The House of Favourite Newspapers

Kessy: Nimefuata Makombe Yanga

0
Aliyekuwa beki wa Simba, Hassan Kessy.

 MUSA MATEJA NA SAID ALLY | CHAMPIONI IJUMAA | MAKALA

NI mwaka mmoja na siku 10 zimekatika tangu aliyekuwa beki wa Simba, Hassan Kessy alipoachana na timu hiyo na kutua kwa wapinzani wao wakubwa, Yanga.

Baada ya kukaa kwa siku hizo zenye milima, mabonde na tambarare, hatimaye beki huyo amefanikiwa kutwaa ubingwa wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara akiwa na kikosi hicho ambapo ubingwa huo unakuwa watatu mfululizo kuutwaa timu hiyo.

Yanga ina pointi 68 na ina wastani mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa dhidi ya Simba ambayo ndiyo inayowafuatia katika msimamo wa ligi kuu, timu zote zimesaliwa na mchezo mmoja, hata kama Yanga itapoteza mchezo wa mwisho, Simba italazimika kushinda idadi kubwa ya mabao ili iwe bingwa jambo ambalo ni gumu kimahesabu japo linawezekana.

Championi Ijumaa, limefanya mahojiano maalum na beki huyo juu ya maisha yake ya Yanga na hapa anafunguka kama ifuatavyo.

Ubingwa una maana gani kwako?

“Hiki ni kitu kizuri kwangu hasa kwa wale ambao walinidharau mwanzo kwa kusema ana nini aende tu, lakini sasa nimefika hapa na kutwaa ubingwa, pia ni furaha kwangu kwa mara ya kwanza nachukua ubingwa wa ligi kuu lakini kwa timu yangu kuchukua ubingwa tena.

Simba walikusema wakati unaondoka, ulilichukuliaje hilo?

“Ilikuwa ni changamoto kwangu kwa sababu sikumaliza vizuri nikiwa na wao hata hivyo sikuwa najali sana kile wanachokisema badala yake nilijikita zaidi kwenye timu yangu mpya kuona nini ambacho nitakifanya ili niwe bora zaidi.

Wakati wa mzozo na Simba, familia walilipokeaje hilo?

“Familia yangu ilikuwa inaumia kuhusu suala hilo kwa sababu kwanza watu wajue wazazi wangu ni mashabiki wa Simba, sasa wakati ule mvutano na timu hiyo waliweka kila kitu pembeni na kunipambania.

“Wao walikuwa wanaumia kusikia maneno mabaya niliyokuwa naambiwa kipindi hicho na waliniambia maisha kokote kama umetoka Simba na kutua Yanga wewe pambana na usife moyo.

Uliwahi kuwa shabiki wa Simba, Yanga kabla ya kuzichezea?

“Hapana mimi sikuwa mshabiki wa timu hizo, awali nilikuwa Mtibwa Sugar ambayo nilikuwa naichezea lakini baada ya kuhama sasa nashabikia timu ambayo naichezea ambayo ni Yanga.

Ulipokosa namba ulijisikiaje?

“Moyoni nilikuwa naamini kwamba mpambanaji hachoki na siku akichoka ujue kwamba kashapata, licha ya kutocheza lakini nilijipa moyo lazima nitacheza, na nashukuru baada ya kupewa nafasi ya kucheza nimeonyesha na kila mmoja ameona uwezo wangu, sasa imani yao ni kubwa juu yangu.

Unamzungumziaje kocha wako George Lwandamina?

“Ni kocha mzuri kabisa, yeye pamoja na benchi la ufundi kwa pamoja wanajua nini ambacho wanakifanya, kwangu naona kuwa ni ‘best coach’.

“Kote nilipocheza soka kulikuwa na makocha wazuri lakini Lwandamina amenifanya niwe na kiwango kizuri wakati ambao mambo yalikuwa yananiendea ovyo kutokana na kutopata namba kabisa ndani ya kikosi cha kwanza.

Ubingwa unautoa zawadi kwa nani?

“Kikubwa naupeleka kwa watu walionisapoti katika kipindi kigumu hasa familia yangu ambayo iliniambia nitulie kwenye masuala yote yaliyokuwa yakinitokea huko nyuma tangu naondoka Simba na kutua Yanga.

Nani walikupa upinzani msimu huu?

“Ni Simba, hakuna mwingine zaidi ya hao maana nilitoka kwao msimu mmoja nyuma ambao nilikuwa nawatumikia, yaani kila Yanga ilipokuwa inafungwa basi maneno yanaongezeka tena tulipofungwa nao, maneno yalizidi, nilikuwa naumia kuona hali hiyo.

“Nilijua kuwa endapo kama wakichukua ubingwa maneno hayo yatazidi lakini nashukuru kwa sasa tumechukua ubingwa mambo yataenda vizuri.

Unazungumziaje upinzani mbele ya MC Alger?

“Ilikuwa mechi kubwa kwa sababu kocha aliniambia nakuamini kucheza mechi hii, hivyo na mimi nikajiamini na kucheza mpira, japo sikuwa na uzoefu lakini nilikuwa natamani nicheze kila mara kwa ajili ya kupata uzoefu.

Una neno gani kwa mashabiki?

“Kwa watu wote nawaambia kwamba wasiwe wana kashifu mtu kwani hawajui ni nini mtu kaandikiwa na Mungu maana unaweza kukuta mtu keshapangiwa ukitoka hapa utaenda pale na utapata hiki.

“Watizame mifano kama ya Samir Nasri na Cesc Fabregas walitoka Arsenal kwa kukosa ubingwa na walienda kuuchukua kwenye timu nyingine tofauti, mimi nilitoka Simba na kutua Yanga na kutwaa ubingwa jambo ambalo najivunia kwa sasa.”

Leave A Reply