The House of Favourite Newspapers

Penzi Lisiloisha  043

0

Mapenzi ya dhati aliyonayo Jafet kwa Anna, yanamfanya awe tayari kufanya chochote kumsaidia msichana huyo. Licha ya tofauti kubwa ya hali zao kiuchumi, Anna akitokea kwenye familia ya kitajiri na kijana huyo akitokea kwenye familia ya kifukara, mapenzi yao yanashamiri kadiri siku zinavyozidi kusonga mbele.

Awali, Jafet alikuwa akisomeshwa na kanisa kwa makubaliano kwamba akimaliza masomo atajiunga na mafunzo ya upadri kwa ajili ya kulitumikia kanisa, lakini baadaye anabadilisha uamuzi na kukataa kwenda kusomea tena upadri kutokana na jinsi alivyokuwa anampenda Anna.

Siku zinazidi kusonga mbele huku wawili hao wakizidi kupendana mno. Baada ya Jafet na Anna kuhitimu kidato cha nne, Anna anaanza maandalizi ya kutafuta shule ili wakasome pamoja kidato cha tano na sita, gharama zote zikiwa ni juu yake kwani wazazi wa Jafet hawakuwa na uwezo wa kumsomesha.

Msichana huyo anafanya kila kinachowezekana na hatimaye wawili hao wanajiunga kidato cha tano kwenye shule moja, bila wazazi wa Jafet kujua chochote. Baadaye Anna anaanza kuumwa figo, baada ya kuhangaika sana Jafet anaamua kumtolea figo moja, wanasafiri hadi India ambako wanafanyiwa upasuaji na msichana huyo kuwekewa figo nyingine kutoka kwa Jafet.

Zoezi hilo linafanyika kwa mafanikio makubwa kisha wanarejea Tanzania. Wiki kadhaa baadaye, wazazi wa Anna wanamshinikiza Jafet awapeleke nyumbani kwa wazazi wake ili wakawashukuru kwa wema wake, anakuwa mgumu lakini baadaye anakubali, wanafunga safari mpaka kijijini Rwamgasa.

Wazazi wa Anna wanashangazwa mno na hali duni na umaskini uliokithiri wanayoikuta nyumbani kwa akina Jafet. Wanarejea jijini Mwanza na siku zinazidi kusonga mbele, hatimaye vijana hao wanahitimu kidato cha sita lakini mama yake Anna hampendi tena Jafet na anafanya kila kinachowezekana kuwatenganisha wawili hao.

Anna anatafutiwa chuo nchini Marekani kisha anapelekwa bila hata kuagana na Jafet, jambo ambalo linamuumiza mno kijana huyo kutoka familia ya kimaskini. Moyo wake unabaki na majeraha makubwa yasiyopona.

Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Yalikuwa ni mateso makali, kifua chake kiliuma mno kiasi kwamba wakati mwingine alihisi kikiwaka moto. Alikuwa mtu wa kulia kwa maumivu makali huku wazazi wake wakifanya kila liwezekanalo kuwapata wazazi wa Anna ili wazungumze nao lakini majibu yalikuwa tofauti na walivyotegemea, simu haikuwa ikipatikana kabisa.

Hawakuchoka, hawakukata tamaa, waliendelea zaidi na zaidi lakini matokeo hayakubadilika, kama ilivyokuwa mara ya kwanza ndivyo ilivyokuwa mara hiyo, simu haikupokelewa.

Hawakutaka kupoteza muda wao tena, mioyo yao iliwauma kwa kuwa walijua kwamba watu hao hawakutaka kusikia lolote lile kutoka kwao na iliwezekana kabisa kwamba simu ile ilivyokuwa ikiita, waliiona ila hawakuona umuhimu wa kuipokea.

Walimpenda kijana wao na hawakutaka kuona akifa na wakati walikuwa na uwezo kidogo wa kumsaidia. Walichokifanya ni kumchukua na kumpeleka hospitali japokuwa mifukoni mwao hawakuwa na fedha za kutosha.

Njiani, bado Jafet alikuwa akilia tu, mbali na mapenzi ambayo yaliufanya moyo wake kuwaka moto lakini bado kifua kilimuuma mno, alitembea kwa shida mpaka barabarani ambapo daladala ilipokuja, wakapanda na kuelekea mjini.

“Jafet, vumilia, Mungu atakuponya,” alisema mama yake huku akibubujikwa na machozi, kwa kumwangalia tu, ungeona ni jinsi gani mwanamke huyo aliumia baada ya kuona kijana wake akiteseka.

“Mama! Nahisi nitakufa,” alisema Jafet kwa sauti ya kukata tamaa.

