The House of Favourite Newspapers

MPENZI WANGU SARAFINA-20

0

Richard alishindwa kuubadilisha ukweli, ukabaki palepale kwamba mtoto wake alikuwa amefariki alipokuwa akizaliwa. Alilia sana, alimwangalia mke wake pale kitandani alipokuwa, moyo wake ulimuuma na kuna wakati alimlaumu Mungu kwa kumsababishia maumivu makali kiasi hicho.

Alisimama mbele ya kitanda alicholalia mke wake, alimwangalia huku moyo wake ukiwa kwenye maumivu makali. Alikumbuka namna Bianca alivyokuwa na hamu ya kumuona mtoto wake, alikumbuka jinsi mwanamke huyo alivyokuwa makini katika kuitunza mimba yake, hakujua ni kitu gani kingetokea baada ya kufumbua macho na kugundua kwamba mtoto wake alikuwa amefariki dunia.

Machozi yalimbubujika, alikuwa kwenye kipindi kigumu, kilichojaa maumivu makali kuliko vipindi vyote. Alisimama palepale, hakutaka kuondoka, alimwangalia mke wake machoni mwake, hakuona kama kungekuwa na mtu ambaye alikuwa na uwezo wa kumpa faraja zaidi ya mtoto wake ambaye alikufariki katika kipindi alichokuwa akizaliwa.

Baada ya saa moja, wazazi wa pande zote wakafika hospitalini hapo. Walipomuona Richard kila mmoja alimuonea huruma, alikuwa mnyonge, mwenye mawazo na hata walipoyaangalia macho yake waligundua kabisa kwamba mwanaume huyo alikuwa na maumivu makali moyoni mwake.

“Pole sana Richard,” alisema baba yake huku akimpigapiga mgongoni.

“Nashukuru sana! Naamini kila kitu kinachotokea kipo katika makusudi yake,” alisema Richard huku akikiinamisha kichwa chake.

Baada ya saa nne kupita ndipo Bianca akafumbua macho kitandani pale. Mtu wa kwanza kabisa kumuona alikuwa mume wake na swali la kwanza kuuliza lilikuwa ni juu ya mtoto wake.

Alitaka kumuona, alikumbuka kwamba kabla ya kupoteza fahamu alikuwa katika chumba cha uzazi kwa ajili ya kujifungua na hata alipoyafumbua macho yake, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kutaka kumuona mtoto wake huyo.

Aliangalia huku na kule, hakukuwa na mtoto, aliwaona wazazi wake na mume wake huyo ambaye uso wake ulikuwa kwenye majonzi tele. Akahisi kulikuwa na kitu kimetokea kwani ilikuwa ni vigumu watu hao kuwa kwenye nyuso hizo na wakati alikuwa amejifungua.

“Mtoto wangu yupo wapi?’ aliuliza Bianca huku akimwangalia mume wake.

“Mke wangu! Subiri kwanza! Unaendeleaje?’ aliuliza Richard huku akimwangalia Bianca.

“Niambie kwanza mtoto wangu yupo wapi!”
“Bianca! Pumzika kwanza!”

Moyo wa Richard ukauma zaidi. Bianca hakutaka kunyamaza, alitaka kusikia mahali alipokuwa mtoto wake. Hakujua kama alikuwa amefariki, alichokijua ni kwamba alijifungua salama na mtoto huyo kuhifadhiwa mahali fulani.

Richard alijitahidi kumtuliza mkewe kitandani pale lakini moyo wake ulikuwa ukiuma mno. Alijizuia kwa nguvu zote asionyeshe majonzi yoyote yale au hata kumwaga machozi kwa mkewe lakini kikafika kipindi akashindwa kabisa kwani kwa jinsi Bianca alivyokuwa akimuulizia mtoto na moyo wake kujua kwamba alifariki ila hakutaka kumwambia ukweli,

Bianca alielewa kilichokuwa kikiendelea, kitendo cha mume wake kunyamaza kumwambia kilichokuwa kimetokea ilimaanisha kwamba mtoto wake alikuwa amefariki dunia kitu kilichomuuma mno.

Akaanza kulia kwa sauti huku akimtaja mtoto wake. Richard aliyekuwa mbele yake akashindwa kuvumilia, haraka sana akatoka na kwenda ukutani ambapo huko akaanza kulia kwa uchungu mkubwa.

