The House of Favourite Newspapers

TUZO ZA SINEMA ZETU 2019 ZAZINDULIWA RASMI

Mtendaji Mkuu wa Azam Media, Tido Mhando akizungumza jambo wakati wa uzinduzi wa Tamasha la Sinema Zetu 2018, ndani ya Hoteli ya Serena iliyopo Posta jijini Dar es Salaam.

HATIMAYE Kituo cha Azam TV kupitia chaneli yake ya Sinema Zetu, leo Jumanne imezindua rasmi msimu mpya wa tuzo zao za Kimataifa za Sinema Zetu, ambapo Mtendaji Mkuu wa Azam Media, Tido Mhando, amesema taratibu zote za maandalizi kuelekea msimu huo mpya zimeshakamilika na kwamba zitaanza rasmi Januari Mosi, mwakani na kuhitimishwa Februari 23 katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.

Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo akielezea furaha yake baada ya kupewa jukumu la kuwa mlezi wa tamasha la tuzo hizo mwakani.

Akizungumzia maboresho ya tamasha hilo kwa msimu wa pili, Tido alisema, kwa kuwa mwanzo wao umeonekana kupokelewa vizuri na washiriki husika, mwakani watahakikisha mshiriki yeyote anawasilisha filamu iliyoandaliwa kuanzia mwaka 2016 hadi 2018, kwani hiyo ndiyo njia pekee inayoweza kuwapa picha halisi ya ufanisi na ubora wa uandaaji wa filamu.

Baadhi ya wasanii wa filamu wakifuatilia kwa umakini uzinduzi wa tamasha hilo mapema leo ndani ya Serena Hoteli, Posta jijini Dar es Salaam.

“Kila mtu anatakiwa kujua kuwa kwa sasa Kiswahili ni miongoni mwa lugha kumi kubwa kuzungumzwa Barani Afrika, hivyo tumeamua kufanya tamasha la tuzo hizi ili iwe njia moja ya kufikisha Lugha ya Kiswahili kwa watumiaji wapya kwani tuzo hizo zitashindanisha takribani mataifa yote ya Afrika ambayo yameshakubali kushirikiana nasi.

Baadhi ya waandishi wa habari na wageni waalikwa waliohudhuria uzinduzi huo wakiwa katika pozi la pamoja.

“Uwasilishaji wa kazi hizo utaanza mara moja Oktoba Mosi, mwaka huu mpaka Novemba 30, mwaka huu, mchakato wote huo wa upokeaji wa kazi za wasanii utakuwa chini ya COSOTA na Bodi ya Filamu Tanzania, huku mwenyekiti wa jopo la majaji atakuwa ni profesa Martin Mhando kwani ndiye aliyekuwa pia Mwenyekiti wa Tamasha la Kimataifa la Filamu Zanzibar,” alisema Tido.

Msanii wa Bongo Movies, Esha Buheti naye alikuwepo.

Katika hatua nyingine, Tido alimtambulisha Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo kuwa ndiye wamempatia jukumu la kuwa mlezi wa tamasha la tuzo hizo litakalofanyika Februari 23, mwakani.

Musa Mateja | GlobalHabariUpdates.

Comments are closed.