The House of Favourite Newspapers

A-Z Vifo vya mahujaji

0

Na Waandishi Wetu
BONGO ni vilio! Kufuatia Watanzania wanne mahujaji miongoni mwa 717 waliopoteza maisha kwa kukanyagana mjini Mina, Maka, Saudi Arabia, hapa Bongo vilio vinaendelea hasa kufuatia habari kuwa, miili ya marehemu hao haitarudishwa nyumbani kwa mazishi.

 Marehemu, Seif Salim Kitimla enzi za uhai wake.

Tukio la mahujaji hao kupoteza maisha lilijiri Alhamisi iliyopita wakati wa zoezi la kumpiga mawe shetani ikiwa ni sehemu ya nguzo kuu katika ibada ya hija kila mwaka nchini humo.Watanzania ambao mpaka sasa wamethibitishwa kupoteza maisha ni Mwanaisha Hassan Juma, Mkungwe Suleiman Hemed na Seif Salim Kitimla.

Mwanamke mwingine Mtanzania jina halijapatikana. Pia kuna raia mmoja wa Kenya, Fatuma Mohammed Jama ambaye alikwenda Maka kwa kutokea nchini.

Jijini Dar, Gazeti la Uwazi baada ya kupata taarifa hizo liliingia mtaani ili kupata nyumba zenye misiba kwa lengo la kuzungumza na wafiwa na kufanikiwa kufika katika msiba wa mmoja wa marehemu, Seif Salim Kitimla (59) ambapo hitima ya kumuombea ilifanyika nyumbani kwake Mtaa wa Chekeni Kijiji cha Mwasonga wilayani Temeke, Dar, Jumamosi iliyopita.

MTOTO WA MAREHEMU

Akizungumza na Uwazi Jumamosi iliyopita, mtoto wa tatu kati ya kumi wa marehemu Seif, Sinani Seif Kitimla alisema kifo cha baba yao kimewasikitisha sana na kwa mara ya kwanza hawakuamini kama amefariki dunia maana familia ilipata jina tofauti na walipofuatilia ndipo wakapata taarifa sahihi.

Mke wa marehemu Seif.

“Tangu baba ameondoka kwenda hija nilikuwa nikiwasiliana naye mara kwa mara. Mara ya mwisho tuliwasiliana Jumatano (iliyopita) jioni, nikampa taarifa ya huku nyumbani.”“Baada ya mazungumzo akaniambia kuwa, siku ya Alhamisi na Ijumaa hatakuwa hewani na simu ataiacha hotelini.

“Alinieleza hivyo kwa sababu siku hizo mbili ndiyo walikuwa wakienda huko (kumpiga mawe shetani). Lakini Ijumaa nilimpigia simu hakupatikana. Hapo tulishasikia habari zilizotokea huko na kupata jina lenye mkanganyiko.
“Ilibidi niende kazini kwake, Ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Tawi la Bandari kuulizia kama wana taarifa yoyote pia kuhakikisha jina.

“Kule nao walisema hakuna lolote ingawa walisema kama ni kweli ni pigo kwao. Baadaye tulikuja kuhakikisha kwa kufanya mawasiliano na Ofisi za Baraza Kuu la Waislam Tanzania (Bakwata) na Ofisi za Ubalozi wa Saudi Arabia ndiyo tukapata uhakika kwamba ni baba. Leo tumefanya sala na kila mmoja atatawanyika hapa, maana wanasema watazika hukohuko,” alisema mtoto huyo.

Mufti Zuberi.

Msiba mwingine wa Mwanaisha ulitajwa kuwa Buguruni, Dar lakini Uwazi lilipofika eneo hilo taarifa zilisema hakuna msiba kwa vile mwili wa marehemu hautarejeshwa nchini.

MAHUJAJI WALIOSALIMIKA

Ukiachia Watanzania hao kupoteza maisha, Bakwata imesema Watanzania wengine wapo salama na habari zaidi zitatolewa baadaye.Kwa mujibu wa Uwazi, Watanzania walionusurika wamo mchekeshaji maarufu nchini, Athuman Amiri ‘Mzee Majuto’, aliyekuwa Mbunge wa Tabora Mjini kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ismail Aden Rage, aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (Cuf), Ibrahim Lipumba na mchezaji wa zamani wa Timu ya Yanga, Sunday Manara.

Wengine ni mfanyakazi wa Shirika la Ugavi Tanzania (Tanesco), Fatuma Korongo, Mufti Mkuu wa Tanzania, Abubakar Zuberi, Shehe wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhadi Musa Salum, Shehe Musa Kundecha na wengine ambao majina hayakupatikana.

Idadi ya waumini wa Kiislamu (mahujaji) waliofariki dunia Septemba 24, mwaka huu, inaumiza na inatesa kihisia. Historia ya vifo vya aina hiyo, ni ndefu na ina maelezo yanayosikitisha. Jiji la Mina au Tent City liko umbali wa kilomita 5 kutoka mji wa Maka, Magharibi mwa nchi ya Saudi Arabia.

Serikali ya Saudi Arabia hutumia zaidi ya Dola Bilioni 60 kila mwaka kuimarisha miundombinu ya shughuli hiyo kama ukarabati wa misikiti. Pia, mambo ya kiusalama huimarishwa ambapo zaidi ya kamera za CCTV 5000 huwekwa kama tahadhari kwani zaidi ya mahujaji milioni 2 wanatajwa kuhudhuria shughuli hiyo takatifu ya kila mwaka.

Mina ni kitongoji chenye ukubwa wa eneo la mraba wa kilometa 20 katika eneo liitwalo Jamaraat. Kiimani eneo hilo ndipo mahujaji hurusha mawe kama ishara ya kuenzi kile ambacho Nabii Ibrahim alikifanya alipotokewa na mwovu shetani.

Hadi sasa inakadiriwa kuwa, zaidi ya watu 3,929 wamekwishafariki dunia kwa sababu mbalimbali huko Mina kwenye shughuli ya hija ikiwemo joto, kuangukiwa na ukuta, misongamano, moto kuunguza mahema na kukanyagana.
Miaka na idadi ya watu waliofariki dunia kwenye mabano ni kama ifuatavyo: Mwaka 1987 (400), 1990 (1400), 1994 (270), 1997 (350), 1998 (180), 2001 (35), 2004, (250), 2006 (362) kabla ya safari hii.

Waombolezaji wakiwa msibani.

Msemaji mmoja wa balozi ndogo ya Tanzania iliyopo mjini Mina alisema kukanyagana kwa mahujaji safari hii kulitokana kuachwa kwa utaratibu wa awali ambapo mahujaji huenda kumpiga shetani kwa awamu, lakini safari hii walikwenda kwa pamoja.

Ziko habari kuwa, ni utaratibu wa kiimani, mahujaji wanapofia Maka ambao ni mji mtakatifu huzikwa eneo hilohilo kwa maana ya kupata thawabu. Lakini hata hivyo, juzi serikali ya Iran ilikuwa ikifanya utaratibu wa kurudisha miili ya marehemu wake nchini Iran kwa mazishi.

Mungu aziweke pema peponi, roho za marehemu wote. Amina.
Imeandikwa na Makongoro Going,’ Haruni Sanchawa na Issa Mnally.

JIUNGE NA GLOBAL BREAKING NEWS!

Leave A Reply