Moyo wake ulimuuma zaidi, alijitahidi mno kumficha mkewe lakini hakufanikiwa na mwisho wa siku kugundua kwamba mtoto wake mpendwa alikuwa amefariuki dunia.

Huo ndiyo ulikuwa ukweli. Mioyo yao iliumia mno, mpaka siku ambayo Bianca aliporuhusiwa kurudi nyumbani, alionekana mnyonge kupita kawaida na muda mwingi alikuwa akilia kwa kilio cha kwikwi.

Richard hakutaka kwenda kazini, kwa siku hizo akaamua kukaa nyumbani kuomboleza kwani kama kuumia, aliumia mno na mbaya zaidi, mkewe ambaye ndiye alikuwa faraja yake pekee naye pia akawa ameumia.

Siku zikakatika, wakaendelea kukaa kwenye majonzi mazito. Baada ya mwezi mmoja kupita, wakakubaliana kukubaliana na hali iliyotokea kwamba kama mtoto wao kufariki, alifariki na hivyo walitakiwa kufanya mambo yao kama kawaida.

Walichokifanya ni kuendelea na maisha ya kawaida huku wakimuomba Mungu awape mtoto mwingine. Kila mmoja alionekana kuwa siriazi kwa kipindi hicho, katika siku zote za hatari za kushika mimba ndizo ambazo walikuwa wakifanya mapenzi kwa nguvu zote.

Walichokuwa wakikihitaji kilikuwa ni mtoto. Mungu aliwapa kila kitu maishani mwao, ili furaha yako ikamilike ilikuwa ni lazima kupata mtoto. Walijitahidi kupita kawaida lakini matokeo yakawa bila kwa bila.

Hawakujua tatizo lilikuwa nini. Miezi sita ya majaribio ikapita lakini Bianca hakushika mimba. Wakawa na hofu, wakahisi kwamba kulikuwa na kitu kilichokuwa kimetokea, wakati mwingine Richard alihisi kwamba mke wake alishindwa kuzihesabu siku zake za kuingia kwa mwezi hivyo kuanza kuhesabu kwa pamoja.

Walifuata kalenda lakini bado Bianca hakujisikia hakuchafuka na mbaya zaidi hata kujisikia kichefuchefu hakujisikia. Hawakukata tamaa, waliendelea zaidi, mwaka ukakatika, hali ilikuwa hivyohivyo, Bianca hakuwa amepata mimba kitu kilichowafanya kwenda hospitalini.

“Kwa muda gani?” aliuliza daktari.

“Mwaka mzima! Hakuna kitu,” alijibu Richard huku akionekana kukata tamaa, muda wote huo Bianca alikuwa kimya, hakuwa na la kuongea, kama kumuomba Mungu, alimuomba sana lakini hakukuwa na kitu chochote kile.

“Itabidi tumfanyie uchunguzi mke wako,” alisema daktari kitu ambacho kwa Richard hakukuwa na tatizo lolote lile.

Hilo ndilo walilolifanya madaktari hao, wakampima Bianca na kugundua kwamba alikuwa na tatizo kubwa katika mfumo wake wa uzazi. Ukuta wake wa uterasi ulikuwa umechanika hivyo kuwa vigumu kwa kushika mimba.

“Unasemaje?” aliuliza Richard huku akionekana kushtuka.

“Kwa hapa! Ni vigumu sana kushika mimba. Kama unasema mimba yake iliharibika, basi tatizo lilianzia hapo,” alisema daktari huku akimwangalia Richard.

Wote wakabaki kimya, wakainamisha vichwa vyao chini, maneno aliyozungumza daktari huyo yaliwaumiza kupita kawaida. Hawakuamini kama huo ndiyo ungekuwa mwisho wa mwanamke huyo kushika mimba.

“Inamaana hatoweza kushika mimba?” aliuliza Richard huku akishtuka.

“Ndiyo! Ila kama atafuata maelekezo ya kidaktari basi atashika baada ya miaka mitatu,” alijibu daktari huyo, jibu lililowafanya wote kunyong’onyea kwani hawakutegemea kusikia kitu kama hicho!

“Miaka mitatu au miezi mitatu?” aliuliza Bianca huku akimwangalia daktari huyo.

“Miaka mitatu! Siku 1095,” alijibu daktari huyo kitu kilichomfanya Bianca kuanza kuangua kilio mahali hapo.

 

Je, nini kitaendelea?
Tukutane Jumatano.

Leave A Reply