The House of Favourite Newspapers

Maambukizo katika kuta za ndani ya moyo

KATIKA mfululizo wa makala za magonjwa bado tunaendelea kuzungumzia magonjwa tofauti ya moyo, ambapo leo tutazungumzia maradhi ya moyo yanayotokana na maambukizi na tutaelezea maambukizi katika kuta za moyo.

Maambukizi katika kuta za ndani za moyo hutokea wakati vimelea ambavyo kwa kawaida huwa bakteria, vinapovamia kuta za ndani za moyo zikiwemo valve na kusababisha maambukizi.

Kwa kuwa katika moyo hakuna mishipa ya damu inayopeleka damu safi moja kwa moja kwenye valvu za moyo, hivyo chembechembe nyeupe za damu zinazoimarisha kinga dhidi ya maambukizi, hufika kwa shida sana kwenye valvu za moyo.

Pale vimelea au bakteria wanapotengeneza uoto kwenye valvu za moyo, hali hii husababisha chembe chembe nyeupe kuwa butu.

Kukosekana mishipa hiyo ya damu ambayo kazi yake ni kupeleka damu moja kwa moja kwenye valvu za moyo, hufanya matibabu ya ugonjwa huu kuwa mgumu, kwa kuwa ni vigumu dawa kufika kwenye eneo husika.

Maambukizi katika kuta za ndani za moyo yamegawanyika katika sehemu kuu mbili kutokana na jinsi ugonjwa unavyoanza.

Moja ni maambukizi ya kuta za ndani za moyo ya papo kwa hapo. Maambukizi hayo huanza kati ya siku hadi wiki kadhaa na mgonjwa huwa na hali mbaya au mahututi.

Aina ya pili ni maambukizi yasiyo ya hapo kwa hapo, katika kuta za ndani za moyo. Maambukizi haya huanza kati ya wiki hadi miezi kadhaa na dalili hutokea polepole.

Kuna vimelea vya aina mbalimbali ambavyo husababisha maambukizi katika kuta za ndani za moyo. Je, ni watu gani walio kwenye hatari ya kupata mambukizi katika kuta za ndani za moyo?

Watu walio katika hatari ya kupata ugonjwa huu ni pamoja na wale mbao walishaugua ugonjwa wa kisukari huko nyuma, akina mama wajawazito, watu wenye matatizo mengine ya valvu za moyo, kung’oa jino au meno na vilevile watu waliofanyiwa upasuaji mdogo wa kuwekewa kifaa cha kudhibiti mapigo ya moyo.

Inafaa kutambua kuwa kutokuwa na vihatarishi hivyo tulivyovitaja haimaanishi kwamba huwezi kuugua ugonjwa huo.

Dalili za ugonjwa huo ni pamoja na kuhisi homa na uchovu wa viungo, maumivu ya kichwa, kikohozi, kupumua kwa shida, maumivu ya kifua, vipele vinavyojulikana kama petechial rash ambavyo husababishwa na kuvuja damu katika mishipa ya ngozi na kusababisha madoa ya rangi nyekundu kwenye ngozi.

Huo ndiyo mwisho wa mada hii kuhusu tatizo la moyo, naamini utakuwa umeelimika vya kutosha.

Comments are closed.