The House of Favourite Newspapers

TUNDA, ZARI ‘VITA NZITO’

WAKATI flani nikiwa likizo, nilikwenda kupumzika kijijini kwetu Mlalo- Lushoto mkoani Tanga. Lushoto ni kati ya maeneo ambayo watalii wengi wamekuwa wakipenda kwenda kwa sababu ya kuwa na vivutio mbalimbali.

Mimi nimesoma kule kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne lakini sikuwahi kujua kama kuna maeneo ya kitalii ambayo wazungu wangependa kufika kuangaza macho.

 

Hivi karibuni nilipofika, nikaenda sehemu flani ambayo ina maporomoko ya maji. Nikapiga picha, nikaposti kwenye ukurasa wangu wa Facebook.

Siku nyingine nikaenda kutembelea kwenye mapango ya mawe ambayo zamani enzi za vita, wazee wetu walikuwa wakienda kujificha pamoja na mifugo yao. Nazo nikatupia mtandaoni.

 

Nikapata likes nyingi na comments za kumwaga kutoka kwa marafiki zangu wa ndani na nje ya nchi. Baadhi wakataka nao watembelee maeneo hayo. Hivi ninavyoandika makala haya, mwezi Desemba nina marafiki wawili kutoka Uingereza watatua nchini na watafika Mlalo kutalii. Wengine ni wafanyakazi wenzangu ambao nao wameniomba niwape maelekezo ya jinsi ya kufika sehemu hizo.

Hapo ndipo nilipobaini nguvu yangu mimi kama mtu wa kawaida katika kuutangaza utalii wa ndani, sasa akifanya hivyo mtu maarufu itakuwaje?

 

Wakati mimi nikiwaza hivyo, kwa wanaotembelea mitandao ya kijamii, watakuwa wameona kile alichokifanya mwanamama Zarina Hassan ‘Zari’ kwenye ukurasa wake wa Instagram. Kama hujaona basi ni kwamba Zari hivi karibuni alitua nchini Uganda kwa ajili ya kutangaza vivutio vya kitalii vilivyomo nchini humo.

 

Sehemu kubwa ya post zake kwa sasa ni kuhusu ziara yake hiyo. Mashabiki wake wameonekana kuvutiwa na kile alichokifanya, pongezi zimekuwa nyingi. Baadhi wakasema, nguvu ya mwanadada huyo mjasiriamali inaweza kuipaisha sana sekta ya utalii Uganda.

Yapo maeneo ambayo nimeona Zari ametembelea, mimi nimeshawishika kwenda lakini kutokuwa kwangu na pesa ni kimekuwa kikwazo. Ila ninachoamini ni kwamba, baada ya promo hiyo aliyofanya, wapo watu wengi kutoka maeneo mbalimbali ya dunia watamiminika Uganda kwa ajili ya kutembelea maeneo yenye vivutio.

 

Najua, ziara yake nchini Uganda imegharamiwa na serikali kupitia Wizara ya Utalii kama ambavyo hata hapa Tanzania mastaa mbalimbali wamekuwa wakitumika katika kutangaza utalii wa ndani. Ila sasa najiuliza, kwani kwa mastaa wetu kutembelea sehemu za kitalii ni mpaka wapewe ofa na wizara au taasisi zinazohusika na mambo ya utalii nchini?

Nauliza hivyo kwa sababu, alichokifanya Zari kingeweza kufanywa hata na staa kama Irene Uwoya au Aunt Ezekiel, akaamua tu kwamba, safari hii badala ya kwenda kusherehekea siku yake ya kuzaliwa kwenye boti, achukue marafiki zake waende kwenye mbuga flani kutalii.

 

Akirudi, mapichapicha waliyopiga huko wakiyatupia kwenye mitandao ya kijamii, kwanza watakuwa wameinjoi lakini pia wamechukua nafasi yao kama mastaa kutangaza vivutio vyetu na kushawishi watu wa ndani na nje ya nchi nao kwenda, hatimaye kushiriki katika kuinua uchumi wa nchi. Nadhani ingekuwa kitu kizuri sana!

Vuta picha, Wema Sepetu na marafiki zake siku moja wanaamua tu kwenda kwenye mbuga za wanyama kama vile Mikumi, Serengeti au Manyara, matokeo yake yatakuwaje? Naamini matokeo yake yatakuwa mazuri sana lakini simuoni Wema kuwa na mawazo haya. Ingekuwa mimi ni Wema hata wizarani ningeenda, nikapeleka wazo langu kwamba nataka kuutangaza utalii uliopo Tanzania na naomba nipewe sapoti. Unadhani ningekataliwa? Sidhani!

 

Ila wema mwenyewe kwa kuwa ana ‘mambo mengi’ hawazi hilo badala yake tunawaona wadogo zake wakipambana na Zari yeye akiangalia.

 

Video Queen, Anna Kimario ‘Tunda’, amefanya jambo zuri kwa taifa lake! Wakati Zari anatupia picha kibao akiutangaza utalii wa Uganda, Tunda naye akawa amechafua ukurasa wake wa Instagram kwa mapicha kibao akiwa kwenye mbuga za wanyama za Manyara na Serengeti. Staa huyu anao wafuasi wengi, kupitia posti zake hizo wapo ambao watavutika na kutaka nao waende.

 

Huku ndiko tunakuita kuweka alama kwenye nchi yako. Tunda amekuwa na skendo mbalimbali, ana udhaifu wake kama binadamu lakini kwa hiki alichokifanya, iwe ni kwa sapoti ya mamlaka za utalii nchini au kwa pesa zake, anastahili kuigwa na mstaa wengine.

 

Niseme tu kwamba, nchi yetu ina vivutio vingi sana vya kitalii ukiachana na mbuga za wanyama. Ili watu wajue na watembelee, mimi na wewe tunatakiwa kupiga kelele sambamba na sisi kutembelea maeneo hayo. Hiyo itamfanya hata rafiki yako atamani kwenda lakini mwisho wa siku tunawashawishi hata walio nje ya nchi kuja kutalii.

JESHI USU LA WANYAMAPORI LAZINDILIWA, SERENGETI MARA – VIDEO

Comments are closed.