Afrika Mashariki na hatimaye kuishi Zanzibar. 

Si hivyo tu, familia hiyo ndiyo iliyoutoa ukumbi huo utumike kuwa bungela Tanganyika. Ilikuwa ni familia ya wafanyabiashara iliyohamia baadaye Dar es Salaam, Tanganyika, ikapanua biashara zake nchini na nje ikiwa inajulikana kama Karimjee Jivanjee & Co Ltd ikijikita katika biashara za kilimo, viwanda na kadhalika.

Abdulkarim akiwa Bungeni

Ukumbi huo ulipewa jina la mjukuu wa Jivanjee aliyeitwa Abdulkarim Yusufali Alibhai Karimjee aliyekuwa spika wa kwanza Mtanganyika tangu Januari 1, 1956 hadi Desemba 26, 1962 wakati Tanganyika ilipokuwa imepata uhuru. Abdulkarim aliyezaliwa 1906 na kufariki 1977, pia alikuwa Naibu Meya wa Dar es Salaam mwaka 1952 na 1956 akawa meya kamili wa jiji hilo.

Wakati wa uhuru yeye ndiye aliyeendesha shughuli zote za bunge na akawa mbunge kamili wa kuchaguliwa badala ya mbunge wa kuteuliwa. Mwaka 1960 hadi 1970 alikuwa Naibu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo nchini (NDC) na Benki ya Biashara ya Taifa (NBC) na ndiye aliyeasisi Maktaba Kuu ya Taifa jijini Dar es Salaam.

Hiyo ndiyo familia ya Karimjee iliyokuwa maarufu si kwa biashara tu, bali kwa kutoa misaada mbalimbali ya kusaidia watu wengine, hususan maskini.  Ilikuwa pia familia iliyopendwa na Mwalimu Julius Nyerere kwa msimamo huo.

Comments are closed.