The House of Favourite Newspapers

Mabilionea Wasio na Huruma-45

0

DK Viola na nduguye Vanessa ambao hivi sasa ni mabilionea kwa fedha haramu wakiwa wameua watu wengi duniani, ikiwemo kuangusha ndege na kulipwa kiasi kikubwa cha fedha kama fidia ya watoto 62 waliokufa katika ajali hiyo ya ndege, wanasakwa kila kona ya dunia ili waweze kufikishwa mahakamani kwa mauaji.

Kazi ya upelelezi alikabidhiwa Inspekta Masala, Mtanzania aliyejipatia sifa kubwa duniani kwa kuchunguza masuala yenye utata, pia alipewa wapelelezi wengine kadhaa kumsaidia lakini wote wameuawa mjini Bangkok ikiwa ni pamoja na daktari aliyewafanyia Dk Viola na Vanessa upasuaji wa kubadilisha sura.

Inspekta Masala amegundua kabisa kuwa Dk Viola na Vanessa ndiyo wanaoendesha mauaji ya wapelelezi wake na anajua anayefuata kuuawa ni yeye. Akitokea nyumbani kwa marehemu Jen, mwanaume aliyebadilisha jinsia kuwa mwanamke ambaye alipiga picha na Dk Viola na Vanessa, Inspekta Masala ametekwa na watu wasiojulikana na kupelekwa hadi ufukweni ambako mwili umetupwa majini ukiwa hauna kichwa ili watu wasimtambue marehemu.

 Baada ya zoezi hilo waliomteka wanaelekea nyumbani kwa tajiri Juan Lee, ambako wamepakia mzigo kwenye ndege yake binafsi ambayo imeruka kuelekea Washington.

Mvuvi Mita Govan amefika ufukweni kukagua mitego yake, anagundua badala ya kunasa samaki, mtego una maiti ya mwanaume aliyekatwa kichwa, yeye na wenzake wanaamua kupiga simu polisi kuwajulisha juu ya tukio hilo.

 Je, polisi watafanya nini? Mzigo uliopakiwa ndani ya ndege ni mzigo gani?

 SONGA NAYO…

 Hallow!”

“Ndiyo.”

“Hapo ni polisi?”

“Ndiyo.”

“Kuna mtu amekufa na kutupwa majini!”

“Hapo ni wapi?”

“Patoyo.”

“Una uhakika na unachokisema?”

“Kabisa.”

“Kweli maana kuna watu huwa wanatusumbua tukifika eneo la tukio unakuta hakuna chochote.”

“Hiyo niliyokupigia nayo ni namba yangu ya simu, ninaitwa Mita Govan, siwezi kusema uongo halafu nikakutajia jina langu halisi, inavyoonekana waliomuua walikuja na gari na kulitelekeza hapa ufukweni karibu kabisa na mahali ambapo nafanyia shughuli zangu za uvuvi!”

“Tunakuja!”

Simu ikakatwa na Mita pamoja na wenzake wakabaki wamesimama kando ya mwili wa mtu aliyeonekana kuwa mwanaume, ambao ulitoa harufu mbaya sababu ya kuharibika. Ilibidi wavumilie mpaka polisi wafike, maana wao ndiyo walikuwa wahusika wakuu, dakika ishirini na tano baadaye, magari mawili ya polisi yalifunga breki karibu kabisa na mahali walipokuwa wamesimama, askari wakashuka wakiongozana na mwanamke aliyevalia koti jeupe akiwa amening’iniza mabegani kifaa cha kupimia kifua na moyo ambacho madaktari  hukitumia kugundua matatizo ya wagonjwa kwa kusikiliza.

“Hamjambo?” askari aliyeonekana kuwa kiongozi wa wenzake aliwasalimia.

“Hatujambo kabisa.”

“Nani amekuwa mtu wa kwanza kuuona huu mwili?”

“Mimi.” Mita aliitikia na baadaye kutoa maelezo ya namna alivyokuta umenasa kwenye mtego wake wa samaki.

“Hili gari?”

“Tumelikuta hapa.”

“Mmeugusa?”

“Hapana.”

Askari walianza kuzunguka huku na kule wakiangalia alama fulani fulani juu ya ardhi na kuchora ramani ya eneo la tukio kwenye karatasi na ilipobidi walimuuliza Mita maswali mengi ili kukamilisha maelezo yao, walipomaliza zoezi hilo walimruhusu daktari kuuchunguza mwili naye kuchukua maelezo yake na mwisho walipekua mifukoni mwa marehemu, wakatoa kitambulisho peke yake.

“Mh! Huyu Inspekta Masala siyo yule aliyeripotiwa kwamba amepotea siku tatu zilizopita? Mbona kitambulisho kimeandikwa jina hilo?”

“Inawezekana, hata hili gari lililoegeshwa hapa ni la kampuni ya Bangkok Tours, ambao kwa maelezo yao walidai alilikodisha kwao, aisee kuna watu wamemuua na wakaja mpaka hapa kumtupa majini! Hili ni tukio la kusikitisha sana!” mmoja wa askari alijibu.

Hapakuwa na ubishi tena kwamba mwili ule wa mtu aliyeuawa na kukatwa kichwa ulikuwa ni wa mpelelezi maarufu duniani Inspekta Masala, wote walisikitika, ikabidi waubebe kwenda nao hadi mjini Bangkok ambako ulipelekwa moja kwa moja kwenye hospitali ya jeshi kuhifadhiwa kabla haujafanyiwa uchunguzi wa ndani wa kidaktari.

