The House of Favourite Newspapers

Yanga Yamnasa Haruna Boban Yampa Gari

Haruna Moshi Boban.

YANGA imeonekana kupania kumaliza kipindi hiki cha usajili kwa kishindo baada ya kumshusha winga mwingine matata, huku wengine watatu wakitarajiwa kujiunga na timu hiyo haraka sana, akiwemo Haruna Moshi Boban.

 

Yanga inafahamika kuwa imekuwa ikilia shida tangu kuanza kwa msimu huu, lakini ajabu ni kwamba imeonekana kufanya usajili kabambe kuliko timu nyingine za Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwemo Simba.

 

Yanga imefanikiwa kumleta jijini Dar es Salaam winga wa Mwadui, Charles Ilanfya ambaye amekuwa akionyesha kiwango cha juu sana msimu huu, lakini usajili wao ambao jana ulioshtua sana ni huo wa mkongwe Boban.

Ilanfya alijiunga na Mwadui akitokea Mtibwa Sugar na msimu huu amefanya kazi kubwa ikiwemo kwenye mchezo dhidi ya Yanga ambao vijana hao wa Jangwani walishinda kwa mabao 2-1.

 

Juzi na jana, kiongozi mmoja wa Yanga alikuwa akitembea na winga huyo kwenye gari lake jijini Dar es Salaam, ikielezwa kuwa wanafanya hivyo kama ulinzi ili kuepuka kuhujumiwa na wapinzani wao.

“Yupo Dar na mazungumzo tumefanya naye, ishu imebaki kusaini na atafanya hivyo baada ya kumaliza mechi ambayo timu yake inayo, baada ya hapo atajiunga na wenzake moja kwa moja.

 

“Huyu ni chaguo la kocha na yeye ndiye alisema kuwa anamuhitaji kwenye kikosi na inaonekana kuwa kila kitu sasa kimekwisha,” kilisema chanzo chetu kutoka ndani ya Yanga.

Mbali na huyo, Yanga leo na kesho wanatarajiwa kumpokea kiungo Kenny Ally kutoka Singida United, ambapo atapewa mkataba wa miaka miwili na timu hiyo.

Kenny alikuwa akiwindwa na Yanga tangu msimu uliopita na mara kwa mara dili lake lilikuwa likishindikana, lakini taarifa zinasema kuwa siku yoyote kuanzia leo atasaini mkataba na timu hiyo.

Ally ambaye anatajwa kuwa mchezaji mahiri sana kwenye timu ya Singida, ameshakubaliana na Yanga kila kitu na nauli ameshatumiwa ambapo atasaini mkataba wake leo au siku chache kabla ya dirisha la usajili halijafungwa.

 

Mbali na huyo, mchezaji mwingine ambaye Yanga wanasubiri kumshusha ni Umar Kasumba, ambaye amewahi kuzichezea timu za Polisi na Villa zote za Uganda kwa sasa akiwa anaichezea Sofapaka ya nchini Kenya.

 

Yanga wanatarajiwa kumalizana na Mganda huyo wakati wowote kuanzia sasa ili aweze kumwaga wino kabla dirisha halijafungwa Jumamosi hii.

 

Mwingine ambaye anatarajiwa kupewa mkataba muda wowote ni Reuben Bomba raia wa DR Congo.

Bomba ambaye anacheza nafasi ya winga ameletwa na Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera.

 

Hata hivyo, jana jioni taarifa zilisema kuwa Yanga wamekamilisha dili kubwa la kiungo mahiri wa zamani wa Taifa Stars na Simba, Haruna Moshi Boban.

Hata hivyo, usajili wa Boban uliwachanganya wengi baada ya hivi karibuni kuelezwa kuwa amegoma kuichezea timu yake ya African Lyon baada ya kutolipwa mshahara wake wa miezi mitatu.

 

Boban ni kati ya wachezaji wakongwe nchini Tanzania na alishawahi kwenda kukipiga kwenye timu ya Gefle IF ya Denmark, lakini baadaye akavunja mkataba na kurejea Bongo.

 

“Boban tayari kila kitu, alishapewa gari na Yanga aina ya IST na atasaini mkataba wa miaka miwili.

“Sisi tunaamini kuwa atatusaidia na amefanya kazi kubwa sana akiwa na Lyon msimu huu, nafikiri kila kitu kitakamilika hivi karibuni, labda leo au kesho mambo yote yatakwisha na ataanza mazoezi na timu,” kilisema chanzo.

Comments are closed.