The House of Favourite Newspapers

Hadithi ya Shigongo: Dimbwi la Damu-14

Ilikuwa harufu mbaya  na kali 
mno, Leah na Manjit 
walishindwa kuelewa ilitokea sehemu gani ndani ya nyumba! Walijaribu kuita jina la Shabir lakini hakuna mtu aliyeitika, kwa sababu gari lilikuwa nje waliamini asilimia mia moja Shabir alikuwa ndani! Ilikuwa si kawaida yake kutoka nje ya ngome bila gari.

Ilibidi wabadili na kuanza kuita jina la bibi Sundra wakiamini alikuwemo ndani, hawakuelewa kuwa alishaachishwa kazi na Shabir muda mrefu ili apate  nafasi ya  kumbaka Victoria kwa urahisi, waliita jina la bibi Sundra kwa muda mrefu lakini bado hawakuitikiwa walishindwa kuelewa kulikuwa na nini ndani ya nyumba na harufu ilizidi kuwakera.

“Mama ni nini lakini?”

“Hata mimi sifahamu lakini hii harufu ni kama inatokea huko ndani!”

“Wapi chumbani kwenu?”

“Ndiyo!”

“Basi nenda kaangalie labda kuna panya amefia ndani!”

“Lakini tangu lini nyumba hii ina panya?”

“Hata mimi sijui, lakini  kaangalie tu mama!”

Leah aliondoka sebuleni na kuanza kutembea kwenda chumbani, kadri alivyokikaribia chumba chao cha kulala   ndivyo harufu ilivyozidi kuongezeka, mlango ulikuwa wazi aliusukuma na kuingia hadi ndani ambako harufu ilizidi kuongezeka kiasi cha kumfanya abane pua yake kwa vidole! Aliangaza huku na kule kuona kama kulikuwa na kitu kilichofia humo ndani lakini hakukiona, aliangalia uvunguni  chini ya meza na hata darini lakini hakukuwa na kitu chochote.

“Manjit!”

“Naam mama!”

“Mbona hakuna kitu?”

“Kweli?” Aliuliza Manjit akielekea chumbani, alipoingia naye harufu ilimshinda na kujikuta akibana pua yake.

“Sasa tufanye nini?”

“Mpigie kwanza baba simu  aje akupe pesa za malipo tupeleke hospitali, hii harufu tutakuja  kuishughulikia baadaye!”

“Sawa!” Aliitikia Leah kisha akakaa kitandani na kunyanyua simu iliyokuwa pembeni mwa kitanda chao, ulikuwa ni muda mrefu hajalala kwenye kitanda chake na alitamani kufanya hivyo lakini suala hilo lilikosa umuhimu kwa wakati huo kwani alihitaji pesa upesi ili akalipe hospitali na matibabu ya Victoria yaendelee.

Alinyanyua simu na kupiga namba za ofisini kwa Shabir kwanza akifikiri labda siku hiyo gari lake lilikuwa bovu aliamua kutumia teksi, simu haikupokelewa hata baada ya kuwa amepiga zaidi ya mara tano! Iliita tu kwa kipindi kirefu na kukatika.

“Sijui wamefunga sababu hakuna anayepokea!”

“Mama jaribu simu yake ya mkononi!”Manjit alimshauri mama yake na kweli Leah akaanza kupiga namba za simu ya mkononi ya Shabir, alishangaa ilipoanza kuita humohumo ndani ya chumba! Wote wawili walishangaa na kushindwa kuelewa ni wapi alikokuwa Shabir kwa wakati huo kwani kuwepo kwa simu yake ndani kulimaanisha hata yeye mwenyewe alikuwa ndani au hakuwa mbali na nyumbani.

“Labda amekwenda dukani tujaribu kumsubiri!” Leah alimwambia Manjit.

