The House of Favourite Newspapers

MPENZI WANGU SARAFINA-21

0

Mawingu mazito yakaanza kujikusanya katika anga lote la Dar es Salaam, watu wote waliokuwa njiani kuelekea majumbani mwao wakaanza kufanya haraka kwani dalili zilionyesha kwamba mvua kubwa ingenyesha muda mfupi ujao.

Wale waliokuwa ndani kwa lengo la kutoka, wakavaa makoti yao huku wengine wakichukua miamvuli kwani hali iliyokuwa ikionekana ilimtia hofu kila mmoja na kuhisi kwamba mvua kubwa ambayo haikuwahi kutokea kwa mwaka huo ingeweza kunyesha dakika chache tu zijazo.

Kwa watu waliokuwa wakiishi mabondeni hawakuwa na amani. Waliichukia mvua, kila ilipokuwa ikinyesha, walikuwa wakiweka ndoo katika sehemu ambazo zilipitisha maji huku wengine wakichukua vifaa vya umeme na kuviweka juu ya kitanda kwa kuhofia mafuriko.

Wakati huohuo Malaika alikuwa ndani ya chumba alichokuwa akiishi na Ibrahim. Alikuwa na hofu kubwa, alikuwa na ugonjwa wa Sickle Cell, kila baridi lilipokuwa likipiga alikuwa akihisi maumivu makali katika mifupa yake kitu kilichomnyima raha kabisa na kuhisi kwamba muda wowote ule angeweza kufariki dunia.

Alijikunyata kitandani, alikosa amani, dalili za mvua kubwa iliyotaka kunyesha ikamfanya kukosa raha kabisa. Nyumba ilikuwa sehemu nzuri na waliishi hapo kwa miaka nane lakini bado moyo wake ulikuwa na hofu kubwa.

Moyo wa Ibrahim ulikuwa kwenye maumivu makali, alimfahamu Malaika, alikuwa msichana aliyekuwa kwenye mateso makali hasa katika kipindi cha baridi. Aliumia kila alipokuwa akimuona akilia, wakati mwingine alimlaumu Mungu, kama alikuwa na uwezo wa kufanya uponyaji, kwa nini hakumponya Malaika ili naye awe mzima kama watu wengine?

“Malaika mpenzi!” alimuita mpenzi wake.

“Abee!”

“Ngoja nikuletee shuka jingine!” alisema Ibrahim, akafungua kabati na kutoa shuka moja na kumfunika Malaika kitandani pale.

Msichana huyo akajikunyata, Ibrahim alikuwa pembeni kwenye kiti, hakutoka nje, alibaki akimwangalia mpenzi wake namna alivyojikunyata kitandani pale. Wakati akisikia maumivu makali moyoni mwake kwa kile kilichokuwa kikiendelea, mvua hiyo kubwa ikaanza kunyesha.

Hali ya hewa ikabadilika ghafla, joto likamezwa na baridi kali kuanza kupiga. Ingawa Smalaika alijifunika shuka kitandani pale lakini yalishindwa kuzuia baridi kumpiga na kumsababishia maumivu katika mifupa yake.

Akaanza kulia kama mtoto, alisikia maumivu makali mno, maimivu ambayo alikuwa akiyasikia kila siku alipokuwa akihisi baridi kali au ugonjwa huo ulipokuwa ukimkumba ghafla.

Ibrahim akasimama kutoka pale kitini na kumfuata Malaika kitandani pale, alipomfikia, akavua nguo zake na kisha kumfunika msichana huyo. Kwa jinsi alivyokuwa akilalamikia maumivu makali moyo wake ulimuuma, siku zote alitamani kumuona msichana huyo akipona na kuwa mzima kabisa lakini kila alipomuomba Mungu kwa ajili ya kufanya muujiza huo, ilishindikana kabisa.

“Nakufa Ibrahim!” alisema Malaika huku akilia kwa maumivu makali.

“Huwezi kufa! Huwezi kufa mpenzi!” alisema Ibrahim huku akimlalia juu yake kwenye zile nguo kama njia mojawapo ya kumpa joto.

Hakuacha kulia, kadiri muda ulivyokuwa ukizidi kwenda mbele ndivyo ambavyo alihisi maumivu makali. Ibrahim aliogopa, siku hiyo hali ilionekana kuwa tofauti kabisa, msichana huyo alikuwa kwenye maumivu makali kuliko siku nyingine.

Nje kulikuwa na mvua lakini hakutaka kukubali, ilikuwa ni lazima kumtoa msichana huyo na kumpeleka hospitalini. Akamnyanyua kitandani pale, akatoka nje, Malaika aliendelea kulia, kwa jinsi baridi lilivyokuwa likimpiga ndivyo alivyozidi kulia zaidi.

