The House of Favourite Newspapers

Linyanyue Penzi Lako Lililolegalega!

NI wiki nyingine mpenzi msomaji tunakutana tena katika Jamvi la XXLove ikiwa ni wiki ya pili ya mwezi wa kwanza ndani ya Mwaka wa 2018. Bila kujali mwaka jana ulikosana mara ngapi na mwenza wako, bila kuangalia mlipigana au kukaa vikao vingapi vya kusuluhisha ndoa yenu, kikubwa ni kujipanga kusawazisha penzi au ndoa yako ili mwaka huu uuanze vizuri na uumalize ukiwa salama salimini katika penzi lako.

Ni kweli kuna kuteleza kama binadamu, lakini kuteleza huko kukizidi, basi ujue una tatizo, tena tatizo kubwa ambalo linatakiwa kutafutiwa ufumbuzi wa haraka. Kama ulimkosea mwenza wako na ukashindwa au ukaona kuomba msamaha ni kujidharaulisha, basi utakuwa umekosea. Jitahidi kunyenyekea kwa yale yote uliyomkwaza na kumuumiza mpenzi wako kisha akakuambia ukweli. Kwa wale wanaume ambao mnajifanya ni vidume na bado mnaendekeza mfumo dume, kwenye mapenzi hakuna kitu kama hicho, kuwa mlaini, zungumza na mwenza wako kwa upendo na furaha. Kama utaendelea na mfumo wako wa ubabe na kiburi hata kama kweli umekosea, basi utakuwa si mtu mwema kwa mpenzi wako.

 

 

Hata kama mpenzi wako anakuvumilia, basi tegemea uvumilivu wake kufika mwisho na yeye kukuchoka kwa tabia zako. Mwaka huu jipange zaidi katika kupata mafanikio ya maisha na hata kwenye uhusiano wako wa uchumba au ndoa. Hata kama mnapendana vipi kwenye uhusiano, lazima mtasuguana, kuna wakati mtakwazana kwa sababu mbalimbali ama kwa maneno, vitendo au hisia. Haijalishi mwaka jana umegombana na umekwazana na mpenzi wako kwa kiasi gani, kama kweli unampenda na kumheshimu mwenza wako, basi hakikisha unajishusha na kurudisha uhai wa penzi lako.

 

Kama ulikuwa ni mwanamke ambaye uliona kabisa kuwa mienendo yako haikuwa sawa kwenye familia au penzi lako, basi jitahidi kurekebisha mapito yako kwa mwaka huu. Ndoa ni ngumu, inahitaji uvumilivu inahitaji kuelewana na kuridhiana kwa kila jambo. Kama ugomvi wako na mwenza wako ulikuwa ni kuchelewa kurudi nyumbani, basi hakikisha unawahi ili uondokane na hiyo karaha, lakini kama na mwaka huu utaendelea na tatizo hilo, bila shaka kuna namna hata kama ungekuwa ni wewe ungechukia. Kama mwaka ulioisha uliona kabisa ni kwa jinsi gani ndoa yako ilivyoyumbishwa na ulevi uliokithiri, basi achana na huo ulevi ili uinusuru ndoa yako, labda kama ulevi ni bora kuliko ndoa yako ndiyo uendelee nao.

 

Inawezekana wewe ni mmoja wa watu ambao ndoa zao ziliyumba sana kiasi cha kukaliwa vikao vingi vya ndugu na vya kidini na mwisho wa siku ndoa yako ikaponea chupuchupu kuvunjika, basi hakikisha Mwaka wa 2018 unautumia vizuri katika kunyanyua penzi lako ambalo lilikuwa limelegalega. Pamoja na yote hayo, bila nguvu na mkono wa Mungu katika kuijenga, kuilinda na kuidumisha ndoa yako, wewe kama mwanadamu ni ngumu sana kuifanya iwe bora. Mtegemee Mwenyezi Mungu kwa kila jambo katika maisha yako, unapokutana na mazito, basi muite yeye, mlilie yeye kwa sababu yeye ndiye kila kitu katika uso wa dunia hii.

 

Wiki hii ninakomea hapa msomaji wangu. Usikose wiki ijayo kwenye mada nyingine nzuri na tamu zaidi. Kwa maoni na ushauri, tembelea ukurasa wetu wa Mimi na Uhusiano kwenye Mtandao wa Kijamii wa Facebook, ni-follow Insta:@ mimi_na_ uhusiano au jiunge na M&U WhatsApp kwa namba ya hapo juu.

Comments are closed.