Walisubiri kwa karibu masaa mawili mpaka Manjit akaanza kusinzia  bila Shabir  kuonekana walijikuta wakianza kuingiwa na wasiwasi, ilikuwa si rahisi hata kidogo kwa mtu makini kama Shabir kuondoka nyumbani kwenda matembezini na kuacha nyumba ikiwa wazi, fikra za Leah zilianza kumfanya  ahisi Shabir alikuwa ametekwa na majambazi na si ajabu alikuwa ameuawa lakini jambo hilo hakudiri hata kidogo kumwambia mtoto wake Manjit.

“Mama nataka kukojoa!”

“Vua uingie chooni  ukojoe lakini tafadhali usichafue choo!”

“Sawa mama!” Manjit aliitikia  kisha kunyanyuka akielekea kwenye choo kilichokuwa ndani ya chumba hicho, alifungua mlango na kuanza kuingia ndani huku suruali yake ikiwa imefunguliwa zipu tayari kwa kukojoa, alisimama mbele ya shimo la choo na kuanza kuachia mkojo wake taratibu kabla hajamaliza alinyanyua uso wake kuangalia juu tena bila sababu yoyote ni huko ndiko macho yake yalipambana na mwili wa mtu aliyevimba ukining’inia kwenye ubao uliokuwa darini. Alipoviangalia viatu vya mtu  aliyekuwa akining’inia aligundua vilikuwa viatu ya baba yake.

“Mama! Mama! Mama! Njoo uone baba huyu hapa!” Alipiga kelele Manjit akikimbia kwenda nje ya choo.

“Niniiii?”

“Baba yupo chooni!”

“Chooni? Anafanya nini?”

“Ananing’inia darini!” Alijibu Manjit lakini maneno hayo kwa Leah yalimaanisha kitu kikubwa zaidi, bila kujiuliza mara mbili alijua Shabir alikuwa amejinyonga na si ajabu  harufu iliyosikika ilikuwa ni ya mwili wake ulioharibika, hakuwa mwongo wala hakuidanganya nafsi yake ni kweli mume wake Shabir alikuwa akining’inia darini mwili wake ukiwa umevimba kupita kiasi! Leah alianza kulia bila kujua kilichopelekea mume wake achukue uamuzi mbaya kiasi hicho.

“Kuna nini kilichotokea hapa?” Aliuliza Leah huku akilia, alimkumbatia mtoto wake na wote waliendelea kulia.

Dakika chache baadaye Leah aliona kipande cha karatasi kikiwa sakafuni, alikichukua na kuanza kukisoma! Ni hicho ndicho kilimpa angalau picha ya kichotokea ingawa haikuwa picha halisi, kiliandikwa:

Mke wangu Leah,

Nimechukua uamuzi huu kwa sababu kitendo nilichokifanya kisingekufurahisha, nimekukosea sana naomba unisamehe na pia niombee sana msamaha kwa Victoria kama atapona! Mwambie ni shetani aliyeniingia mpaka nikajikuta nikifanya mambo niliyomtendea, alikuwa mtoto mwema na mtiifu ambaye hakustahili hata kidogo unyama nilioufanya! Najuta kufanya kosa hilo, naomba umshughulikie mpaka apone! Mimi natangulia kuzimu na ninajua adhabu yangu itakuwa mbaya sana, acha nikutane nayo kwa sababu ninastahili.

Ni mimi mumeo

Marehemu Shabir.

Leah aliisoma barua hiyo mpaka mwisho, ndiyo ilimpa jibu kuwa Shabir hakunyongwa bali alijinyonga mwenyewe lakini haikumpa jibu la kwanini alijinyonga na ni kitu gani alimfanyia Victoria mpaka akaamua kuchukua uamuzi huo,  kwa mbali akilini mwake alihisi labda Shabir alimbaka Victoria mpaka kumpa ujauzito! Kichomfanya afikirie hivyo ni mazingira ya safari yake ya Bombay, ilikuwa ya ghafla mno na haikuwa na sababu ya kuwepo na Shabir kusisitiza Victoria abaki, kitu kingine kilichomfanya awaze hivyo ni  ugonjwa uliokuwa ukimsumbua Victoria, kuwa mimba iliharibika na kuozesha mfuko wake wa uzazi.