Wakatafuta Bajaj na kumpandisha. Kila neno aliloongea Malaika mahali hapo, alisema kwamba alikuwa akifariki dunia kwani maumivu aliyokuwa nayo kipindi hicho yalikuwa makubwa kiasi kwamba asingeweza kuvumilia hata mara moja.

Bajaj haikuchukua muda mrefu ikafika katika Hospitali ya Mwananyamala na kuanza kutibiwa. Alikuwa kwenye hali mbaya, tatizo alilokuwa nalo lisingeweza kutibika mahali hapo, akatakiwa kuhamishwa na kupelekwa katika Hospitali kubwa ya Moscow Medical iliyokuwa Posta jijini Dar Es Salaam.

“Kwa nini Moscow?” aliuliza Ibrahim.

“Kwa huu ugonjwa ulipofikia, apelekwe huko! Sisi hatuna dawa za kumpa,” alisema daktari huku akimwangalia Ibrahim.

“Ila ile hospitali ni gharama kubwa! Tutaweza kuzimudu?” aliuliza Ibrahim.

“Nyie nendeni huko tu! Lolote litakalotokea sawa tu! Sidhani kama watakataa kumtibu mtu mwenye hali mbaya kama huyu,” alisema daktari.

Hawakuwa na jinsi, Ibrahim akamchukua Malaika wake na kuondoka hospitalini hapo. Japokuwa hakukuwa mbali lakini kwa Malaika ilikuwa ni sawa na kutoka Dar mpaka Arusha, aliona kama wanachelewa kufika kwani maumivu aliyokuwa akiyasikia katika mifupa yake hayakuweza kuelezeka.

“Mungu! Kwa nini usiniue! Niue tu nikapumzike! Niue tu kama ulivyomuua mama yako kuliko kunitesa hivi,” alisema Malaika huku akiwa ndani ya Bajaj kuelekea hospitalini.

Hawakuchukua muda mrefu wakafika hospitalini hapo ambapo moja kwa moja Malaika akapeleka katika chumba cha matibabu na kuanza kutibiwa. Muda wote Ibrahim alikuwa nje ya chumba kile, kichwa chake kilikuwa na mawazo mno. Pale alipokuwa alishindwa kuendelea kukaa kwani muda wote alikuwa akisikia sauti ya kilio kutoka kwa Malaika aliyekuwa ndani ya chumba kile.

Akasimama na kuondoka kwani alizidi kuumia na kuhisi kwamba huo ndiyo ungekuwa mwisho wa msichana wake ambaye kila siku kwake alikuwa ni wa thamani kuliko mtu yeyote yule.

Akatoka nje ya hospitali hiyo, akakaa sehemu na kujiinamia, machozi yalikuwa yakimtoka kama mtoto mdogo, pale alipokaa peke yake, akaanza kusikia vishindo vya mtu akija kule alipokuwa.

Akayainua macho yake, akamuona dada mmoja, nesi akitembea kwa mwendo wa harakahara kuelekea sehemu huku akiwa amebeba mtoto. Hakujua nini kilitokea lakini kwa jinsi nesi yule alivyoonekana, alikuwa na hofu, hakujiamini na hata alipokutanisha naye macho, hakuonekana kuwa sawa.

Hakutaka kupuuzia, alipopita, naye akasimama na kuelekea kule alipokwenda nesi yule kwa mwendo wa kunyata. Alitaka kujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea mahali hapo.

Akamuona nesi yule akisogea mpaka sehemu fulani iliyokuwa na pipa safi na zuri kisha kumuweka mtoto yule kwa juu huku akiwa amemfunika vizuri. Hapohapo nesi yule akahukua simu, akapiga sehemu na kuanza kuongea na mtu fulani.

“Huku nyuma…ndiyo…kwenye pipa…sawa….usisahau kuniwekea kwenye akaunti ya simu ya namba hii…sawa…tupo wanne…haina shida,” alisema maneno hayo na kisha kukata simu, harakaharaka akaondoka na kumuacha mtoto yule.

Huku akiwa na maswali mengi, akaliona gari moja la kifahari likisimama umbali kama wa mita hamsini, mwanaume mmoja akateremka na kuanza kuelekea kule alipokuwa.

Akagundua kilichokuwa kikiendelea, ilionyesha kwamba mtoto alikuwa ameibwa ndani ya hospitali hiyo na mwanamke huyo ndiyo alikuwa akija kumchukua.

Kwa haraka sana akasimama na kuelekea kule kulipokuwa na mtoto yule, hakutaka kujiuliza maswali, akamchukua na kuanza kukimbia naye kwa machale pasipo kuonekana. Akapita salama getini, tena akisalimiana na walinzi kisha kutokomea zake.

****

Hicho kilikuwa kipindi cha huzuni kuliko vyote. Richard na mke wake walibaki wakimwangalia daktari, hawakuamini kile walichoambiwa kwamba walitakiwa kusubiri kwa mwaka mzima ndipo Bianca angepata mimba na kujifungua salama.

