The House of Favourite Newspapers

DENTI MWINGINE ATENGULIWA MKONO NA MWALIMU WAKE

MOROGORO: Wakati walimu wawili wa Shule ya Msingi ya Kibeta iliyopo Bukoba mkoani Kagera wakiburuzwa mahakamani wakidaiwa kumchapa viboko hadi kufa denti wa darasa la 5, Sperius Eradius, tukio lingine kama hilo limenaswa.  

 

Tukio hilo ni la denti wa Shule ya Sekondari ya Sumaye iliyopo Bigwa mkoani Morogoro, Vivian Alphonce kudaiwa kupigwa na mwalimu wake hadi kuteguka mkono na kumsababishia maumivu makali. Ilidaiwa kuwa, siku ya tukio denti huyo alirejea nyumbani akiugulia huku akidai kuwa, amechapwa na mwalimu hadi kuumizwa mkono wake.

 

Kufuatia hali hiyo, baba mzazi wa Vivian aliyefahamika kwa jina la Alphonce akiwa na mjomba wa mtoto huyo, walichukua hatua za kwenda shuleni hapo ili kujua kilichotokea.

 

Wakiwa sambamba na mwandishi wetu, wazazi hao walitinga ofisi ya mwalimu mkuu wa shule hiyo aliyefahamika kwa jina la Mwaluko na baada ya kusikiliza maelezo ya wazazi hao, mwalimu aliyedaiwa kuhusika na tukio hilo aliitwa na kutoa ufafanuzi huu;

”Vivian ni mtoto ambaye nampenda sana, nikiwa zamu huwa nampa madaraka ya kuwasimamia wenzake. Kweli jana ni miongoni mwa wanafunzi zaidi ya 10 tuliowachapa kwa kuchelewa na sijamchapa fimbo nyingi kama anavyodai na sijui kama alivunjika mkono, ndio naona sasa.

 

“Vivian sema ukweli, nimekupa adhabu ya viboko 4 mkononi wewe na wenzio na kama uliumia mkono, hapa shule tuna huduma ya kwanza kwa nini hukusema kama umeumia mkono? “Wazazi sisi walimu lengo letu tumjenge Vivian afanye vizuri shuleni, sasa akija shule saa 3 kipindi kimoja kimeisha siyo sawa,” alisema mwalimu huyo.

 

Baada ya maelezo hayo baba wa mtoto huyo alionesha kuelewa kilichotokea ambapo alimgeukia binti yake na kumsihi ajitahidi kuwahi shuleni huku pia akiwaambia walimu hao kumpa adhabu zinazostahili denti huyo kwa lengo la kumuweka sawa. Wakati mwandishi wetu anatoka ofisini kwa mwalimu mkuu, baba wa moto huyo alitakiwa kubaki na haikujulikana walichozungumza.

Kwa sasa mwanafunzi huyo amepata nafuu na anaendelea vizuri na masomo yake.

Stori: Dunstan Shekidele, Amani

Comments are closed.