“Mimba aliitoa wapi Victoria kama sio kwa Shabir?” Aliwaza Leah huku akilia machozi.

Baadaye aliamua kupiga simu polisi kuwataarifu juu ya tukio lililotokea, dakika kama kumi baadaye polisi walifika wakiwa na magari yao na kugonga mlango wa nyumba, Leah alitoka na kwenda kuwafungulia. Waliingia moja kwa moja hadi ndani na Leah aliwapeleka hadi chumbani kwake na kuwafungulia mlango wa choo, walimwona Shabir akining’inia darini.

“Nyie mlikuwa wapi mpaka ameharibika kiasi hiki? Mlikuwa hamjagundua tu?”

“Tulikuwa safarini Bombay, tulirudi siku nane zilizopita na  kumkuta msichana tuliyemwacha hapa nyumbani na baba akiwa hoi  bin taaban, tena alikuwa hapo nje! Tukamchukua na kumpeleka hospitali ambako alilazwa na kugundulika alitoa mimba vibaya na mfuko wake wa uzazi ukaharibika, tumekaa hospitalini mpaka leo bila mume wangu kuja kutuona! Tuliporudi hapa ndipo tukakuta harufu hii mnayoisikia, tulianza kutafuta ni kitu gani kilikuwa kikinuka namna hiyo, mwanzoni tulifikiri ni  panya amekufa lakini baadaye   tukamkuta humu akining’ini….!” Leah alishindwa kumalizia na kuangua kilio, askari aliyekuwa jirani alimkumbatia na kuanza kumfariji.

“Kitu gani kingine mlikikuta?’

“Ni hii barua tu!”

“Hebu niione!” Aliuliza askari mmoja  mwenye nyota tatu begani.

Leah alimkabidhi askari yule barua na akaanza kuisoma hadi mwisho, alipomaliza alitikisa kichwa chake kisha akamuangalia Leah  kwa macho ya huruma usoni.

“Najua kilichotokea!”

“Ni nini?”

“Nitakueleza baadaye, hebu vijana teremsheni huo mwili!”Aliamuru mzee huyo na palepale maaskari walivaa glovusi mikononi na kuushusha mwili wa Shabir kutoka darini, waliubeba na kuupeleka moja kwa moja  hadi kwenye gari ambako waliupakia, Leah na Manjit walipanda gari jingine na safari ya kwenda kituo cha polisi ilianza, mwili wa Shabir ulipelekwa moja kwa moja hospitali ya Canadian Hospital ambako ulihifadhiwa chumba cha maiti.

Kituoni Leah alitoa maelezo yake na baadaye kuruhusiwa kurudi nyumbani ambako alishindwa kukaa na kuamua kuondoka kwenda hospitalini, alimkuta Victoria bado yupo katika maumivu makali! Alitamani sana kumuuliza juu ya kilichotokea lakini alishindwa, na alishindwa pia hata kumweleza juu ya kifo cha Shabir! Manjit alikuwepo pamoja nao, alikuwa bado akiendelea kumlilia baba yake mzazi Shabir! Hakuwahi  pamoja na umri wake mdogo  kuwaza kuwa siku moja mwisho wa baba yake ungekuwa huo.

Manjit na mama yake hawakulala mpaka asubuhi, mioyo yao ilikuwa bado iko katika majonzi makubwa, Leah alitamani sana kujua nini kilichotokea kati ya Victoria na  mumewe mpaka akaamua kujinyonga, moyo wake ulimwambia amuulize Victoria lakini upande mwingine alisita, aliona angeweza kumsababishia maumivu makali zaidi. Lakini asubuhi ya siku hiyo hali ya Victoria ilikuwa nzuri kidogo, dawa za Avelox alizoandikiwa zilionekana kumsadia kidogo.