Wakaondoka hospitalini hapo wakiwa na huzuni tele, hawakuwa na jinsi, hawakupingana na daktari huyo, kama walivyoambiwa ndivyo walivyotakiw akufanya na hivyo kusubiri.

Siku ziliendelea kukatika, hakukuwa na mtu aliyekuwa na furaha ndani ya nyumba, kila mmoja alionekana kuwa mnyonge, tena katika kipindi kama hicho ambapo ukuta wa kizazi chake ulikuwa umechanika, Richard hakutakiwa kuingiza mbegu ndani ya Bianca kwa kuepuka kumsababisha matatizo makubwa, hivyoo alitakiwa kusubiri.

Siku zilikatika, miezi ikakatika na hatimaye mwaka kukatika. Wakarudi tena kwa daktari yuleyule wa magonjwa ya kinamama na kuzungumza naye, akampima Bianca, ule ukuta wa kizazi uliokuwa umechanika ukarudi katika hali yake ya kawaida na kuambiwa kwamba sasa walitakiwa kutafuta mtoto.

Hiyo ndiyo kazi iliyobaki. Wakajituma usiku na mchana, wala hawakuchukua wiki nyingi, Bianca akaanza kukosa siku zake za mwezi, akampa taarifa mumewe na walipokwenda kupima, akaonekana kuwa mjauzito.

Hicho ndicho walichokuwa wakikihitaji kwa kipindi kirefu, Richard akaanza matunzo mapya, akajitoa mara tatu ya vile alivyojitoa kipindi cha nyuma. Muda huo kila mmoja alikuwa makini, hawakutaka kuona wakimpoteza mtoto kama ilivyokuwa kipindi cha nyuma.

Walitaka kujua jinsi mapema kabisa, baada ya miezi kadhaa wakaenda kupima na kipimo cha Ultra Sound na kuambiwa kwamba Bianca alikuwa na watoto mapacha wa kiume kitu kilichomfanya kila mtu kuwa na furaha.

“Mapacha?” aliuliza Richard.

“Ndiyo! “ alijibu daktari.

“Mungu wangu! Siamini! Mke wangu una watoto mapacha! Mke wangu una watoto mapacha!” alisema Richard, machozi yakaanza kumtoka kwa furaha, alirukaruka kama kichaa, kila alipomwangalia mkewe, alisikia furaha kubwa ambayo hakuwahi kuipata kabla.

Wakaondoka na kurudi nyumbani, waliendelea kufurahia, wakafanya shopping, tena mjini Dubai! Walizunguka sehemu nyingi, mpaka nchini Ufaransa kwa ajili ya kuwanunulia vitu watoto wao.

Bianca alipofikisha miezi nane akapelekwa katika Hospitali ya Moscow Medical Center kwa ajili ya kusubiri hukohuko kwa mwezi mzima, hata akishika uchungu, aushike akiwa hukohuko na si kuanza kukimbizana.

Kila siku Richard akawa na kazi ya kwenda hospitalini hapo kumjulia hali mke wake, alifurahi kila alipokuwa akimwangalia. Aliporudi nyumbani, mawazo yake yalikuwa kwa mkewe lakini zaidi yalikuwa kwa watoto wake mapacha ambao hakuwaona ila aliwasubiri kwa hamu.

“Umezungumza nao?” alisikika daktari mmoja akiuliza.

“Ndiyo! Wamesema wanatoa milioni kumi!”
“Haina shida. Wapange kabisa na walinzi ili mwanaume huyo akitoka na mtoto asiulizwe maswali yoyote yale,” alisema daktari.

“Sawa haina shida!”

Nesi akafanya kama alivyoambiwa, ilikuwa ni lazima waibe mtoto na kumpa bilionea mmoja aliyetafuta mtoto katika maisha yake bila mafanikio. Walinzi wakapangwa na kuahidiwa kupewa pesa, hakukuwa na tatizo lolote lile, na mtoto aliyetakiwa kuibwa alikuwa mmoja kati ya wale wawili ambao alitakiwa kujifungua Bianca.

Mchezo ukaenda kama ulivyotakiwa, Bianca akajifungua huku akiwa hoi, na bila kupima mara ya kwanza asingeweza kujua kama alijifungua mapacha. Akalala kitandani hoi, nesi mmoja akamchukua mtoto mmoja, akatoka naye mlango wa nyuma wakati Bianca akiwa hoi, akaenda naye mpaka nje, pale alipomuweka kwa ajili ya mwanaume mmoja kuja kumchukua, akamchukua Ibrahim na kuondoka naye, hata alipofika getini, walinzi wakaonekana kutokuwa na hofu, waliambiwa kuhusu mwanaume huyo, hivyo hata walipomuona Ibrahim wakahisi ndiye mwenyewe, wakamsalimia na kutokomea na mtoto huyo.

 

Je, nini kitaendelea?

Tukutane kesho.

Leave A Reply