Kikao kiliketi haraka sana kwenye Makao Makuu ya Shirika la Upelelezi la Thailand, wakijadili juu ya kilichotokea, hasa mauaji ya wapelelezi waliokuwa wakifuatilia kesi ya Dk Viola na nduguye Vanessa, mwisho kabisa walikubaliana kuwa watu wote hao waliuawa na mtu mmoja ambaye kazi ya kumtafuta ilitakiwa kuendelea mpaka kuhakikisha anatiwa nguvuni, upelelezi ulikuwa sasa umezaa upelelezi mwingine.

Taarifa zilipotumwa Makao Makuu ya Scotland Yard nchini Uingereza, CIA na Interpol nchini Marekani, hapakuwa na mshtuko mkubwa sana uliosababishwa na kifo cha Inspekta Masala, badala yake uongozi wa shirika hilo ulitoa kauli  moja tu ya “mzikeni” na jambo hilo likafanyika kwenye makaburi ya Halmashauri ya Jiji la Bangkok bila kiongozi yeyote wa Scotland Yard, CIA wala Interpol kuhudhuria, kitendo hicho kiliwashangaza watu wengi ukizingatia heshima ambayo Inspekta Masala alikuwa nayo duniani.

Vyombo mbalimbali vya habari duniani vilitangaza juu ya kifo cha mpelelezi huyo maarufu duniani, hata mitandao ya kijamii ilijaa habari zake watu wakifafanua na kuelezea juu ya kazi alizozifanya na kuwalaani CIA na Scotland Yard kwa namna walivyouchukulia msiba wake kwa uzito mdogo.

Nchini Tanzania ulikuwa ni kama msiba wa taifa, rais wa nchi hii alituma salamu za rambirambi kwa familia ya Inspekta Masala kijijini kwao Bupandwamhela wilayani Sengerema ambako karibu kila mwananchi aliyemfahamu alikuwa akilia kwani Masala aliwapenda sana wananchi wa kijiji chake na aligusa maisha ya watu wengi.

Walisikitika kwa sababu hawakupata nafasi ya kuuona mwili wake kwa mara ya mwisho na kuuaga, walitamani mazishi yake yangefanyika kijijini kwake lakini walipopewa taarifa jinsi mwili ulivyoharibika ilibidi wakubaliane na hali halisi ya kuomboleza bila kuona mwili wa ndugu yao.

“Twalumelile no!” (Tumeumia sana!) aliongea mzee Musa Ngamira kwenye msiba nyumbani kwa Inspekta Masala ambako wananchi walikusanyika.

“Tutaliba!”(Hatusahau!) alijibu mzee mwingine maarufu kwa jina la Sahani ama vijana wengi walimwita ‘pleti’ ambaye alikuwa rafiki mkubwa sana wa Inspekta Masala kijijini pale.

***

Saa sabini na mbili baadaye, ndege aina ya Gulfstream 550GS ilianza kushuka angani kuelekea kwenye Uwanja wa Ndege wa Washington Abraham Lincolin Army Base, ulikuwa ni uwanja wa Jeshi la Wananchi wa Marekani uliotumiwa na jeshi hilo peke yake au na ndege za masuala ya kiusalama, hasa yaliyohusisha shirika la kijasusi la nchi hiyo; CIA.

Watu zaidi ya hamsini, wengi wakiwa ni viongozi wa CIA, Interpol na Scotland Yard walikusanyika sehemu maalum ambapo ndege hiyo ilitegemewa kusimama, wote walikuwa wakijiandaa kumpokea mtu muhimu, walivyoonekana ni kama vile walikuwa wakimtarajia Papa wa Vatican, dakika kumi baadaye ndege iligusa ardhi na baadaye kuserereka mpaka mahali ambapo ilisimama kabisa, watu wote hamsini wakasogea karibu kabisa na ndege hiyo wakisubiri mlango ufunguliwe.

Ulipofunguliwa walitoka watu watatu, wawili wakiwa wamemshikilia mmoja aliyeonekana dhaifu na amechoka, wakamsaidia kushuka hadi chini kwa kutumia ngazi maalum ya kushukia kwenye ndege, alipokanyaga chini tu alinyoosha mkono wake na kusalimiana na Mkurugenzi wa CIA aliyekuwa mbele kabisa.

“Welcome to America Mr. Masala!”(Karibu Marekani bwana Masala!)

“Thank you so much! I can’t  believe I am alive, the whole world knows I am dead.”(Ahsante sana! Siamini niko hai, dunia nzima inaamini mimi ni marehemu)

“We had to fake your death because you are dealing with dangerous people the world has never had!”(Ilibidi tujifanye umekufa kwa sababu watu unaopambana nao ni hatari mno, kuliko watu wote hatari ambao dunia imewahi kuwa nao!)

“Sure, but I am ready to start the second phase! I have to pin these people down and bring them before justice”(Hakika, lakini niko tayari kuanza muhula wa pili, hawa watu lazima niwapate na niwafikishe mbele ya sheria!)

“That is what we are looking forward to see!”(Hicho ndicho tunachosubiri kushuhudia!)

Je, nini kitaendelea? Nini kimetokea mpaka Inspekta Masala kuwa hai wakati dunia nzima inafahamu ni marehemu? Fuatilia wiki ijayo siku ya Jumatatu katika Gazeti la Championi Jumatatu.

Leave A Reply