“Dada Leah kwanini Manjit analia  tangu jana?” Victoria aliuliza.

“Hakuna kitu anakuhurumia tu!”

“Ahsante sana kwa kuja maana usingekuja kwa hakika ningekufa! Mambo aliyonifanyia baba ni mabaya mno na sikutegemea angeweza kunifanyia hivyo!”

“Mambo gani?” Ingawa Leah hakutaka kuuliza alijikuta swali hilo likimtoka mdomoni, badala ya Victoria kutoa jibu alibanwa na kwikwi na kuanza kulia, kitendo hicho kilisababisha nyuzi zilizoshonwa tumboni mwake zote zifumuke na utumbo kuanza kuonekana nje!

“Nesi! Nesi!” Leah aliita

“Nini! Nini dada?”

“Njoo uone utumbo unataka kutoka!”

Manesi wote waliokuwa ofisini walitimua mbio hadi kitandani alikolala Victoria, walishangazwa na hali waliyoikuta! Victoria alikuwa bado akilia kwa nguvu, walielewa hiyo ndiyo sababu iliyofanya nzuri zifumuke kwa sababu alilia kwa nguvu na kukaza misuli ya tumbo wakati kidonda kilikuwa bado hakijapona vizuri.

“Call the doctor immediately!”(Mwiteni daktari haraka!) Alisema muuguzi mmoja na simu ilipigwa ofisini kwa daktari Martin Cook, bingwa wa upasuaji wa hospitali ya Canadian Fellowship Consultant Hospital! Haikuchukua hata dakika mbili daktari akawa tayari ameshafika, alipoliona tumbo la Victoria lilivyokuwa wazi hakuwa na kingine cha kushauri zaidi ya Victoria kurudishwa chumba cha upasuaji.

“She needs secondary stiching!”(Anahitaji kushonwa kwa mara ya pili!)

Victoria alikimbizwa haraka chumba cha upasuaji na kumwacha Leah akilia na kujilaumu ni kwanini aliliuliza swali lake,chumba cha upasuaji Victoria alishonwa kwa mara ya pili, ilikuwa ni kazi ngumu kwa sababu kidonda kilishakaa muda mrefu, iliwachukua madaktari masaa mawili kuirekebisha hali hiyo walipomaliza alirudishwa wodini, safari hii haikuwa wodi ileile ya mwanzo alipelekwa katika wodi yenye uangalizi maalum (ICU) ambako hakuna ndugu hata mmoja aliyeruhusiwa kumwona mpaka  kidonda chake kilipopona vizuri siku kumi na saba baadaye! Katika siku hizo mazishi ya Shabir yalifanyika.

Siku ya ishirini aliruhusiwa kutoka hospitali kwenda nyumbani ambako alimsimulia Leah kila kitu kilichotokea wakati yeye na Manjit wakiwa Bombay, tangu mwanzo hadi mwisho wa habari hiyo Leah na Manjit walilia machozi walishindwa kuamini kama Shabir alikuwa mtu katili  kiasi hicho! Walimhurumia sana Victoria kwa yaliyomkuta, habari hiyo ilipunguza maumivu waliyokuwa nayo juu ya Shabir na kifo chake, hata Manjit alijikuta akisema “Kifo cha baba kilikuwa adhabu yake!”

“Nisamehe dada sikupenda kufanya hivyo, nisingeweza kukusaliti kwa sababu wewe ni kila kitu kwangu ila baba alinilazimisha, ni heri ningekuwa na macho ningeweza kupambana naye!” Alisema Victoria akiwa amepiga magoti na kumshika Leah miguuni.

“Hapana usifanye hivyo Victoria, nakupenda wewe ni kama mtoto wangu! Nimekulea tangu utoto wako, ninajua si kosa lako huna haja ya kuniomba msamaha, ninakupenda, nitakupenda siku zote za maisha yangu. Pole sana!”

“Ahsante dada!”

