Mwalimu avamiwa, akatwa koromeo

Makongoro Oging’ na Issa Mnally

UKATILI! Mwalimu Nelson Andrew (23), amevamiwa na watu wanaodaiwa kuwa ni vibaka na kumkata kwa kisu koromeo katika jaribio la kumtaka awape fedha la sivyo wangemuua.

Mwalimu Nelson Andrew akiwa na jeraha shingoni baada ya kujeruhiwa.

Akizungumza na Uwazi hivi karibuni, kaka wa mwalimu huyo, Andes Enock alisema tukio hilo lilijiri saa nane mchana wa Septemba 10, mwaka huu, wakati yeye na mjeruhiwa huyo wakipitisha biashara ya vyombo hatua chache kutoka kwenye nyumba wanayoishi.

Andes aliendelea kusema kwamba, wakiwa na mwalimu huyo walitoka nyumba aliyopanga wakiwa wamebeba vyombo vya ndani wakivitembeza mitaani kwa lengo la kuviuza huku wakisaidiana na mwalimu huyo katika biashara hiyo.
“Tulikuwa na mwalimu, mimi nilikuwa mbele yake huku tunaongea lakini kila nilipoongea hakuwa akinijibu.

ilipoangalia nyuma ndipo nikaona amepigwa kabali na kundi la vijana zaidi ya wanane huku amepitishiwa kisu shingoni na damu zikimtoka chapachapa. Alikabwa kiasi cha kushindwa kupiga kelele. Nilipouliza kuna nini, wale wahalifu walimwachia na kukimbia.

“Mwalimu alidondoka chini huku akizidi kutokwa damu nyingi. Nilitafuta usafiri na kumpeleka Kituo cha Polisi cha Mwinyijuma ambapo tulipewa PF 3 kisha tukamkimbiza Hospitali ya Mwananyamala ambapo madaktari walisema tatizo ni kubwa hivyo kumpeleka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

“Alifanyiwa uchunguzi na ikabainika kwamba alikuwa amekatwa koromeo. Alikuwa akipumua kwa shida hali iliyosababisha afanyiwe upasuaji na kulazwa kwa siku tano.“Mpaka sasa anapumua kwa shida ndiyo maana hospitali walimtoboa tundu kwenye koromeo, anashindwa kula, anakunywa uji tu tena kwa shida.

“Mdogo wangu ni mkazi wa Kijiji cha Nyanganga, wilayani Uvinza, Kigoma. Baada ya kumaliza masomo Chuo cha Ualimu Ndala, Tabora alikuja hapa kwangu akisubiri kupangiwa kazi. Niliona tusaidiane katika biashara ya kutembeza vyombo mitaani lakini kwa bahati mbaya akavamiwa na kujeruhiwa,” alisema Andes.

Hata hivyo, hali ya mwalimu huyo bado ni mbaya na anahitaji matibabu ya karibu lakini kinachowapiga chenga ni gharama kwa vile alikuwa hajaajiriwa.Hivyo kwa yeyote anayependa kumsaidia anaweza kutumia namba 0676 416378 au 0759 538451.

JIUNGE NA GLOBAL BREAKING NEWS!


Loading...

Toa comment