The House of Favourite Newspapers

ZITTO: Nimelipeleka Suala la CAG na Spika Jumuiya ya Madola -Video

Mbunge wa Kigoma Mjini na Kiongozi wa chama wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe (kushoto) akiongea na wanahabari leo jijini Dar.

Kiongozi wa chama wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, amesema kufuatia mvutano mkubwa uliojitokeza kati ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Mussa Assad, ameamua kulifikisha suala hilo kwa katibu mkuu wa mabunge ya Jumuiya ya Madola (CPA) kwa hatua zaidi.

 

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Zitto amesema alichukua uamuzi huo Januari 9, mwaka huu kwa sababu Spika Ndugai alikuwa amevunja katiba kwa kuingilia uhuru na mamlaka ya CAG, kama ibara ya 143 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na tayari barua yake imeshajibiwa.

 

Zitto ameendelea kueleza kwamba katika majibu aliyopewa na Katibu Mkuu wa Mabunge ya Jumuiya ya Madola (CPA), Akbar Khan mwenye ofisi yake nchini Uingereza, suala hilo limefikishwa kwa mwenyekiti wa mabunge ya jumuiya ya madola, Emilia Lifaka kwa ajili ya kujadiliana na Spika Ndugai juu ya namna ya kulishughulikia suala hilo, bila kuvunja katiba ya nchi.

 

Pia Zitto ameendelea kueleza kwamba, licha ya hatua hiyo, pia yeye na wabunge wenzake watano, wamefungua kesi ya kikatiba kutaka tafsiri ya sheria juu ya mamlaka ya spika kuingilia ofisi ya CAG.

 

“Pia kupitia mwanasheria wetu, Fatma Karume tumepeleka mahakamani shauri kutaka tafsiri ya kisheria juu ya mamlaka ya spika na pia kuitaka mahakama imzuie CAG kuitikia wito wa Kamati ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge,” amesema Zitto.

Comments are closed.