Huo ndio ukawa mwisho wa Shabir, kifo chake kilimaanisha mali zote alizozimiliki kubaki mikononi mwa Leah na Manjit mtoto wake, Manjit wakati huo alikuwa na umri wa miaka kumi na mbili tu hivyo hakuwa na uwezo wakuiendesha biashara ya baba yake, Leah angeweza kufanya hivyo lakini elimu yake ilikuwa ndogo na isitoshe kosa alilolifanya Shabir ni kutomwonyesha jinsi biashara yake ilivyofanyika.

Kiliitishwa kikao cha wafanyakazi wa vituo vyote vya mafuta walivyovimiliki katika nchi ya Canada, ni katika mkutano huo ndiko wahasibu  wataalam wa mahesabu wa kampuni walimshauri Leah aiweke mali yote chini ya uangalizi wa kampuni ya Wataalam wa miradi, hao ndio wangemsaidia kuiendesha biashara yake  mpaka Manjit afikishe umri wa miaka kumi na nane au ishirini, wakati huo atakuwa akisomeshwa katika shule za mahesabu na uchumi ili akija kukabidhiwa miradi ya baba yake asishindwe kuiendesha, lilikuwa ni wazo zuri lililoungwa mkono karibu na wajumbe wote wa mkutano na bila mvutano wowot lilipitishwa, kampuni ya MULTI LATERAL INVESTIMENT INC. Iliyomilikiwa na wataalam wa mahesabu  nchini Canada ilikabidhiwa shughuli zote za kampuni ya Shabir.

Chini ya usimamizi wa kampuni hiyo kazi zote ziliendeshwa vizuri, kiasi kwamba baada ya mwaka mmoja mkutano wa Bodi ulipokaa   faida kubwa ilikuwa imepatikana na  Bodi kulazimika  kuipa  MULTI LATERAL INVESTIMENT INC mamlaka ya kuendelea hiyo kwa miaka mingine kumi zaidi, kipindi ambacho Manjit angekuwa ametimiza umri wa miaka ishirini na mbili na angekuwa amemaliza elimu ya Chuo kikuu.

“Mwanangu nataka usome sana ili hii kazi isije kukushinda!”

“Usiwe na wasiwasi mama najitahidi kadri ya uwezo wangu na sitakuangusha!” Hiyo ndiyo ilikuwa ahadi ya Manjit kwa mama yake.

************************

Miaka kumi na mbili haikuwa mingi kama ilivyotegemewa na wengi  ghafla ilikatika na kampuni ya MULTI LATERAL INVESTIMENT INC ikakabidhi kazi kwa Manjit ambaye tayari alikuwa na umri wa miaka 22 akiwa na digrii ya uchumi kutoka chuo kikuu cha Ottawa! Kwa mwili wake ulivyokuwa mkubwa ilikuwa si rahisi  hata kidogo kuamini kuwa umri wake ulikuwa ni miaka 22, kama mtu angeulizwa ni lazima angetaja hata miaka 35  au zaidi, Manjit alionekana kuwa na umbile kubwa kuliko umri wake.

Wakati huo Victoria alikuwa na umri wa miaka 42! Alikuwa mama mzima, hakuwa na mtoto wala mchumba! Mambo yote aliyofanyiwa na marehemu Shabir alishayasahau lakini jambo moja alishindwa  kabisa kulitoa akilini mwake nalo ni kaka yake Nicholaus! Bado alimkumbuka Nicholaus kupita kiasi, kila siku iliyokwenda kwa Mungu ilikuwa ni lazima amfikirie, bado alikitunza kipande cha noti walichogawana miaka mingi kabla, ni hicho ndicho kilichomtia simanzi zaidi lakini aliamini iko siku angekutana na kaka yake. Leah aliishi naye vizuri na alimtunza kama mtoto wake.

“Ipo siku nitakutana na Nicholaus ninaamini yupo hai!”

 

 Je, nini kitaendelea?
Tukutane Jumatatu hapahapa.

Comments are closed.