The House of Favourite Newspapers

MPENZI WANGU SARAFINA-10

0

David alichanganyikiwa, hakuamini kile alichokiona, picha ya msichana Sarafina ikaja kichwani mwake, hakuamini kama kweli yule msichana aliyechoka, aliyekongoroka, asiyekuwa na mvuto wowote alikuwa Sarafina, yule msichana aliyekuwa akimsifia kila siku, mwenye umbo mtata.

Alinyamaza ndani ya gari, hakutaka kuzungumza kitu, alikuwa na mawazo tele. Mtoto aliyekuwa amemshika alifanana sana na yeye. Moyo wake ukamwambia kwamba mtoto yule alikuwa wake, ila swali muhimu alilojiuliza ni kuhusu mtoto yule, ile mimba hakutoa? Na kama hakutoa, ni kitu gani kilitokea mpaka kuiacha.

Wakati yeye akifikiria hayo, naye Gloria aliyekuwa pembeni yake alikuwa akifikiria yake. Kichwa chake kilichanganyikiwa, alikuwa akijiuliza maswali mengi kuhusu msichana yule, ombaomba aliyekuwa mtaani ambaye alimsaidia kiasi cha fedha.

Ilikuwaje amjue David? Kwa nini David alivyoitwa alishindwa kusema kitu chochote kile zaidi ya kubaki akimwangalia mwanamke yule kwa macho yaliyojaa mshangao mkubwa? Je, walikuwa wakijuana au? Kila alilojiuliza, alikosa jibu kabisa.

“David! Tell me something,” (David! Niambie kitu) alisema Gloria huku akimwangalia mwanaume huyo.

“What do wanna know?” (unataka kufahamu kuhusu nini?) aliuliza David.

“Who was she?” (yule mwanamke ni nani?) aliuliza Gloria.

“My classmate?”(mwanadarasa mwenzangu)

“So, why didn’t you stop the car and listen to her? Is there something wrong?” (Kwa hiyo, kwa nini hukusimamisha gari umsikilize? Kuna tatizo lolote?) aliuliza Gloria.

“Nothing!” (hakuna kitu)

Hakujua ni kitu gani alitakiwa kumwambia Gloria, jinsi alivyoonekana, msichana huyo alijaza maswali mengi kichwani mwake. Alijua fika kwamba kama angemwambia ukweli huo ndiyo ungekuwa mwisho wa yeye kuwa naye hivyo ilikuwa ni lazima ampange rafiki yake, Paschal kwa ajili ya kulitatua tatizo lile.

“Hebu subiri kwanza. Yaani yule Sarafina kanichanganya,” alisema David, hapohapo akachukua simu yake na kupiga upande wa pili.

Gloria alikuwa akisikiliza tu, alitaka kujua ukweli juu ya kile kilichokuwa kimetokea. Alimsikia David akizungumza na mwanaume kutoka upande wa pili, alikuwa Paschal ambaye pia alimfahamu kama rafiki yake mkubwa.

Akataka kuonana naye, hilo halikuwa tatizo na hata David alipokata simu, akamwambia kwamba walitakiwa kubadilisha safari na kwenda nyumbani kwa Paschal kwa ajili kuzungumza naye kuhusu yule msichana. Gloria hakukataa, alitamani kujua ukweli hivyo kwenda huko ambapo walitumia dakika thelathini, wakafika Kijitonyama Mabatini.

“Aisee nimekutana na Sarafina,” alisema David huku akimwangalia Paschal, yaani walitakiwa kuzungumza kikawaida na kwa sababu rafiki yake huyo alikuwa mzoefu wa kuunganisha stori, hakukuwa na tatizo lolote lile.

“Wacha weee! Sipati picha anavyoringa sasa hivi! Anafanya kazi wapi, kulekule uwanja wa ndege?” aliuliza Paschal.

“Daah! We acha tu! Yule demu amekuwa ombaomba mitaani!”
“Unasemaje? Sarafina huyuhuyu kawa ombaomba?”
“Ndiyo!”
“Pamoja na maringo yake yote yale? Pamoja na kukukataa kwa kukumwagia maji, leo kawa ombaomba?” aliuliza Paschal, alichokuwa akikizungumza ndicho alichokuwa akikitaka David.

“Ndiyo! Masikini weee! Sarafina amefikia hatua ile!” alisema David huku akiangalia chini, alijifanya kuumia sana.

“Duuh! Na Gloria kamuona?”
“Nimemuona. Kumbe mlisoma naye?”
“Ndiyo! Demu alikuwa ananata yule, anajua kuringa, alikuwa anapenda magari yule, mabosi ndiyo walikuwa wanamchukua tu!” alisema Paschal.

“Masikiniiiiii! Leo ndiyo amekuwa ombaomba!”
“Ni Mungu! Nadhani anamlipa kwa kile alichokifanya. Alijua kututukana wanaume,” alisema Paschal.

Kwa jinsi walivyokuwa wakizungumza, ilikuwa ni vigumu kugundua kwamba kile alichokuwa akiambiwa Gloria kilikuwa ni uongo. Watu hao hawakupangana, hawakuzungumza kwa siri, kila kitu walichokuwa wakikizungumza kiliaminika kichwani mwa msichana Gloria na kuamini kwamba kweli Sarafina alikuwa msichana mbaya ambaye alikuwa na maringo mno.

Walipomaliza, wakaondoka, moyo wa David ukatulia, kidogo tabasamu likaanza kuonekana usoni mwake japokuwa bado alikuwa akijiuliza kuhusu Sarafina.

Maisha yaliendelea, mapenzi yaliendelea kwenda mbele, kila mmoja alimuonyeshea mwenzake jinsi alivyokuwa akimpenda. Sarafina hakutoka kichwani mwa David, moyo wake ulimuuma sana kwani alijua fika kwamba mtoto aliyekuwa na Sarafina alikuwa mtoto wake, alimuacha akiteseka mitaani na yeye akila raha na mwanamke mwingine kabisa.

“Ila sawa. Sina kosa, nilimwambia akatoe mimba, nikampa hela, kama hakutoa, hilo janga lake, mimi nilinawa mikono yangu! Sina hatia, naamini hata Mungu atanielewa,” alisema David huku akijaribu kuyatoa majonzi moyoni mwake, hakika akafanikiwa, moyo wake ukapoa, kaubaridi kakaingia, mawazo juu ya Sarafina na mtoto Malaika yakaanza kutoka, kwa kifupi ni kwamba alianza kurudi katika hali yake ya kawaida.

 

Je, nini kitaendelea?

Tukutane kesho.

Leave A Reply