“Kufa? Hauwezi kufa Jafet, hauwezi kufa,” aliingilia baba yake, alisema maneno ya kijasiri, alimtaka kijana wake kutokutaka kukata tamaa, alitakiwa kupambana na ugonjwa uliokuwa ukimsumbua.

Safari iliendelea zaidi, abiria wote waliokuwa ndani ya gari lile walibaki wakimwangalia Jafet ambaye alilalamikia maumivu makali. Kila mmoja alimuonea huruma, hawakujua alikuwa nani, aliumwa nini lakini jinsi alivyokuwa akilalamika kutokana na maumivu makali aliyokuwa nayo, walijikuta huruma ikiwaingia.

Walichukua dakika arobaini na tano ndipo wakafika hospitalini ambapo moja kwa moja wakampeleka mapokezi, wakaandikiwa na kuchukua kadi kisha kusubiri katika benchi ambapo zamu yao ingefika baada ya dakika kadhaa.

“Mtoto wenu anaumwa nini?” aliuliza nesi mmoja huku uso wake ukionyesha huzuni.

“Anasumbuliwa na kifua nesi.”

“Sawa! Hebu mleteni huku,” alisema nesi yule, hapohapo Jafet akachukuliwa na kupelekwa katika chumba ambacho daktari alimhitaji.

****

“Ushawahi kusoma kitabu cha shairi kilichoandikwa na mwandishi William Shakespeare?” aliuliza William.

“Kipi?”

“Wewe unakijua kipi?”

“Hamlet, Macbeth na King Lear,” alijibu Anna.

“Ulishawahi kukisoma Romeo And Juliet?”

“Nimekisikia, nimekitafuta ila sikukipata,” alijibu Anna.

“Nitakutafutia.”

“Kuna nini na hicho kitabu?”

“Wakati mwingine nimekuwa nikikaa na kufikiria kuhusu huyu mtu aliyeitwa Romeo, ni kama ninamuona mbele yangu, aliamua kupenda, alikuwa tayari kugombana na mtu yeyote lakini si kuona akimpoteza Juliet, wazazi wake waligombana na wazazi wa Juliet kwa kuwa tu kila upande ulikuwa tajiri ila pamoja na hayo, wawili hawa hawakuachana, kila siku Romeo alimuonyeshea Juliet jinsi alivyompenda, hata kwa Juliet ilikuwa hivyohivyo,” alisema William na kuendelea:

“Anna, nimekuwa nikikwambia mara kwa mara kwamba ninakupenda, sijajua kwa nini, sijajua hasa kile kinachokufanya kunikataa zaidi ya kukuona mara kwa mara unalia, kinachokufanya kulia, hutaki kuniambia, nikikwambia nakupenda na kukuhitaji, unanikataa na kulia, hivi kwa nini?’ aliuliza William huku akimwangalia Anna usoni.

“Kawaida tu,” alijibu Anna.

“Hakuna mtu anayelia kawaida, ni lazima kuna kitu, niambie nijue, niambie naweza kukufariji Anna,” alisema William kwa sauti ya chini na yenye kubembeleza.

“Hapana! Hakuna kitu.”

“Una uhakika?”

“Ndiyo!”

William alijua fika kwamba anadanganywa lakini hakutaka kuuliza zaidi, alijua kwamba mbali na maisha yaliyokuwa yakiendelea nchini Marekani lakini kulikuwa na kitu kilichomsumbua sana Anna kichwani mwake.

Alitaka kukijua kitu hicho kwa kuamini kwamba hiyo ndiyo ingekuwa pointi yake ya kwanza kabisa kuanzia safari yake ya kumfanya msichana huyo akubaliane naye na hatimaye wawe wapenzi.

Anna alijaribu kuwa msiri, hakutaka mtu yeyote afahamu kilichoendelea moyoni mwake. Siku hiyo walitembea sana ndani ya bustani hiyo huku William akijitahidi kumchangamsha Anna lakini msichana huyo hakuchangamka ipasavyo, na kama alitoa tabasamu, halikuwa lile litokalo moyoni, lilikuwa tabasamu bandia.

“Anna, can you be my only Juliet?” (Anna, unaweza kuwa Juliet wangu pekee?) aliuliza William, alikuwa amemshika Anna mkono.

“It’s impossible William,” (Haiwezekani William) alisema Anna kwa sauti ndogo yenye kumaanisha.

“Why?” (Kwa nini?)

“I can’t fall in love, let me be your BFF,” (Siwezi kuangukia kwenye mapenzi, acha niwe BFF wako)

“Best Friend Forever?” (Rafiki wa karibu milele)

“Yes!” (ndiyo)

William akashusha pumzi ndefu. Jibu la Anna, hakika lilimchanganya.

 Je, nini kitaendelea? Usikose kufuatilia siku ya Jumatano kwenye Gazeti la Risasi Mchanganyiko.

Leave A Reply